1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaJamhuri ya Kongo

Waasi wa M23 waudhibiti mji wa kimkakati wa Kitshanga

23 Oktoba 2023

Waasi wa M23 wameudhibiti tena upya mji wa kimkakati wa Kitshanga wilayani Masisi baada ya mapigano makali kati yao na wanamgambo wajiitao "Muungano wa Vijana Wazalendo."

https://p.dw.com/p/4XuBh
Waoiganaji wa M23 wakiwa katika majukumu ya ulinzi
Waoiganaji wa M23 wakiwa katika majukumu ya ulinziPicha: Guerchom Ndebo/AFP

Vijana hao wanaolisadia jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo waliukimbia mji huo wakati milio wa risasi ikiendelea kurindima mchana kutwa wa jana Jumapili na kusababisha mamia ya raia kukimbia makaazi yao. 

Wiki moja iliyopita, mji huo wa Kitshanga ulikuwa umedhibitiwa na Vijana Wazalendo wanaodaiwa kulisaidia jeshi la Kongo.

Lakini sasa wameukimbia tangu asubuiya jana Jumapili baada ya shambulio kali la waasi wa M23 dhidi ya ngome zao.

Vyanzo mbalimbali vimeelezea kuwa waasi wa M23 walivurumisha mabomu kuelekea mji huo ulioko umbali wa kilomita 80 kutoka mji wa Goma, hali iliyosababisha baadhi ya wananchi kujeruhiwa na wengine kupata hifadhi katika kambi ya kijeshi ya Umoja wa Mataifa eneo hilo.

Soma pia:Congo yataka vikosi vya Afrika Mashariki viondoke DRC

Mapema mwanzoni mwa juma lililopita, baadhi ya waandishi wa habari walisindikizwa hadi Kitshanga  na mamlaka ya kijeshi hapa Kivu Kaskazini kwa lengo la kushuhudia usalama ulivyoanza kurejea baada ya makundi hayo ya Vijana Wazalendo kuuteka mji huo kutoka mikononi mwa M23.

Hali ya wasiwasi miongoni mwa wananchi

Hali ilikuwa ya wasiwasi pia katika kijiji cha Kinyandoni wilayani Rutshuru wakati makundi hayo ya Vijana Wazalendo yakizilenga kwa makombora ngome za M23.

Mapigano hayo yalishika kasi kuendelea hadi vijiji jirani ambapo nyumba kadhaa ziliharibiwa kwa mabomu, vilithibitisha vyanzo vya kiraia.

Maoni ya wakaazi wa Goma juu ya vikosi vya Jumuiya ya Afrika Mashariki

Kwenye miji yote hiyo miwili iliyo, raia wanasema wameshuhudia wapiganaji wa M23 wakishika doria hadi leo asubuhi, hukuwa wakiangaliwa na vikosi vya Umoja wa Mataifa pamoja na Kikosi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Soma pia:Kongo: Mapigano yaendelea kati ya waasi wa M23 na Maimai

Kwenye ukurasa wao wa X ,waasi hao wa M23 walithibitisha kuudhibiti mji wa Kitshanga huku jeshi la FARDC likiendelea kujiweka kando na vurugu hizo kufuatia kile wanachokiita kuheshimu makubaliano ya usitishwaji wa mapigano kwenye eneo hili.