1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUganda

Museveni atetea kutiwa saini kwa sheria dhidi ya ushoga

1 Juni 2023

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ametetea kutiwa saini kwa moja ya sheria kali zaidi duniani dhidi ya ushoga inayohusisha adhabu ya kifo na kusema ilihitajika kuzuia watu wa jamii hiyo kuwarubuni wengine kujiunga nao

https://p.dw.com/p/4S3K0
Uganda Kampala | Präsident Yoweri Museveni
Picha: SNA/IMAGO

Matamshi hayo ya Museveni ni ya kwanza tangu alipotia saini kuwa sheria mswada huo na kuzua lawama kali kutoka mataifa ya Magharibi pamoja na vitisho kutoka kwa rais wa Marekani Joe Biden na wadau wengine vya kukatizwa kwa msaada kwa Uganda miongoni mwa vikwazo vyingine.

Museveni asema hakuna atakayewatingisha 

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Museveni Jumatano jioni, imesema wakati wa mkutano na wabunge wa chama chake cha National Resistance Movement NRM, rais huyo alisema kuwa mchakato huo wa kutiwa saini umekamilika na hakuna atakayewatingisha. Museveni ameongeza kuwa chama cha NRM hakijawahi kuwa na lugha mbili na kwamba kile kinachosema mchana ndicho kinachosema usiku.

Museveni aonya dhidi ya ushoga

Kiongozi huyo wa NRM pia amewaambia wabunge wake kwamba kabla ya kutia saini muswada huo, alifanya mashauriano ya kina kujaribu kuamua iwapo ushoga ulitokana na maumbile na akashawishiwa na wataalamu kwamba huo sio ukweli na badala yake ushoga unatajwa ni matokeo ya "kuchanganyikiwa kisaikolojia". Museveni amesema na namnukuu...."tatizo ni kwamba ndio umechanganyikiwa. uko na tatizo binafsi. Sasa usijaribu kuwalaghai wengine. ukijaribu kufanya hivyo, tutakuandama na kukuadhibu." Pia amesema kuwa iwapo mtu atamkamata mtoto na kumbaka, atauawa na kwamba anaunga mkono kikamilifu suala hilo.

Wanaharakati watoa wito wa vikwazo dhidi ya Museveni

Wakimbizi waliotoroka Uganda kutokana na sheria dhidi ya ushoga ya mwaka 2014
Wakimbizi wa Uganda wanaojihusisha na ushoga katika kambi ya Kakuma Picha: Sally Hayden/ZUMA/imago images

Wanaharakati wa Uganda wametoa wito kwa wafadhili wa kimataifa kumuwekea vikwazo kiongozi huyo kutokana na sheria hiyo. Katika taarifa ya pamoja siku ya Jumatatu baada ya mswada huo kutiwa saini kuwa sheria, makundi ya kutetea haki yalilaani sheria hiyo waliyoitaja kuwa hatari na ya kibaguzi ambayo itaendelea kukandamiza uhuru wa kijamii chini ya uongozi wa Museveni ambao wamesema umezidi kuwa wa kidikteta tangu alipochukuwa uongozi mwaka 1986.

Jamii ya kimataifa yamuonya Museveni

Umoja wa Ulaya na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, pia wameikosoa sheria hiyo na kuonya kuwa msaada wa kigeni na uwekezaji nchini Uganda huenda ukakabiliwa na utata iwapo sheria hiyo haitafutiliwa mbali. Mnamo mwaka 2014, wafadhili wa kimataifa walikatiza msaada kwa Uganda baada ya Museveni kuidhinisha mswada ulionuia kuweka hukumu ya maisha gerezani kwa mahusiano ya kimapenzi ya jinsia moja ambao baadaye ulibatilishwa.

Sheria mpya ya sasa , inatoa hukumu ya maisha gerezani kwa tendo la ngono la jinsia moja na miaka 20 jela kwa kupigia debe ushoga. Sheria hiyo pia inasema kuwa taasisi ikiwemo vyombo vya habari na mashirika yasiokuwa ya serikali yanayopigia debe ushoga, yatatozwa faini kali.