1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAfrika Kusini

Waliokufa kwenye mkasa wa moto Afrika kusini waongezeka

31 Agosti 2023

Idara ya huduma ya usimamizi wa masuala ya dharura Afrika Kusini, imesema moto uliozuka usiku wa kuamkia leo, katika jumba la ghorofa tano nchini humo, umesababisha vifo vya watu 73 wakiwemo watoto 7 mjini Johannesburg.

https://p.dw.com/p/4VoUM
Afrika Kusini |  Johannesburg
Wafanyakazi wa zimamoto katika eneo la mkasa wa moto mjini Johannesburg, Afrika KusiniPicha: Shiraaz Mohamed/REUTERS

Akiandika katika mtando wake wa X uliokuwa unajulikana kama Twitter, Robert Mulaudzi, msemaji wa idara hiyo ya huduma ya usimamizi wa masuala ya dharura amesema watu wengine 52 walijeruhiwa katika mkasa huo.

Mulaudzi amesema watu wengi wameondolewa katika jengo hilo. 

Mgcini Tshwaku,  afisa mmoja wa usalama nchini humo amesema jengo hilo lilikuwa limekaliwa kiharamu.

Amesema kwa kawaida huwa hakuna umeme katika majengo kama hayo na inashukiwa kwamba moto wa mishumaa ama moto uliotumika kupikia huenda ukawa chanzo cha kuzuka kwa moto huo. 

Soma pia:Janga la moto lauwa watu zaidi ya 70 Afrika Kusini

Mpaka sasa hakuna uchunguzi rasmi uliyofanyika na kubaini hasa kile kilichotokea.

Idadi ya waliokufa imeongezeka kidogo kuanzia 70 hadi 73 baada ya moto huo kuanza mapema leo Alhamisi katika jengo hilo.

Idadi zaidi ya walioangamia huenda ikapanda kufuatia maafisa wa uokoaji kwenda ghora moja hadi nyengine kuwatafuta wahanga wa mkasa huo. 

Rais Ramaphosa atuma salamu za pole

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema mkasa huo uliosababisha mauaji ya wengi ni mkubwa huku akisema yuko pamoja na familia zilizofikwa na janga hilo.

Meya wa mji wa Johannesburg Kabelo Gwamanda, pia ametuma salamu zake za rambirambi kwa familia zinazoomboleza.

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa Picha: Stanislav Krasilnikov/TASS/dpa/picture alliance

Soma pia:Afrika Kusini: Moto wauwa zaidi ya watu 60 wengine kujeruhiwa

Mablanketi na mashuka bado yalionekana katika madirisha yaliyopiga weusi kufuatia moto huo, yaliyotumiwa na baadhi ya watukuruka nje kujaribu kujiokoa.

Baadhi ya walioshuhudia walisema baadhi ya wazazi waliwatupa watoto wao nje ya madirisha yaliyokuwa wazi baada ya kukosa matumaini ya kuukwepa moto huo.

Ndani ya jengo hilo wafanyakazi wa dharura walikutana na miili iliyokuwa imerundikana katika mlango uliokuwa umefungwa ili kuwazuia polisi kuingia ndani.  

Huduma za afya katika eneo la mkasa

Wafanyakazi wengine walionekana wakiwasaidia manusura wa mkasa huo waliokuwa na majeraha ya moto na walioonekana kuwa na maumivu makali.

Noma Mahlalela aliye na miaka 41 mkaazi wa katika jengo hilo amesema hali iliyoonekana asubuhi ya leo ilikuwa ya kusikitisha miili ilikuwa imetapakaa kila mahali mingine ikiwa imechomeka vibaya isiyoweza kutambulika. 

Soma pia:Watu 15 wafariki kwenye ajali ya moto kiwandani, Ufilipino

Nae Kenny Bupe aliyenusurika amesema walikuwa wakikimbizana ndani ya jengo kutafuta mahali pa kutokea.

Amesema alikuwa miongoni mwa watu waliovunja milango na kukimbilia eneo salama.

Kenny aliyekwenda katika jengo hilo kumtembelea rafiki yake ameongeza kuwa wengi walikufa kufuatia kuvuta moshi wenye sumu. 

Afrika Kusini iliyo na uchumi mkubwa wa kiviwanda, ina idadi kubwa ya wahamiaji ambao wengi wao hawajasajiliwa kutoka mataifa mengi ya Afrika. 
 

Moto wateketeza mali soko la Karume kwa mara nyingine