1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela wa Ujerumani Scholz apongeza juhudi za amani Ukraine

13 Agosti 2023

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amepongeza mkutano wa kilele ulioongozwa na Saudi Arabia kuhusu kupatikana amani na kumaliza mapigano nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/4V7Jv
Berlin direkt - Sommerinterview mit Bundeskanzler Olaf Scholz
Picha: Thomas Kierok/ZDF/dpa/picture alliance

Katika mahojiano yake ya kila mwaka ya msimu wa kiangazi na televisheni ya Ujerumani ya ZDF, Scholz amesema ni vyema kwa jamii ya kimataifa kuendeleza mazungumzo, kwa sababu yanaongeza mbinyo kwa Urusi kufahamu kuwa imeuchukua mkondo mbaya na kwamba lazima iwaondoe askari wake Ukraine na kutoa nafasi ya kupatikana amani.

Soma pia: Mkutano wa kimataifa juu ya Ukraine wamalizika Jeddah

Wawakilishi kutoka karibu nchi 40 zikiwemo China, Ujerumani, India na Marekani zilishiriki katika mazungumzo ya mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Jeddah, ijapokuwa Urusi haikualikwa. Mazungumzo sawa na hayo ya kimataifa ya kujadili mkondo wa kupatikana amani Ukraine yalifanyika pia mjini Copenhagen, Denmark mwezi Juni.