1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaPakistan

Je mustakabali wa kisiasa wa Imran Khan ni upi ?

10 Agosti 2023

Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistani Imran Khan sasa ni mfungwa baada ya mahakama kumtia hatiani kwa kosa la rushwa . Je, ni nini mustakabali wa Imran Khan katika siasa baada ya kukamatwa ?

https://p.dw.com/p/4Uv1o
Pakistan Ex-PM Imran Khan
Picha: Akhtar Soomro/REUTERS

Mwanasiasa huyo wa upinzani wa umri wa miaka 70, ambaye bado ni maarufu katika taifa hilo la Kusini mwa Asia, alipatikana na hatia ya kuuza na kusema uongo kuhusu kupokea zawadi za serikaliza thamani ya zaidi ya dola 635,000 wakati wa kuhudumu kwake kama waziri mkuu wa nchi hiyo kuanzia mwaka 2018 hadi 2022. Khan amekanusha mashtaka hayo dhidi yake na kusisitiza kuwa ni mwathiriwa wa mateso ya kisiasa. Kwasasa amezuiliwa katika jela ya Attock umbali wa kilomita 60 Magharibi mwa mji mkuu, Islamabad. Gereza hilo linajulikana kwa hali zake mbaya na wafungwa wanajumuisha wanamgambo waliohukumiwa.

Hukumu inatishia kumaliza Khan kisiasa

Hukumu hiyo inatishia kumaliza azma ya Khan ya kisiasa. Yeyote anayepatikana na hatia ya kosa la jinai haruhusiwi kushiriki katika uchaguzi nchini Pakistan. Hii ina maana kwamba Khan hataweza kushiriki katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba. Kiongozi huyo wa upinzani ndiye mpinzani mkuu wa kisiasa kwa Waziri Mkuu wa sasa wa Pakistan Shehbaz Sharif. Madika Afzal, mshiriki katika taasisi ya Brookings, ameiambia DW kwamba hatima ya kisiasa ya Khan inatiliwa mashaka baada ya kumatwa kwake.

Pakistan imekuwa katika tete kisiasa tangu Khan alipoondolewa madarakani

Pakistan imekuwa katika hali ya vurugu za kisiasa tangu Khan alipoondolewa madarakani kupitia kura ya kukosa imani naye mwaka jana. Tangu hapo, Khan amekuwa akifanya kampeini ya uchaguzi ghafla na kupanga maandamano makubwa. Pia ameibuka kuwa mkosoaji mkubwa wa jeshi lenye nguvu la nchi hiyo, akilishutumu kwa kupanga njama dhidi yake ili kumweka nje ya mamlaka. Hata hivyo jeshi limekanusha madai hayo.

Wafuasi wa Imran Khan wafanya maandamano wakati wa kukamatwa kwa Khan mjini Karachi mnamo Mei 9 2023
Wafuasi wa Imran Khan wafanya maandamano wakati wa kukamatwa kwa Khan mjini Karachi mnamo Mei 9 2023Picha: Asif Hassan/AFP

Pakistan imeshuhudia mawaziri wakuu wa zamani wakikamatwa katika kipindi cha miaka iliyopita, huku Khan akiwa wa saba kufungwa jela. Hata kaka wa waziri mkuu wa sasa, Nawaz Sharif, ambaye pia aliwahi kuwa waziri mkuu, alikamatwa mara kadhaa kwa tuhuma za ufisadi. Zaigham Khan, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mwandishi wa habari aliyeko Islamabad, ameiambia DW kwamba uwezekano wa Khan kurejea madarakani unaonekana kuwa mdogo. Zaigham Khan ameongeza kuwa ijapokuwa ni vigumu kumtenga, huenda akakosa kurudi madarakani katika uchaguzi mkuu ujao.

Khan akabiliwa na kesi zaidi ya 100

Tangu kuondolewa madarakani kwa Khan, mashirika mbalimbali ya serikali yamefungua zaidi ya kesi 100 dhidi yake kwa tuhuma za kudharau mahakama hadi ugaidi na pia kuchochea ghasia. Na inaonekana kuwa hakuna mwisho kwa matatizo ya kisheria yanayomkumba waziri mkuu huyo wa zamani. Mnamo mwezi Mei, mamlaka ilimzuia Khan kwa siku tatu katika kesi tofauti ambayo alihukumiwa wakati wa wikendi. Kukamatwa kwake wakati huo kulizua ghasia mbaya, huku maelfu ya wafuasi wake kote nchini humo wakiingia barabarani kuandamana na kukabiliana na vikosi vya usalama. Baadhi yao pia waliharibu mali ya jeshi na serikali. Mamlaka baadaye ilianzisha msako mkubwa na kuwakamata maelfu ya wafuasi wa Khan na wafanyakazi kutoka chama cha Tehreek-e-Insaf (PTI).

Chama cha Khan chaweza kuwania ubunge

Wakati huu, Khan ameitisha maandamano ya amani. Siku ya Jumamosi, chama cha PTI kilisema kuwa tayari kimeasilisha rufaa katika mahakama ya juu kuhusiana na maamuzi katika kesi ya Khan. Iwapo mahakama ya juu haitabatilisha uamuzi wa mahakama ya chini na hatia hiyo kudumishwa, Khan atazuiwa na sheria kuwania wadhifa au kuongoza chama cha PTI. Lakini chama chake bado kinaweza kugombea uchaguzi wa ubunge.