1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoUfaransa

EURO 2024: Mbappe avunjika pua katika ushindi wa Ufaransa

18 Juni 2024

Shirikisho la soka la Ufaransa FFF limesema kuwa Kylian Mbappe hatohitaji kufanyiwa upasuaji lakini atavaa barakoa maalum atakaporejea uwanjani baada ya kuvunjika pua katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Austria.

https://p.dw.com/p/4hAtM
Euro 2024 Austria - Ufaransa
Kylian Mbappe( kulia) akishangilia na Ousmane Dembele baada ya beki wa Austria Maximilian Wober kujifunga mwenyewe Picha: Hassan Ammar/AP Photo/picture alliance

Bao la kujifunga la Maximilian Woeber lilitosha kuipa Ufaransa ushindi katika mechi yao ya kwanza ya michuano ya Kombe la mataifa ya Ulaya dhidi ya Austria.

Woeber alijifunga mwenyewe kunako dakika ya 38 ya mchezo baada ya kujaribu kuokoa krosi ya Kylian Mbappe. 

Austria, iliyo chini ya kocha Ralf Rangnick iliamka usingizini kipindi cha pili na kubuni nafasi kadhaa za kufunga bao japo kipusa wa bahati hakuwa upande wao.

Soma pia: Maamuzi ya VAR kufafanuliwa kwa mashabiki katika Euro 2024 

Hata hivyo, nyota Kylian Mbappe aliondolewa uwanjani katika za mwisho baada ya kupata jeraha la pua alipogongana na beki wa Austria Kevin Danso.

Rais wa shirikisho la soka la Ufaransa FFF Philippe Diallo amewambia waandishi wa habari kuwa, Mbappe hatohitaji kufanyiwa upasuaji.

Kocha wa Ufaransa Didier Deschamps amesema ameridhika na ushindi huo japo amewahimiza wachezaji wake kuwa makini hasa katika safu ya ushambuliaji.

Belgium v Slovakia Group E - UEFA EURO 2024
Wachezaji wa Ubelgiji wakisherehekea baada ya Romelu Lukaku kufunga baoPicha: Vincent Kalut/IMAGO

Ushindi huo unaiweka Ufaransa alama tatu sawa na Uholanzi iliyoipiga Poland 2-1 katika mechi ya Jumapili. Vijana wa Didier Deschamps wanakutana na Uholanzi mnamo siku ya Ijumaa mjini Leipzig huku Austria ikivutana mashati na Poland mjini Berlin.

Na katika dimba la Deutsche Bank Park, Slovakia imeionyesha kivumbi Ubelgiji baada ya kuifunga 1-0 katika mechi ya kundi E.

Soma pia: Ufaransa, England zapigiwa upatu kubeba Euro 2024 

Ivan Schranz aliifungia Slovakia bao la kipekee na la ushindi kunako dakika ya 7 ya mchezo na kuwakata maini vijana wa kocha Domenico Tedesco.

Kipigo hicho kilikuwa cha kwanza kwa Ubelgiji katika mechi 16 chini ya kocha mpya Domenico Tedesco na kurudisha kumbukumbu ya kampeni yao mbaya wakati wa Kombe la Dunia la FIFA nchini Qatar.

Ujerumani itamudu kufanya maajabu Kombe la Euro 2024?

Hata hivyo, mabao mawili ya mshambuliaji Romelu Lukaku yalifutwa na teknolojia ya video VAR baada ya kukutwa ameotea na baadae Lois Openda kuunawa mpira kuelekea kupatikana kwa bao la pili.

Slovakia sasa imeungana na Romania kileleni mwa kundi E baada ya kuibamiza Ukraine 3-0 katika mechi ya mapema iliyochezwa mjini Munich. Ubelgiji inayo fursa ya kujikomboa watakapoteremka uwanjani siku ya Jumamosi kuzipiga na Romania mjini Köln.

Leo ni zamu ya Uturuki kuonyeshana ubabe na Georgia kabla ya Ureno kumaliza udhia na Jamhuri ya Czech.