1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaJamhuri ya Kongo

Jeshi Kongo lakabiliana na mashambulizi ya M23

27 Oktoba 2023

Milio ya risasi iliendelea kusikika mchana kutwa siku ya Alhamisi karibu na mji mkuu wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Goma, kufuatia mapigano makali kati ya jeshi la Kongo, FARDC, na waasi wa M23.

https://p.dw.com/p/4Y5xb
Wanajeshi wa Jeshi la Kongo na Uganda wakiwa katika doria
Wanajeshi wa Jeshi la Kongo na Uganda wakiwa katika doriaPicha: Alain Uaykani/Xinhua/picture alliance

Mapigano hayo kati ya waasi wa M23 na muungano wa vijana wazalendo wanaoungwa mkono na jeshi la Kongo yalitokea katika mji mdogo wa Kibumba eneo la Nyiragongo.

Vyanzo vya kiraia katika eneo hilo vilizungumza juu ya utumiaji wa silaha nzito na jeshi la Kongo dhidi ya ngome za M23, milio iliyoanza kukaribia hata viunga vya mji wa Goma. 

Duru za kijeshi zilisema kuwa lengo ilikuwa ni kuwazuia waasi wa M23, ambao usiku wa Jumatano kuamkia Alhamisi walijaribu kujipenyeza katika mji wa Goma wakipitia katika mbuga ya wanyama ya Virunga.

Soma pia:Mapigano yaibuka Kongo kati ya M23 na vijana wazalendo

Tangu Alfajiri ya leo Ijumaa, milio ya risasi inarindima katika kijiji cha Bambo wilayani Rutshuru ambako waasi wa M23 wanakabiliana na muungano huo wa Vijana Wazalendo.

Mashambulizi hayo ya kila upande yamesababisha raia kuyakimbia makaazi yao, na kuingia katika kambi za wakimbizi huku wakisema hakuna mahitaji muhimu ya kiutu.

Tyisabe Climantine ambae alitengana na mumewe wakati wa makabiliano ya wanajeshi wa Kongo na waasi wa M23, aliambia DW kuwa usalama wa raia ni mdogo.

Raia: Tunahitaji amani kujenga nchi yetu

Ombi la raia kutoka sehemu mbalimbali zinazoshuhudia machafuko ni upatikanaji wa amani na pia kutolewa misaada ya dharura na serikali ya Kongo.

Baadhi ya raia wakiwa njiani kuelekea sehemu salama baada ya kuzuka mapigano Kongo
Baadhi ya raia wakiwa njiani kuelekea sehemu salama baada ya kuzuka mapigano KongoPicha: Benjamin Kassembe/DW

Wakati huo huo, milio ya risasi ilisikika pia majira ya mchana kati karibu na  vijiji vya Shonyi, Kazinga na Rushashi  wilayani Rutshuru ambako makundi ya vijana hao wazalendo yalipigana dhidi ya waasi wa M23.

Licha ya mapigano hayo ya mji wa Kibumba, waasi wa M23 wameendelea kuudhibiti mji huo unaopakana  kwa ukaribu na nchi jirani ya Rwanda. 

Soma pia:Mwanajeshi wa Kenya auawa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na misaada ya binadamu, OCHA, lilisema zaidi ya raia laki moja wameyakimbia makaazi yao mwezi huu wa Oktoba kutokana na mapigano katika maeneo mbalimbali ya Kivu Kaskazini.