1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafuasi wa jeshi Sudan waandamana tena

18 Oktoba 2021

Mamia ya waandamanaji wanaoliunga mkono jeshi la Sudan wameandamana tena Jumapili, na kuzidisha kile waziri mkuu wa kiraia Abdalla Mahdok alichokitaja kuwa ni mzozo mbaya na hatari zaidi wa kipindi cha mpito nchini humo.

https://p.dw.com/p/41oE6
Sudan I Protest in Khartoum
Picha: Marwan Ali/AP/picture alliance

 Waandamanaji hao walikusanyika nje ya kasri la rais katikati mwa mji mkuu Khartoum, wakidai kuvunjwa kwa serikali ya kidikteta ya mpito, na kusema imewaangusha kisiasa na kiuchumi.

Ali Askouri, mmoja wa waandaji amesema maandamano hayo yataendelea hadi serikali hiyo itakapotimuliwa, na kuongeza kuwa wameliomba baraza huru, ambalo ni chombo kinachoundwa na wanajeshi na raia, kinachosimamia serikali ya mpito, kutojihusisha tena na serikali hiyo.

Maandamano hayo yanajiri wakati siasa za Sudan zikikumbwa na mgawanyiko miongoni mwa makundi yanayoongoza mpito kutoka miongo mitatu ya utawala wa chuma cha Omar al-Bashir.

Soma pia: Mfumuko wa bei waongezeka zaidi nchini Sudan

Bashir aliondolewa na jeshi mnamo Aprili 2019, kufuatia maandamano makubwa ya umma yalioongozwa na vuguvugu la Vikosi vya Uhuru na Mabadiliko, FFC, ambao ni muungano wa kiraia uliogeuka msingi muhimu wa kipindi cha mpito.

Sudan I Protest in Khartoum
Waandamanaji wa Sudan wakiwa katika siku ya pili ya maandamano mjini Khartoum wakidai kuvunjwa kwa serikali ya mpito inayojumlisha raia na wanajeshi.Picha: Marwan Ali/AP/picture alliance

Mgawanyiko miongoni mwa wanamapinduzi

Maandamano ya karibuni, ambayo yaliachwa bila kusumbuliwa na vikosi vya usalama, yameandaliwa na kundi lililojitenga na FFC.

Wakosoaji wanadai kuwa maandamano hayo yanaongozwa na maafisa wa jeshi na vikosi vya usalama, na yanajumlisha wapinzani wa mapinduzi wanaokubaliana na utawala uliyopita. Kundi kuu la FCC limeitisha maandamano kinzani siku ya Alhamisi.

Soma pia: Maelfu waandamana Sudan kupinga serikali

Maandamano hayo yalifanyika kwenye kasri la rais ambako serikali ya mpito ina makao yake, huku waandamanaji wakipaza sauti za "Jeshi moja, watu wamoja" na kutaka iundwe serikali ya kijeshi.

Kundi lililojitenga lilitoa taarifa kuwahimiza wafuasi wake kushikilia msimamo wao, na pia kuingia mitaani siku hiyo. Lilisema linapinga mapinduzi ya kijeshi, na vivyo hivyo udikteta wa kiraia.

Sudan | nach Putschversuch | Premierminister Abdalla Hamdok
Waziri Mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok ameonya kuwa nchi hiyo inakabiliwa na mzozo mbaya na hatari zaidi.Picha: AFP/Getty Images

Sudan imepitia mabadiliko makubwa tangu kuondolewa kwa Bashir, ambaye anatakiwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC, kwa makosa ya mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu jimboni Darfur, ambako mzozo ulioanza mwaka 2003 ulisababisha mauaji ya watu 300,000.

Soma pia: Jaribio la mapinduzi lazimwa nchini Sudan

Matukio ya sasa yanajiri baada ya serikali kusema Septemba 21, kwamba ilitibua njama ya jaribio la mapinduzi, ambalo ilililaumu kwa maafisa wa jeshi na raia wenye mafungano na utawala wa Bashir.

Siku ya Ijumaa, waziri mkuu Hamdok alionya kuwa mchakato wa mpito unakabiliwa na mzozo mbaya na hatari zaidi. Waziri wake wa fedha Gibril Ibrahim siku ya Jumamosi aliwahutubia waandamanaji wanaotaka kujiuzulu kwa serikali.

Msemaji wa FFC Jaafar Hassan, alisema waandamanaji wanaoliunga mkono jeshi walikuwa wafuasi wa utawala uliopita na makundi ya nje ambayo maslahi yake yameathiriwa na mapinduzi. Maandamano ya Alhamisi yameitishwa kudai uhamishaji kamili wa madaraka kwa raia.

Chanzo: AFP,AFPTV.