1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Papa Francis awasili nchini Papua New Guinea

6 Septemba 2024

Papa Francis amewasili nchini Papua New Guinea baada ya kuhitimisha ziara yake nchini Indonesia. Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani ameanza mkondo wa pili ya safari yake ya siku 12 katika eneo la Asia-Pasifiki.

https://p.dw.com/p/4kMpm
Indonesia | Ziara ya Papa Francis katika mji wa Jakarta
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa FrancisPicha: Tatan Syuflana/AP Photo/picture alliance

Baada ya kuongoza Misa iliyohudhuriwa na umati watu wapatao laki moja katika uwanja wa mpira wa Gelora Bung Karno, mjini Jakarta, nchini Indonesia,  kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amewasili salama salmini nchini Papua New Guinea, kuendelea na ziara yake ndefu zaidi nje ya nchi anayofanya kwa lengo la kuwafikia Wakatoliki katika pembe za mbali za dunia.

Indonesia Jakarata | Zaidi ya waumini 80.000 wahudhuria Misa
Papa Francis alipokuwa anaingia katika uwanja wa mpira wa Gelora Bung Karno mjini Jakarta.Picha: Indonesia Papal Visit Committee

Ziara hiyo ya siku tatu nchini Papua New Guinea katika mji mkuu wa Port Moresby, Papa Francis atakukutana na viongzi wa nchi hiyo, jumuiya za kiraia na viongozi wa makanisa.

Soma Pia: Papa, Imamu wa Indonesia waonya dhidi ya uchochezi wa kidini 

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani mwenye umri wa miaka 87 anafanya ziara ya tatu tangu aanze majukumu ya kulitumikia kanisa katoliki kama Papa katika taifa hilo lenye watu milioni 12, wengi wao wakiwa Wakristo.

Ni Papa wa pili kuzuru nchini Papua New Guinea, baada ya aliyekuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Mtakatifu Yohane Paulo wa pili aliyezuru nchi hiyo mnamo mwaka 1984.

Papua New Guinea| Waziri Mkuu James Marape
Waziri Mkuu wa Papua New Guinea James MarapePicha: Julia Nikhinson/AP Photo/picture alliance

Papa Francis pia atashiriki katika misa ya Jumapili kabla ya kuondoka kuelekea mji wa Vanimo kwa ajili ya kukutana na wamisionari wa Kikatoliki.

Papua New Guinea, taifa mwanachama wa Jumuiya ya Madola ambalo lilikuwa koloni la nchi jirani yake Australia, hadi lilipopata uhuru mnamo mwaka 1975, ni nchi kubwa iliyozungukwa na milima, misitu na mito ni nchi ambayo ina watu wa makabila ya mengi ya kiasili. Makao makuu ya Kanisa Katoliki Vatikan, yanakadiria kuwa kuna takriban Wakatoliki milioni 2.5 nchini humo.

Soma Pia: Papa ahimiza kujikinga na misimamo mikali

Akiwa nchini Papua New Guinea, ajenda ya Papa Francis inaambatanishwa zaidi na vipaumbele vyake vya kimkakati ambavyo ni haki ya kijamii na kuondoa umaskini ambavyo ni muhimu sana kwa taifa hilo la Kusini - Pasifiki na nyumbani kwa zaidi ya watu milioni 10, wengi wao wakiwa ni wakulima wadogo wadogo.

Papua New Guinea | Maporomoko katika mkoa wa Enga
Watu wa Papua New Guinea katika eneo la Enga lililokumbwa na maporomoko mnamo Mai 24,2024Picha: STR/AFP/Getty Images

Kiongozi wa kanisa katoliki duninai Papa Francis katika ziara yake hii anatoa wito wa umoja wa kidini na anawahimiza watu kupanda mbegu za upendo, kufuata njia ya mazungumzo kwa ujasiri, kuendelea kuonyesha wema na kuwa wajenzi wa umoja na amani.

Baada ya ziara ya nchini Papua New Guinea Papa Francis ataelekea katika nchi za Timor Mashariki na Singapore.

Vyanzo: AP/AFP