1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yadungua droni mbili zilizolenga Moscow

Angela Mdungu
26 Agosti 2023

Urusi imeripoti kuwa mji mkuu Moscow, ulishambuliwa na droni usiku wa kuamkia Jumamosi hali iliyosababisha kufungwa kwa muda kwa viwanja vikubwa vya ndege vya mji huo.

https://p.dw.com/p/4VbgJ
Polisi wakiwa katika eneo lililoshambuliwa na droni mjini Moscow
Polisi wakiwa katika eneo lililoshambuliwa na droni mjini MoscowPicha: AP Photo/picture alliance

Mapema Jumamosi 26.08.2023, Meya wa Moscow Sergei Sobyanin alisema kuwa ndege isiyo na rubani ilidunguliwa na mifumo ya ulinzi wa anga katika wilaya ya Istra mjini Moscow. Wilaya hiyo iko umbali wa kilometa 50 kutoka Kremlin.

Shirika la habari la serikali la Urusi TASS limeripoti kuwa, viwanja vya ndege vya Sheremetyevo, Domodedovo na Vnukovo vililazimika kukatisha safari za ndege kwa saa kadhaa.

Soma zaidi: Urusi yazima shambulio jingine la droni mjini Moscow

Katika mkoa wa Belgorod unaopakana na Ukraine, gavana Vyacheslav Gladkov alisema kuwa mifumo ya anga iliaangusha droni karibu na kijiji ca Kupino. Hakuna majeruhi wala uharibifu ulioripotiwa kutokana na shambulio hilo. Hata hivyo amesema watu wanne walijeruhiwa kwenye kijiji kingine cha Urazovo baada ya Ukraine kufanya mashambulizi.

Alichapisha picha zinazoonesha uharibifu katika majengo. Ukraine haikupatikana kwa haraka kuzungumzia mashambulizi hayo na mara nyingi haisemi hadharani kuwa inahusika kwa mashambulizi ndani ya Urusi. Mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani kusini mwa Urusi yamekuwa yakifanwa mara kwa mara kwa miaka mingi.

Urusi yashambulia Kharkiv

Katika hatua nyingine, watu wawili wameuwawa baada ya majeshi ya Urusi kukishambulia kijiji karibu na mji wa Kupiansk Kaskazini Mashariki mwa Kharkiv. Mamlaka mjini Kupiansk ambako ni kilometa sita kutoka uwanja wa mapambano zimekuwa wakiwataka wananchi wanaoishi karibu na mji wahame tangu mwanzoni mwa mwezi Agosti wakati Urusi ilipoongeza mashambulizi yanayolenga kulidhibiti eneo hilo.

Uharibifu uliotokana na shambulio la droni mjini Moscow
Uharibifu uliotokana na shambulio la droni mjini MoscowPicha: picture alliance/AP

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Telegram, gavana wa mkoa wa Kharkiv, Oleh Synehubov akizungumzia tukio hilo lililosababisha vifo hivyo ameandika kuwa mashambulizi hayo ya adui yaliulenga mgahawa mmoja ambapo wakaazi walioathiriwa na tukio hilo walikuwemo ndani yake. Ameongeza kuwa mtu mmoja amejeruhiwa katika tukio hilo. 

Jeshi la Urusi hivi karibuni lilisema kuwa linasonga mbele karibu na eneo hilo ambalo lilirejea mikononi mwa Ukraine mwaka uliopita ingawa sasa linakabiliwa na mashambulizi mapya.

Kyiv ilianza kujibu mashambulizi mwezi Juni  ili kuyarejesha maeneo yake yaliyonyakuliwa, lakini imesema kuwa inatambua kuwepo kwa mapambano magumu wakati ikipigana kupenya kwenye ngome za Urusi zilizodhibitiwa vilivyo.

Reuters/ap/afp