1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUganda

Museveni, kuongoza NAM kwa miaka mitatu ijayo

19 Januari 2024

Mataifa yanayounda muungano usiofungamana na upande wowote NAM yamezitaka nchi tajiri kutokandamiza juhudi zao za maendeleo.

https://p.dw.com/p/4bTUG
Yoweri Musevini - Rais wa Uganda
Rais wa Uganda Yoweri Museveni baada ya kutawazwa kuwa mwenyekiti mpya wa NAM na kutoa wito wa mshikamano zaidi baina ya mataifa wanachama ili kufanikisha azma yaoPicha: ABUBAKER LUBOWA/REUTERS

Ratiba ya Siku ya tano ya mkutano wa kilele wa mataifa yasiyofungamana na upande wowote kwa kifupi NAM imekuwa ya kikao cha marais na viongozi wa ngazi za juu ambapo Rais Museveni wa Uganda alitawazwa kuwa mwenyekiti mpya wa NAM kwa miaka mitatu ijayo.

Museveni ametoa hotuba yake ya kwanza kwa kuchambua chanzo cha muungano huo wa mataifa 120 akisema bado haujafanikisha maazimio ya waasisi wake kutokana na hila za mataifa tajiri ya Ulaya na Marekani.

"Halafu mtu anasema hili ndilo wazo sawa, usipokubaliana nalo tutakushambulia… kweli? Unawezaje kudai kuwa wewe ni mwanademokrasia ilhali unawachukulia wengine kama watumwa. Kwa hiyo nguvu za NAM ziwe katika kuwa sauti moja hasa kwenye jukwaa la Umoja Mataifa," alisema Museveni.

Umoja wa Mataifa wakosolewa kwa kuwa dhaifu

Makamu wa rais wa Cuba Salvador Valdes Mesa ameunga mkono mtazamo wa Museveni huku akionya juu ya hatua za mwendelezo za kuyawekea masharti mataifa yanayoendelea ili kupata misaada na mikopo ambazo amesema huyadhoofisha kiuchumi, na hizo zikiwa ni hila za makusudi.

Uturuki I Cevdet Yılmaz
​​​​Makamu wa Rais wa Uturuki Cevdet Yilmaz katika mkutano wa NAM nchini Uganda, ameukosoa Umoja wa Mataifa kwa kushindwa kutumiza wajibu wake kutokana na kukandamizwa na Marekani na Ulaya.Picha: Metin Aktas/AA/picture alliance

Makamu wa rais wa Uturuki Cevdet Yilmaz kwa upande wake ameukosoa Umoja Mataifa kwa kutotumia mamlaka yake kulinda haki za wanyonge kiuchumi na kijamii hali inayofungua milango ya mizozo akiuangazia ule wa Israel na Hamas.

"Umoja Mataifa umepooza kutokana na udhaifu na kukandamizwa na mataifa mengine na ndiyo maana hata umeshindwa kushinikiza juu ya amani ya kudumu Mashariki ya Kati haiwezekani bila kuutatua mzozo kati ya Israel na Palestina," alisema.

Soma pia:Umoja wa Mataifa: Hali Ukanda wa Gaza inatisha

Aidha amesema NAM ndilo jukwaa la kipekee kwa mataifa yanayoendelea kujenga msingi wa ushirikiano wa kiuchumi na kujenga mazingira nafuu ya biashara na uwekezaji miongoni mwao. 

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika, Mousa Faki Mahamat amekariri kuwa bara hilo litazidi kujenga mshikamano na mataifa mengine kama njia ya kujikomboa dhidi ya ukoloni mamboleo.

Muungano wa Nchi zisizofungamana na upande wowote uliundwa mnamo mwaka 1955 mwanzoni mwa vita baridi kwa lengo la kutoa jukwaa kwa mataifa yaliyokuwa yakipinga shinikizo la kuchukua upande kati ya kambi mbili duniani moja ikiongozwa na Marekani na nyingine uliokuwa Muungano wa Kisovieti.

Mkutano wa kilele wa mjini Kampala unamalizika Jumamosi ambapo maazimio yatasomwa huku mkutano mwingine wa kundi la G77 na China ukianza ili kujadili mikakati zaidi ya ushirikiano wa kiuchumi na uwekezaji.