1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi wa ndani DRC wakata tamaa na kuhisi kutelekezwa

5 Septemba 2023

Vurugu na ukosefu wa misaada vyawakatisha tamaa wakimbizi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Katika kambi za wakimbizi wa ndani Ituri kumeshuhudiwa ongezeko la watu waliokata tamaa na kuhisi kutelekezwa.

https://p.dw.com/p/4VxdZ
Demokratische Republik Kongo | Binnenvertriebene im Flüchtlingslager Kanyaruchinya
Picha: Aubin Mukoni/AFP/Getty Images

Waasi wa ADF, wenye mafungamano na kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu IS, wamekuwa wakisababisha vurugu na uharibifu mkubwa tangu miaka ya 1990 kaskazini mwa jimbo jirani la Kivu Kaskazini lakini katika miaka ya hivi karibuni wamepanua mashambulizi yao hadi Ituri.

Wamekuwa wakishindana vitendo vya ukatili na kundi la wanamgambo wa ndani la Codeco ( Ushirika wa Maendeleo ya Kongo), ambalo linashutumiwa kwa mauaji ya watu 15 mwezi uliopita katika kambi ya wavuvi.

Henriette Lofaku mwenye umri wa miaka 60 alikuwa akiishi na watoto wake 6 huko Walense-Vokutu, kijiji kilicho kwenye mpaka kati ya majimbo hayo mawili. Jioni moja ya Aprili mwaka 2021, ADF iliwashambulia na watoto wake watatu waliuawa kwa mapanga.

Soma pia: Zaidi ya raia 150 wauawa Kongo katika wiki mbili: UN

Kwa sasa Lofaku amekimbilia katika mji wa Komanda, takriban kilomita 75 kutoka mji mkuu wa jimbo la Bunia. Anasema waliacha na kupoteza kila kitu baada ya makazi yao kuchomwa moto na waasi hao.

Simulizi sawa na hiyo ameitoa pia Juliette aliyeonekana kuwa na majonzi alipokuwa akieleza masaibu yaliyomkuta ambapo dada yake na mwanawe waliuliwa huku watu wengine wa familia hiyo wakilazimika kuyahama makazi yao.

Eneo la Komanda ni kimbilio la maelfu ya watu

DR Kongo MONUSCO | Flüchtlingslager in Ituri
Makazi ya wakimbizi wa ndani huko IturiPicha: Alain Uaykani/Xinhua/IMAGO

Maeneo ya Komanda, ambayo yamekuwa kimbilio la wale wanaokimbia ghasia, huwapa hifadhi karibu watu 40,000 ambao kulingana na jumuiya inayotoa misaada ya kibinadamu eneo hilo, wanaishi huku kukiwa na usaidizi mdogo sana.      

Christine Dida, mama wa watoto wanane, ambaye alikimbia eneo la Djugu miaka mitatu iliyopita na ambaye sasa anaishi kwenye maturubai anasema wanateseka mno na hawana chochote iwe dawa au chakula. Bi Dida anasisitiza kuwa mamlaka zinapaswa kuzingatia uwepo wao.    

Bahati Letakamba, baba mwenye watoto tisa naye amekaa kwa muda wa miaka mitatu huko Komanda, anasema ili kukidhi mahitaji yao, wanapaswa kufanya kazi kwenye mashamba ya jamii ya watu wa asili. Kwa huzuni kabisa, alionesha unga kidogo wa muhogo uliobaki ili kulisha familia yake.

Soma pia: HRW: Waasi wa CODECO walifanya mauaji ya kikatili Ituri, DRC

Serge Mahunga wa kundi lisilo la kiserikali la "Solidarites Internationales" linalofanya kazi huko Komanda amesema hali ya waliokimbia makazi yao ni mbaya sana eneo hilo.

Huko Bunia, katika kambi nyingine ya wakimbizi wa ndani iliyoanzishwa mwaka 2019, imewapokea zaidi ya watu 14,000 ambao wanaishi pia katika hali ya wasiwasi kutokana na mfululizo unaoendelea wa mashambulizi kwenye vijiji kadhaa vilivyo karibu.

Kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa, takriban watu milioni 1.7 wameyakimbia makazi yao huko Ituri. Hiyo ni asilimia 40 ya wakazi wa jimbo hilo.

Mgogoro mkubwa na unaopuuzwa

DR Kongo Flüchtlinge aus Flüchtlingslager Kanyaruchikya
Wakimbizi wa ndani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kogo huko KanyarucinyaPicha: Benjamin Kassembe/DW

Baada ya kutembelea huko Komanda, Bruno Lemarquis, mratibu wa mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa nchini DRC anasema hiyo ni takwimu ya kushangaza huku akisisitiza kuwa mgogoro huo wa kibinadamu umekuwa ukiendelea kwa miaka 25 nchini DRC, na ni mojawapo ya mgogoro mkubwa, mgumu na mrefu zaidi duniani ambao pia lakini unapuuzwa.

Mapigano kati ya  makundi mbalimbali ya wanamgambo kati ya mwaka 1999 na 2003 yalisababisha vifo vya maelfu ya watu huko Ituri. Baada ya muongo mmoja wa utulivu, machafuko yalianza tena mnamo mwaka 2017.

Kulingana na Lemarquis, mwaka uliopita mahitaji ya kibinadamu yameongezeka mno kutokana na kuibuka kwa migogoro mipya kama vile uasi wa kundi la M23 huko Kivu Kaskazini. Wanajeshi wameondoka katika majimbo jirani, ikiwa ni pamoja na Ituri, ili kuingilia kati migogoro hiyo na hivyo kusababisha ombwe la usalama ambalo limetumiwa kama fursa na makundi mengine yenye silaha.

Soma pia: Zaidi ya raia 45 wauawa baada ya kushambuliwa na wanamgambo, Ituri

Watu waliokimbia makazi yao wanaikosoa serikali ya Kongo kwa kutowasaidia. Gavana wa jimbo la Ituri Jenerali Johnny Luboya N'kashama amesema serikali ina "rasilimali chache" na inatoa msaada kadri ya uwezo wake.

Kwa ujumla, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ina wakimbizi wa ndani zaidi ya milioni sita, wengi wao wakiwa jimboni Ituri, Kivu Kaskazini na Kusini. Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu inasema  kati ya dola bilioni 2.25 zinazohitajika kuwasaidia watu hao, ni pekee dola milioni 747 zilizopatikana kufikia Agosti 16 mwaka huu wa 2023.

(AFPE)

Masaibu ya wakimbizi wa ndani jimboni Ituri Kongo