1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Ujerumani yasisitiza kuendelea kutoa misaada Ukraine

Hawa Bihoga
14 Agosti 2023

Waziri wa masuala ya fedha Ujerumani amesema wataendelea kuiunga mkono Ukraine katika kutoa misaada endelevu, wakati taifa hilo likiendelea kupambana na vikosi vya Urusi ambavyo vinashambulia maeneo muhimu.

https://p.dw.com/p/4V8K4
Ukraine | Christian Lindner in Kiew
Picha: Thomas Imo/photothek/IMAGO

Ikiwa ndio ziara yake ya kwanza mjini Kyiv tangu uvamizi wa Urusi mwaka uliopita, waziri wa fedha Christian Lindner amesema atafanya mazungumzo muhimu na maafisa wa ngazi za juu wa Ukraine.

Mazungumzo hayo yatalenga namna wizara ya fedha Ujerumani, itakavyoweza kusimama bega kwa bega, ikiwemo kutoa misaada muhimu na endelevu kwa Ukraine.

"Tunasimama upande wa Ukraine, bega kwa bega," Lindner aliwaambia waandishi wa habari baada ya kuwasili Kyiv kwa treni.

Soma pia:Kansela wa Ujerumani Scholz apongeza juhudi za amani Ukraine

Tangu uvamizi wa Urusi mnamo Februari 2022, Ujerumani imetoa euro bilioni 22  kwa Ukraine katika msaada wa kibinadamu, kifedha na kijeshi.

Ujerumani bado ipo chini ya shinikizo

Ziara hiyo inafanyika wakati Ujerumani ikiwa chini ya shinikizo kutoka kyiv, ikitaka itume makombora ya masafa marefu aina ya Taurus ili kuongeza ufanisi wake katika uwanja wa mapambano dhidi ya vikosi vya Urusi.

Litauen l Nato-Gipfel in Vilnius l Ukrainischer Präsident Selensky
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyyPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Hata hivyo serikali ya Ujerumani hadi sasaimepinga maombi hayo, kwa wasiwasi kwamba makombora hayo yanaweza kufika katika ardhi ya Urusi na kuuchochea mzozo huo uliodumu kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

Soma pia:Zelensky asifia mifumo ya ulinzi ya Marekani, Ujerumani

Mykhailo Podolyak, msaidizi mkuu wa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, aliliambia gazeti la Bild la Ujerumani kwamba makombora ya Taurus yalikuwa "muhimu" kwa mapambano ya Ukraine.

Amewaondoa wasiwasi washirika hao muhimu kwamba makombora hayo yatatumika "pekee katika eneo la Ukraine, ndani ya mipaka inayotambulika kimataifa ya 1991".

Waziri huyo wa masuala ya fedha Ujerumani Lindner amewasisitizia waandishi wa habari kwamba lazima Ukraine ishinde vita hivyo.

Wataendelea kutoa misaada kadri inavyohitajika na kadri inavyowezekana, alisisitiza mazunguzo ya Kyiv hayatalenga tu hali ya sasa isipokuwa na hata hapo baadae.

"Ukraine lazima ishinde vita hivi," waziri Lindner alisema.

Urusi yashambulia maeneo ya kimkakati

Katika uwanja wa mapambano mamlaka ya Ukraine imesema, Urusi imeendelea na mfululizo wa mashambulizi yake ya anga usiku kucha.

Katika mji wa bandari wa Odesa leo Jumatatu, hatua ambayo imewajeruhi wafanyakazi watatu wa duka kubwa la mahitaji ya chakula.

Aidha Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amesema katika eneo la Kherson nako vikosi vya Urusi vimeshambulia hadi katika maeneo ya raia.

Amesema vikosi vya Urusi vinavyokalia kwa mabavu vimeendelea kushambulia maeneo yetu hasa Kherson

"Kuna waliokufa, kuna waliojeruhiwa.Kijiji cha Veletenske kilipigwa makombora."

Aliongeza kuwa nyumba moja iliteketea kwa moto. Mvulana alijeruhiwa, ana majeraha makubwa ya moto na sasa yuko katika uangalizi maalum.

Soma pia:Zelensky ameapa kulipiza kisasi baada ya kuuwawa watu wanne karibu na Kherson

Urusi imekuwa ikizuia mauzo ya nafaka ya Ukraine kupitia bandari ya Odessa na bandari zingine za Bahari Nyeusi tangu katikati ya mwezi Julai, kufuatia kujiondoa katika makubaliano ya nafaka na Ukraine, na tangu wakati huo imekuwa ikishambulia  kwa nguvu, maeneo ya kimkakati hasa bandari.

Athari za vita vya Ukraine kwa watumiaji wa ngano Afrika