1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kitisho cha kuongezeka kwa mashambulizi ya droni Moscow

Mikhail Bushuev Iddi Ssessanga
30 Agosti 2023

Anga ya jiji la Moscow siyo shwari tena, wakati droni za Ukraine zinaulenga mara kwa mara mji mkuu huo wa Urusi. Wakati mbinu hiyo ni ya kimkakati, inaweza kuashiria mabadiliko katika mkakati wa Ukriane kuhusu mzozo huo.

https://p.dw.com/p/4Vkrc
Urusi l droni ya Ukraine yagonga jengo Moscow.
Wachunguzi walichunguza jengo lililoharibiwa mjini Moscow baada ya kugongwa na droni mnamo Agosti 2023.Picha: Shamil Zhumatov/REUTERS

Usiku wa Mei 3, ndege zisizo na rubani mbili zilizokuwa na vilipuzi ziliruka bila kizuizi juu ya Moscow, na kugonga kubwa la jengo la Seneti ya Kremlin. Shambulio hilo la kwanza kabisa la ndege zisizo na rubani kwenye mji mkuu wa Urusi, ambalo kuna uwezekano mkubwa liliratibiwa na Ukraine, lilileta pigo kubwa la ishara kwa Urusi.

Tangu wakati huo, mashambulizi ya ndege zisizo na rubani mjini Moscow yameongezeka mara kwa mara. Kituo cha Biashara cha Kimataifa cha Moscow, ambayo ni wilaya ya majengo marefu ya kibiashara ziliko wizara mbili za Urusi, imepigwa mara nne. Wiki iliyopita, Moscow ilikumbwa na mashambulizi ya takriban kila siku ya ndege zisizo na rubani.

Kulingana na Wizara ya Ulinzi ya Urusi, kitu cha kuruka kisichokuwa na rubani kutoka mashariki kilidunguliwa karibu na Moscow siku ya Jumatatu. Maafisa wa Urusi walisema ndege mbili zisizo na rubani za Ukraine zilidunguliwa kwenye maeneo ya Tula na Belgorod siku moja baadaye.

Mashambulizi ya droni hutimiza malengo mengi

Wachambuzi wanasema Ukraine inatekeleza malengo kadhaa na mashambulizi yake ya ndege zisizo na rubani. Mojawapo ni "kutuma ujumbe mzito na wa wazi kwa ulimwengu na raia wake kwamba Ukraine haijakaa bila kufanya kitu bali inajibu uchokozi wa Urusi," mtaalamu wa kijeshi wa Israel Sergey Migdal aliiambia DW.

Shambulio linalodaiwa kuwa la droni dhidi ya jengo la seneti ya Kremlin.
Picha mnato iliyochukuliwa kutoka vidio ikionesha kitu kinachoruka kikilipuka karibu na jengo la seneti ya Kremlin mnamo mwezi Mei.Picha: Ostorozhno Novosti/REUTERS

Ulrike Franke, mtaalam wa ndege zisizo na rubani na teknolojia ya kijeshi kutoka Baraza la Mahusiano ya Kigeni la Ulaya mjini Paris, alisema uvamizi huo pia unatoa uhakika kwamba vita hivyo haviko mbali sana na vinaweza kuja Urusi.

Soma pia: Urusi na Ukraine zaendelea kushambuliana kwa kutumia droni

Migdal alisema mashambulizi hayo yameweka shinikizo kwa Urusi kuhamisha mifumo zaidi ya ulinzi wa anga kutoka mstari wa mbele hadi Moscow. Mashambulizi ya anga yanayoendelea yanaweza pia kuibua hisia zisizofikiriwa, za vurugu, za kupaparika kutoka kwa Urusi, kama vile "kuzamisha meli ya Uturuki kutokana na kuchanganyikiwa, ambayo inaweza kusababisha mvutano mkubwa na Rais wa Uturuki Erdogan, jambo ambalo Urusi inataka kuliepuka," Migdal aliongeza.

