1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaPakistan

Mahakama Pakistan yamfungulia kesi nyingine Imran Khan

23 Oktoba 2023

Mamlaka nchini Pakistan zimemfungulia mashtaka waziri mkuu wa zamani, Imran Khan, kwa madai ya kuvujisha nyaraka za siri ya kidiplomasia.

https://p.dw.com/p/4XvG8
Waziri Mkuu wa Zamani Pakistan Imran Khan
Waziri Mkuu wa Zamani Pakistan Imran KhanPicha: Akhtar Soomro/REUTERS

Hii ni hatua nyengine kali dhidi ya mwanasiasa huyo mwenye ushawishi mkubwa nchini humo, ambaye sasa anaweza kukabiliwa na hukumu ya kifo na kuondoa uwezekano wa kushiriki katika uchaguzi mwezi Januari. 

Tangu kuondolewa madarakani mwaka jana, Khan amekuwa akikabiliwa na kesi nyingi ambazo anasema zimeundwa kumzuia asigombee uchaguzi ujao Januari 2024.

Mwanasiasa huyo alifungwa jela mwezi Agosti kwa miaka mitatu kwa makosa ya ufisadi lakini kifungo chake kilibatilishwa, badala yake aliwekwa kizuizini kwa shtaka la kusambaza nyaraka za serikali.

Soma pia:Khan kuzuiwa kwa wiki mbili zaidi Pakistan

Jaji Mohamed Zulqarnain amesema Khan pamoja na Shah Mahmood Qureshi, aliyekuwa waziri wake wa mambo ya kigeni, wamefunguliwa mashitaka kwa kuvujisha siri za taifa kwenye mkutano wa hadhara na kesi yao itasikilizwa wiki hii katika gereza lenye ulinzi mkali katika jiji la Rawalpindi.

Kesi hiyo inahusiana nahotuba ya Khan, kuonyesha barua ya siri katika mkutano wa hadhara baada ya kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye bungeni mwaka jana.

Inadaiwa kwamba barua hiyo ni uthibitisho Khan alikuwa akitishwa na kwamba kuondoshwa kwake madarakani ilikuwa njama ya Marekani inayodaiwa kutekelezwa na jeshi na serikali nchini Pakistan.

Hukumu ya kifo itamkabili Khan?

Kulingana na Umair Niazi, mmoja wa mawakili wa utetezi wa Khan, shitaka la kufichua siri za serikali linabeba hukumu ya maisha jela au kifo.

Hata hivyo, wakili huyo amesema anaamini Khan na Qureshi wataachiliwa huru kwani hawakufanya kosa lolote.

Kiongozi wa timu ya wanasheria wa Waziri Mkuu wa zamani Pakistan Imran Khan, Naeem Haider Panjutha akizungumza na waandishi wa habari
Kiongozi wa timu ya wanasheria wa Waziri Mkuu wa zamani Pakistan Imran Khan, Naeem Haider Panjutha akizungumza na waandishi wa habariPicha: Anjum Naveed/AP/picture alliance

Niazi alihoji mbele ya hadhara kosa la msingi dhidi ya Khan akiwa waziri mkuu wa nchi pamoja na Shah Qureshi akiwa waziri wa mambo ya nje wa nchi, aliongeza kwamba wanasiasa hao sio maafisa wa idara ya serikali.

"Waziri Mkuu ndiye mtendaji mkuu wa nchi na analazimika kuchukua maamuzi ya kisera ya nchi," alisema.

Soma pia:Mahakama ya Islamabad yasitisha hatia ya ufisadi kwa Khan

Aliongeza kwamba Waziri Mkuu anapaswa kuamuru sera ya nje ya nchi, sio lazima kuchukua maagizo kutoka Marekani, bali pia anatakiwa ajipange na ndio hatua aliyoichukua mteja wake.

"Kuna uingiliaji wa wazi wa mataifa ya nje katika masuala ya nchi yetu na ndivyo amefanya, na watu wanamuunga mkono kwa hilo.” alimaliza Niazi kwa kutoa ujumbe wa Khan

Hati hiyo iliyopewa jina la Cipher haijawekwa hadharani na ama serikali au mawakili wa Khan, lakini ilionekana kama mawasiliano ya kidiplomasia kati ya balozi wa Pakistan kwa Washington na Wizara ya Mambo ya Nje huko Islamabad.

Maafisa wa Washington na Pakistan wamekanusha madai hayo. 

Huku haya yakijiri, Mahakama ya Juu Pakistan imetoa uamuzi wa kupinga kusikilizwa kwa kesi za raia katika mahakama za kijeshi.

Uongozi wa kijeshi na kiraianchini Pakistani ulikuwa umechukua uamuzi wenye utata wa kuwashitaki raia kwenye mahakama za kijeshi baada ya maandamano ya vurugu na mashambulizi ya kijeshi mnamo Mei 9 kufuatia kukamatwa kwa Khan.
 

Imran Khan ana kiu ya kukomesha machafuko Pakistan