1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Congo yataka vikosi vya Afrika Mashariki viondoke DRC

Jean Noël Ba-Mweze
10 Oktoba 2023

Serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo imesema vikosi vya uingiliaji vya jumuiya ya Afrika ya mashariki, EAC, laazima viondoke kwenye ardhi ya Kongo ifikapo mwezi Desemba.

https://p.dw.com/p/4XLHc
Kenya ni miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki zilizowatuma wanajeshi wake kusaidia kutokomeza machafuko mashariki mwa DRC.
Kenya ni miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki zilizowatuma wanajeshi wake kusaidia kutokomeza machafuko mashariki mwa DRC.Picha: Brian Inganga/AP/picture alliance

Vikosi vya EAC vilitumwa mkoani Kivu kaskazini ili kusaidia kurejesha amani upande huo wa mashariki mwa Kongo ambako waasi wa M23 wanaendelea kupambana na vikosi vya serikali.

Lakini vikosi hivyo vinaonekana kushindwa jukumu hilo na hivyo mamlaka ya Kinshasa inavitaka kurudi makwao. 

Ni zaidi ya mwaka mmoja tangu vikosi vya EAC vilipowasili mkoani Kivu kaskazini kwa lengo la kurejesha amani.

Kundi linalojiita Wazalendo laokoa baadhi ya vijiji kutoka kwa M23

Lakini waasi wa M23 waliendelea kuteka vijiji kadhaa katika maeneo ya Masisi na Rutshuru. Vijana wanaojulikana kama Wazalendo ndio wanapambana sasa na kundi la M23 na wamefaulu kuchukuwa baadhi ya vijiji hivyo.

ICC yatoa wito wa kukabiliana na uhalifu wa kivita DRC

Baada ya mkutano ambao makamu waziri mkuu anaehusikae na ulinzi Jean-Pierre Bemba aliushiriki nchini Tanzania, serikali ya Kongo imeamua vikosi vya EAC kuondoka ifikapo Desemba ijayo.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Felix tshisekedi
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Felix tshisekediPicha: Isa Terli /AA/picture alliance

Mkuu wa kikosi cha EAC nchini DRC ajiuzulu

"Vikosi vya kikanda yaani vya jumuhiya ya Afrika mashariki ni lazma viondoke Kongo ifikapo Desemba kama tulivyokubaliana kwani havijaweza kutatua swali la M23. Ndiwo ujumbe wetu katika mkutano huo kabla marais kukutana ili kutambua kwamba vikosi hivyo havikufaulu. Halafu hatua zitachukuliwa," amesema Patrick Muyaya, waziri wa mawasiliano wa Kongo. 

Mashirika ya kijamii yaunga mkono wito wa serikali ya Congo

Mashirika ya kiraia mkoani Kivu kaskazini yanaunga mkono kauli ya serikali ya Kongo kwani kazi ya vikosi vya jumuiya ya Afrika Mashariki haijaonekana hata kidogo mkoani humo. Ndivyo alivyoeleza Telesphore Mithondeke, msemaji wa shirika la kiraia la Masisi, moja ya maeneo yaliyodhibitiwa na M23.

DR Congo: Vikosi vya EAC havijafanikiwa kuwadhibiti waasi

"Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo haina tena haja ya vikosi vya kuja tu kuangaliya mambo. Kongo inahitaji misaada ambayo ikiwa ya kijeshi, wawe wanajeshi ambao wanakuja kupigana. Hapana kwa kuangaliya vita. Raia wa Kongo hana tena haja ya misaada kama na hiyo. Raia wa Kongo ana haja ya watu wa kuja kumsaidia kuboresha usalama." 

Wakazi wa Kinshasa pia wanaitaka Serikali izingatie msimamo wake ili vikosi vya EAC kuondoka na kuruhusu jeshi la Kongo kupigania nchi hii.

"Tunataka waondoke kwani tangu walipokuja ndipo M23 waliendelea kuthibiti maeneo. Kwa hivyo tunataka waende kwani hakuna wanachokifanya hapa. Tutaungana sisi wenyewe na kupigania nchi yetu," amesema Irène Ndaya, mmoja wa wakaazi wa Kinshasa.

Agosti mwaka 2022 ndipo vikosi vya jumuhiya ya Afrika ya mashariki viliwasili mkoani Kivu kaskazini. Lakini baada ya Serikali ya Kongo kutambua hakuna kinachoendelea, raïs Félix Tshisekedi alitaka jumuiya ya Afrika kusini (SADC) kutuma vikosi vyake ili kuchukuwa nafasi ya vikosi vya EAC.