Mashambulizi hayo ya ndege zisizo na rubani yanazidi kulazimisha mamlaka ya Moscow kufunga anga ya eneo hilo. Siku ya Jumatatu, viwanja vya ndege vya Moscow vilisimamisha kwa muda safari zote za ndege huku kukiwa na vitu vya angani vilivyoingia visivyo na rubani.

Mashambulizi hayo ya ndege zisizo na rubani yanazidi kulazimisha mamlaka ya Moscow kufunga anga ya eneo hilo. Siku ya Jumatatu, viwanja vya ndege vya Moscow vilisimamisha kwa muda safari zote za ndege huku kukiwa na vitu vya angani vilivyoingia visivyo na rubani.

Levin alisema hii "bila shaka" inafanya kazi. Shirika la ndege la Turkmenistan, kwa mfano, tayari limesimamisha safari zote za ndege kwenda Moscow hadi taarifa nyingine.

Kituo cha Biashara cha Moscow
Wilaya ya Kituo cha Biashara ya Kimataifa cha Moscow, imelengwa na mashambulizi kadhaa ya droni.Picha: Valery Sharifulin/Tass/dpa/picture alliance

Kufikia sasa, kubaini kiwango cha uharibifu uliosababishwa na uvamizi huu kwa sekta ya usafirishaji ya Urusi na trafiki ya anga bado ni changamoto, kulingana na Franke, kwa sababu viwanja vingi vya ndege ulimwenguni siku hizi vinalazimika kusimamisha shughuli kwa muda kutokana na kuonekana kwa ndege zisizo na rubani.

Lakini mambo yangezidi kuwa magumu zaidi ikiwa ndege zisizo na rubani za Ukraine zingepiga uwanja wa ndege wa kiraia wa Moscow, na kuharibu njia za ndege, vituo au hata ndege ya abiria.

"Kisha mashirika ya ndege ya kigeni yangeanza kukwepa Moscow hadi vita viishe, kama baadhi yanavyofanya," Migdal alisema.

Ulinzi dhaifu wa anga Moscow?

Wataalamu hawakubaliani juu ya jinsi mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Ukraine dhidi ya Moscow yanavyofanikiwa, na jinsi ulinzi wa anga wa mji mkuu huo unavyoshikilia, kwani ukweli bado hauko wazi.

Soma pia: Ukraine yazishambuliwa Moscow, Crimea kwa droni

"Hatujui ni droni ngapi ambazo kwa kweli zimezuiwa," Franke alisema kama mfano, na kuongeza kuwa itakuwa mbaya kusema "mashambulizi haya ni rahisi" kufanya. Anaamini kuwa pande zote mbili zinabadilika kulingana na uwezo wa kila mmoja katika aina fulani ya mchezo wa paka na panya.

Hata hivyo, ukweli kwamba ndege zisizo na rubani zinafika Moscow ni "tatizo" kwa Urusi, mtaalamu wa kijeshi wa Israel David Sharp aliiambia DW. "Kwa kweli, mashambulio kama hayo yanapaswa kudhibitiwa kwenye mpaka na Ukraine au juu ya ardhi ya wazi, sio mara baada ya droni kuingia jijini."

Mifumo ya ulinzi wa anga ya Moscow bado ni dhaifu, ingawa jiji hilo lilipaswa kuwa eneo lenye ulinzi bora zaidi nchini Urusi tangu enzi ya Usovieti, Mykhailo Samus, mtaalam wa kijeshi wa Ukraine aliyeko Prague, aliiambia DW. Mifumo ya ulinzi wa anga ya Urusi, alisema, inalenga "lengo la kawaida," kama vile makombora ya masafa marefu, badala ya vitu vidogo vinavyoruka kama vile UJ-22 za Ukraine na Bober, au droni za "Beaver."

