1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaPakistan

Pakistan kuvunja bunge kutoa nafasi ya uchaguzi mpya

9 Agosti 2023

Mwanasiasa maarufu aliyefungwa jela Imran Khan kuwekwa pembeni katika uchaguzi mkuu ujao huku tetesi za uchaguzi kucheleweshwa zikipata nguvu

https://p.dw.com/p/4Uxeg
Pakistan Politik I Imran Khan
Picha: Anjum Naveed/AP/picture alliance

Pakistan inajiandaa kuvunja bunge hii leo, huku serikali ya mpito ikitarajiwa kuteuliwa, kusimamia uchaguzi ambao utamuweka pembeni mwanasiasa maarufu nchini humo,aliyewahi kuwa waziri mkuu,Imran Khan.

Tangu alipoondolewa madarakani kwa nguvu na bunge waziri mkuu wa zamani Imran Khan,mnamo mwezi Aprili mwaka jana, Pakistan imekuwa katika mkwamo mkubwa wa kisiasa.

Na matatizo yameongezeka zaidi katika nchi hiyo kufuatia kufungwa jela mwishoni mwa wiki mwanasiasa huyo maarufu na aliyekuwa mchezaji nyota wa kimataifa wa Kriketi,baada ya kushtakiwa na kuhukumiwa kwa makosa ya rushwa.

Chama chake kimekuwa kikiandamwa kwa miezi chungunzima.

Uchaguzi mpya ndani ya siku 90

Hii leo Pakistan inasubiri bunge livunjwe na kufungua njia ya kufanyika uchaguzi mpya na waziri mkuu anayeondoka Shehbaz Sharif katika hotuba yake ya mwisho katika baraza lake la mawaziri alisema kwamba katika kipindi cha miezi 16 iliyopita serikali yake ilijaribu kadri iwezavyo kuimarisha hali ya mambo na kulitumikia taifa kwa kujitolea kikamilifu lakini pia akasisitiza kwamba Pakistan haiwezi kupiga hatua mpaka utakapokuwepo Umoja wa Kitaifa.

Prime Minister Shahbaz Sharif
Picha: National Assembly of Pakistan/AP/picture alliance

Kwa mujibu wa katiba bunge litakapovunjwa waziri mkuu wa mpito anabidi atangazwe ndani ya kipindi cha siku tatu zitakazofuata na ndiye atakayesimamia uchaguzi mpya.

Kwa mujibu wa sheria uchaguzi unapaswa kufanyika ndani ya siku 90 tangu bunge kuvunjwa lakini serikali inayoondoka imeshatowa tahadhari kwamba uchaguzi huenda ukasogezwa mbele.Muungano usiotarajiwa kati ya vyama vilivyozoeleka vya kurithishana ambavyo vina mizozo na ambavyo vilishirikiana kumuondowa kwa nguvu madarakani Imran Khan,hivi sasa vina uungwaji mkono kidogo katika nchi hiyo ya tano kwa idadi kubwa ya watu duniani.

Hali ya uchumi pia nchini humo bado ni ya kujikongoja, licha ya shirika la fedha la kimataifa IMF kuipatia msaada wa kujikwamua huku ikizongwa na madeni, mfumko wa bei na ukosefu mkubwa wa nafasi za ajira katika sekta ya viwanda kutokana na ukosefu wa sarafu za kigeni kwaajili ya kununua mali ghafi.

Inaelezwa kwamba uchaguzi unaotarajiwa nchini humo ni muhimu sana kwasababu ndio utakaotowa mwelekeo wa serikali mpya itakayoingia kuiongoza nchi hiyo kwa miaka mingine mitano ijayo ambayo kimsingi itapaswa kuwa na nguvu za kufanya maamuzi muhimu ya kuukwamua uchumi.Hata hivyo kwa upande mwingine kwa miezi kadhaa zimekuwepo tetesi kwamba huenda uchaguzi ukaakhirishwa.

Pakistan | Finanzminister Ishaq Dar stellt den Haushalt für das Haushaltsjahr 2023/24 vor
Picha: Akhtar Soomro/REUTERS

Na data zilizotokana na utafiti uliofanywa mwezi Mei hatimae zilichapishwa  mwishoni mwa juma lililopita na serikali imesema tume ya uchaguzi inahitaji muda kuchora upya mipaka ya majimbo, hatua ambayo imesababisha mivutano na hasira miongoni mwa vyama vingi vya kisiasa nchini Pakistan.

Baadhi ya wanaofuatilia siasa za nchi hiyo wanasema hatua yoyote ya kuchelewesha uchaguzi inaweza kuwapa washirika wa muungano wa PML-N yaani Pakistan Muslim League na Pakistan Peoples Party PPP nafasi ya kutafuta njia ya kukizuia chama cha Imran Khan,cha Pakistan Tehreek eInsaaf-PTI.

Lakini ukweli wa mambo ni kwamba pia kuuchelewesha uchaguzi huo kunaweza kuukasirisha sana Umma wa Pakistan.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW