Watu wapatao 10 wauwawa Ecuador
10 Januari 2024Rais wa Ecuador Daniel Noboa ametoa amri kuyakabili na kuyaangamiza kabisa magenge ya wahalifu baada ya watu waliokuwa wamejihami na bunduki kufyetua risasi katika studio ya televisheni na majangili kutishia mauaji ya kiholela, katika siku ya pili ya ugaidi nchini humo.
Polisi imesema watu wanane wameuliwa na watatu kujeruhiwa katika mashambulizi yaliyofanywa katika mji wa bandari wa Guayaquil.
Soma pia: Daniel Noboa ashinda uchaguzi wa urais nchini Equador
Maafisa wawili waliuwawa kinyama na wahalifu waliojihami na silaha katika mji ulio karibu wa Nobol. Watu wapatao 10 wameuliwa katika mfululizo wa mashambulizi ya magenge ya wahalifu wakati Ecuador ikitumbukia katika kile ambacho rais Noboa amekitaja kuwa ni mgogoro wa ndani wa kivita.
Rais Noboa ameamuru operesheni za kijeshi kuyaangamiza magenge ya wahalifu baada ya wahalifu kutangaza vita kufuatia tukio la kutoroka gerezani Jumapili iliyopita kwa wakuu wa magenge ya dawa za kulevya.