"Vitu vidogo kama hivyo hutengenezwa kwa nyenzo zenye mchanganyiko badala ya chuma, hufuata mifumo changamano ya ndege na hivyo kutoa changamoto kwa mfumo wowote wa ulinzi wa anga," alisema Samus. Wataalamu wanasema mapungufu ya ulinzi wa anga pia yapo katika eneo pana karibu na mji mkuu wa Urusi.

Jengo la Wizara ya Ulinzi ya Urusi mjini Moscow
Mfumo wa ulinzi wa anga umewekwa kwenye paa la jengo la wizara ya ulinzi mjini Moscow.Picha: picture alliance / NurPhoto

"Ili kudungua shabaha, lazima kwanza uitambue. Hili litafanywa na vituo vya rada, ambavyo kwa hakika vinapaswa kuwa sehemu ya uwanja jumuishi wa rada," alisema Samus. "Lakini tunaweza kudhani kuwa Urusi haina uwanja huo wa rada. Mifumo yake ya ulinzi wa anga hugundua vitu mmoja mmoja lakini haifikii eneo lote."

Soma pia: Urusi yaituhumu Ukraine kufanya mashambulizi ya droni Moscow

Waukraine, kwa hivyo, wanarusha droni ili kuona vituo vya rada na, baada ya kubaini mapungufu, hurusha ndege zaidi "za ndani kabisa ya eneo la Urusi, ambapo kuna mifumo michache ya ulinzi wa anga kuliko katika maeneo ya mpakani," Samus alielezea.

Kulingana na Migdal, ndege isiyo na rubani ikishafika Moscow, mamlaka ya Urusi inaweza tu kutumia ulinzi wa mwisho kama vile mfumo wa makombora ya masafa mafupi ya Pantsir. Hata hivyo, alisema mifumo ya ulinzi wa anga ina sekunde 15 hadi 30 pekee ili kuondoa droni zinazoingia kabla ya kufikia shabaha yake.

Je, Ukraine itapanua kampeni yake ya droni?

Ukraine haina silaha za masafa marefu kama vile makombora ya Urusi yanayoongozwa na Kalibr na makombora ya kasi kubwa zaidi ya Kinzhal. Kwa kuzingatia udhaifu huu wa kimbinu, Ukraine inatumia mashambulio ya ndege zisizo na rubani badala yake, alisema Migdal.

Soma pia: Marekani yaonya Urusi kuwa makini katika urushaji ndege zake

Kwa kuwa nyingi ya ndege hizo hubeba kilo chache za vilipuzi, "mashambulizi ya droni yana umuhimu mdogo, kwani hayataondoa viwanja vya ndege vya Urusi, wala jeshi la anga la Urusi," Migdal alisema. "Kwa kweli, mashambulizi ya drone yanafaa zaidi kwenye mstari wa mbele."

Vita vya Ukraine | Mashambulizi ya droni mjini Moscow.
Droni pia zimeshambulia majengo ya makaazi mjini Moscow.Picha: Maxim Shemetov/REUTERS

Wataalamu wanatabiri kuwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Ukraine dhidi ya Moscow yataongezeka licha ya ufanisi wao mdogo. "Hii ni hatua ya ufunguzi," alisema Sharp, akiongeza kuwa shambulio la drones 25 kwa wakati mmoja lingeashiria awamu mpya kabisa.

"Itakuwaje ikiwa badala ya tatu, droni 33 au 300 zingerushwa kutoka pande zote," Migdal alisema. Ukraine inaweza kutumia mashambulizi kama haya kuzima kabisa viwanja vya ndege vya Moscow, kwa mfano, kuashiria ushindi muhimu kwa Kiev. Hili, Migdal aliongeza, lingeilazimisha Kremlin kufikiria upya ni mwelekeo gani inataka vita viende, "iwe hayo ni maelewano na mazungumzo, au kujibu kwa ghafla na kwa nguvu bila mazingatio yoyote."

Makala hii ilitafsiriwa awali kutoka Kijerumani