1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaHungary

Hungary yachukua urais wa zamu wa Umoja wa Ulaya

1 Julai 2024

Hungary imechukua urais wa zamu wa Umoja wa Ulaya na imeahidi kuwa mpatanishi mwaminifu licha ya wasiwasi uliopo kulingana na wakosoaji kwamba serikali ya Hungary inatawala kimabavu na pia ni rafiki wa Urusi.

https://p.dw.com/p/4hkAJ
Ungarn Corona-Pandemie | Viktor Orban
Picha: John Thys/AP Photo/picture alliance

Hungary imesisitiza kuwa iko tayari kuchukua wajibu na majukumu ya kuongoza kambi hiyo ya nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Waziri wa Hungary anayeshughulikia maswala ya Umoja wa Ulaya Janos Boka, amesema nchi yake kuwa Rais wa zamu wa Umoja wa Ulaya wa haiahidi miujiza, lakini inaahidi uwezekano wa kupatikana maendeleo katika baadhi ya maeneo na uwezekano wa kufanyika mabadiliko katika maeneo mengine kwa lengo la kuirudisha hadhi ya Ulaya iwe juu tena!

Brussels Umoja wa Ulaya | Viktor Orban
Waziri Mkuuu wa Hungary Viktor OrbanPicha: John Thys/AP Photo/picture alliance

Naye Balozi wa Hungary katika Umoja wa Ulaya, Balint Odor, amewasilisha vipaumbele vya nchi yake kwa muda wa miezi sita ijayo na kimsingi vinahusu uchumi wa Ulaya.

Soma Pia:  Urais wa Hungary utaimarisha au kuudhoofisha Umoja wa Ulaya?

Amesema Ulaya inashindwa katika swala la ushindani na kwamba ni lazima zifanyike jitihada za ziada ili kuongeza nguvu za kiuchumi za bara Ulaya. Ameongeza kusema kwamba hii itakuwa mada kuu ya mkutano wa kilele usio rasmi wa Ulaya huko jijini Budapest utakaofanyika mwezi Novemba.

Hungary 2024 |Waziri wa Hungary  Janos Boka
Waziri wa Hungary anayeshughulikia maswala ya Umoja wa Ulaya Janos Boka Picha: Peter Lakatos EPA

Jukumu la urais wa kupokezana wa Umoja wqa Ulaya ni kuweka ajenda, kuwa mwenyekiti wa mikutano ya nchi wanachama katika nyanja zote isipokuwa kwenye masuala ya kigeni, maswala yanayohusu ukanda wa euro, kutafuta makubaliano kati ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya pamoja na kufikia makubaliano juu ya sheria na Bunge la Ulaya.

Licha ya upande unaoegemea siasa za mrengo wa kulia kuwa na wanasiasa wa kuunga mkono vipaumbele vyaHungarybaada ya kupata mafanikio kwenye uchaguzi wa Bunge la Ulaya lakini uwezo wa nchi ambayo ni Rais wa Umoja wa Ulaya katika kuendesha sera na Umoja huo ni mdogo.

Wachambuzi wanasema kwa maana hiyo itachukua miezi kadhaa kwa Tume mpya ya Ulaya na wabunge wapya hadi watakapoanza majukumu yao. 

EU Josep Borrell
Mkuu wa maswala ya Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya Josep BorrellPicha: Nicolas Economou/NurPhoto/picture alliance

Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban,ameiongoza nchi hiyo ya Ulaya tangu mwaka 2010 na mara kwa mara amekuwa akizozana na makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels kuhusu utawala wa sheria na masuala ya haki za binadamu nchini mwake.

Soma Pia: Orbán kufanya uhamiaji kuwa lengo la urais wa Hungary kwa Umoja wa Ulaya  

Wakosoaji wanasema Orban hana uvumilivu na wala haheshimu maoni yaliyo kinyume na kile anachoamini yeye. Pia ni kiongozi pekee wa jumuiya ya Umoja wa Ulayaambaye anaendelea kudumisha uhusiano na Urusi licha ya uvamizi wa nchi hiyo dhidi ya Ukraine.

Rais huyo wa Hungary Viktor Orban amekataa katakata kupeleka silaha nchini Ukraine na mara kwa mara amekuwa akipinga vikwazo vya Jumuiya ya Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi vinavyowekwa kutokana na vita.

Mwaka jana, Bunge la Ulaya lilipitisha azimio lakini halikuwa la kisheria. Azimio hilo liliangazia kurudi nyuma kwa Hungary kwenye maadili ya kidemokrasia na wajumbe walihoji ni jinsi gani nchi hiyo inaweza kuaminiwa kutwaa urais wa umoja huo kwa kipindi cha miezi sita.

Vyanzo: DPA/AFP