1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaEcuador

Daniel Noboa ashinda uchaguzi wa urais nchini Equador

16 Oktoba 2023

Noboa mwenye umri wa miaka 35 amemshinda msoshalisti Luisa Gonzalez mwenye umri wa miaka 45 kwenye kura ya marudio.

https://p.dw.com/p/4XZEb
Daniel Noboa, mshindi wa uchaguzi wa urais nchini Ecuador ameahidi kurejesha usalama na utulivu katika taifa hilo la Marekani kusini.
Daniel Noboa, mshindi wa uchaguzi wa urais nchini Ecuador ameahidi kurejesha usalama na utulivu katika taifa hilo la Marekani kusini.Picha: Jimmy NEGRETE /API/AFP

Baada ya asilimia 93 ya kura kuhesabiwa, Noboa alikuwa mbele kwa asilimia 52 huku Gonzalez akiwa wa pili kwa asilimia 48.

Baraza la uchaguzi nchini humo limesema kulingana na kura zilizokwisha hesabika, matokeo hayo hayawezi yakabadilika.

Noboa ameahidi kurudisha amani katika nchi hiyo iliyovurugwa na vita vya umwagaji damu vya magenge ya ulanguzi mihadarati.

Gonzalez amekubali kushindwa na amempongeza Noboa kwa ushindi wake.

Amesema hayo alipokuwa akizungumza na wafuasi wake mjini Quito.

Wagombea hao wawili walishiriki kura ya marudio baada ya kuchukua nafasi ya kwanza na pili mbele ya wagombea wengine sita katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa Agosti 22.

Masuala makuu ambayo yanawapa wapiga kura changamoto nchini humo ni pamoja na uchumi ambao umetatizika tangu kutokea kwa janga la COVID-19, ongezeko la uhalifu ikiwemo mauaji na ghasia za magerezani.