1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jaribio la mapinduzi lazimwa nchini Sudan

Saleh Mwanamilongo
21 Septemba 2021

Vyombo vya habari nchini Sudan vimesema hatua zinachukuliwa kudhibiti hali ya kiusalama. Huku nchi hiyo ikikabiliwa na mabadiliko dhaifu tangu mwaka 2019.

https://p.dw.com/p/40bVi
Jeshi la Sudan lasema  kumefanyika jaribio la mapinduzi ambalo limeshindwa
Jeshi la Sudan lasema kumefanyika jaribio la mapinduzi ambalo limeshindwa Picha: Hussein Malla/AP Photo/picture alliance

Msemaji wa serikali amesema shughuli ya kuwahoji wanaoshukiwa kuwa nyuma ya jaribio hilo la mapinduzi itaanza muda mfupi ujao.

Vyombo vya habari nchini Sudan vinaripoti kuweko na jaribio la kuchukua jengo ambalo lina vyombo vya habari vya serikali. Shirika la habari la AFP linamnukuu afisa wa serikali akisema kumekuwa na jaribio la mapinduzi lililoshindwa, na watu wanapaswa kukabiliana nalo.

Kituo cha Tevisheni cha taifa nchini Sudan kimeripoti asubuhi ya leo kwamba kumefanyika jaribio la mapinduzi ambalo limeshindwa.

 ''Ndugu wananchi tumepokea taarifa hii ya dharura. Mshauri wa masuala ya habari wa mkuu wa majeshi ya ulinzi, Taher Abu Haja ametangaza kuzimwa jaribio la mapinduzi.''

Duru za kijeshi na serikali ziliiambia AFP kwamba jaribio hilo lilihusisha kundi la maafisa ambao wamesimamishwa mara moja.

Hatua za kiusalama

Waziri Mkuu wa Sudan, Abdalla Hamdok amekabiliwa na shinikizo za kiuchumi
Waziri Mkuu wa Sudan, Abdalla Hamdok amekabiliwa na shinikizo za kiuchumiPicha: picture-alliance/AP Photo

Taher Abuhaja, afisa mwandamizi wa serikali ya mpito ya Sudan amesema jaribio la kuchukua madaraka limeshindwa. Kwa upande wake Mohamed al-Fekki, afisa mwingine wa serikali amesema kila kitu kimedhibitiwa na serikali na mapinduzi yameshindwa.

Hakukuweko na misongamano ya magari katikati mwa jiji la Khartoum. Vikosi vya usalama hata hivyo vililifunga daraja kuu kwenye Mto Nile linalounganisha mji wa Khartoum na mji wa Omdurman.

Sudan kwa sasa inaongozwa na serikali ya mpito iliyoundwa na wawakilishi wa kijeshi na kiraia baada ya kupinduliwa kwa rais wa zamani Omar al Bashir Aprili 2019. Serikali hiyo ya mpito ilipewa jukumu la kusimamia kurudi kwa utawala kamili wa raia.

Zaidi ya miaka miwili baada ya kuundwa kwa serikali ya mseto, Sudan inaendelea kukumbwa na matatizo ya kiuchumi ya muda mrefu toka utawala wa Bashir.

Maandamano ya kutaka mageuzi

Maandamano ya kupinga makubaliano ya amani yaliyotiwa saini na vikundi vya waasi mwaka 2020
Maandamano ya kupinga makubaliano ya amani yaliyotiwa saini na vikundi vya waasi mwaka 2020Picha: Ibrahim Ishaq/AFP/Getty Images

Jana Jumatatu, waandamanaji waliifunga barabara kuu na vile vile kitovu muhimu cha biashara nchini, cha Port Sudan, kupinga makubaliano ya amani yaliyotiwa saini na vikundi vya waasi mwaka jana.

Maandamano mengine yalikuwa yamepangwa kufanyika mjini Khartoum leo na wanajeshi walikuwa wametumwa kushika doria mitaani.

Serikali ya mpito ya Sudan, ya waziri mkuu Abdalla Hamdok imekuwa ikikabiliwa na shinikizo la kuleta mageuzi ya kiuchumi na kisiasa, licha ya ahadi zake za kutaka kuboresha maisha ya raia wa Sudan.

Vyanzo : Mashirika ya habari