Wafanyabiashara Uganda walia Burundi kufunga mpaka na Rwanda
12 Januari 2024Shughuli za biashara miongoni mwa mataifa ya Afrika mashariki zimerahisishwa kutokana na masharti na taratibu sawia na nafuu hasa kwenye forodha za mipakani.
Hatua ya Burundi kufunga mipaka yake na Rwanda inaathiri jumuiya ya wafanyabiashara na wenye viwanda wa Uganda wanaouza bidhaa zao katika soko la Burundi ambayo haina mipaka ya moja kwa moja na nchi hiyo.
Bidhaa nyingi kutoka Uganda kuelekea Burundi hupitia Rwanda ambayo ni njia fupi ikilinganishwa na kupitia Tanzania.
Mkurugenzi wa shirikisho la wenyeviwanda Uganda Dkt Ezra Muhumuza amesema "tumo katika mashaka kuhusiana na bidhaa zetu mbalimbali ambazo italazimu kupitishwa safari ndefu ya Tanzania kufikishwa Burundi."
Soma pia: Burundi yafunga mpaka na Rwanda baada ya shambulio baya
Naye afisa wa habari wa shirikisho la sekta binafsi Uganda PSFU Florence Mambea amezihimiza Burundi na Rwanda kuzingatia njia za mashauriano kutatua migogoro ya kisiasa bila kutatiza biashara.
Katika taarifa yake, Rwanda imelezea masikitiko yake kuhusu hatua ya serikali ya Rwanda kufunga mipaka yake ikisema kuwa hii inakinzana na itifaki za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Wito watolewa wa kufanya mazungumzo
Sektetariati ya Jumuiya ya Afrika mashariki kupitia kwa katibu mkuu Dkt. Peter Mathuki nayo imesambaza taarifa kwenye vyombo vya habari ikielezea masikitiko yake lake ikihimiza suala hilo litatuliwe haraka iwezekanavyo.
Kwa upande wake baraza la biashara Afrika Mashariki EABC limeitisha mkutano wa dharura wa wadau katika sekta binafsi mjini Kampala kujadili suala hilo ili kufikia mkakati wa kushawishi Burundi kubadili msimamo wake.
EABC inasema kuwa ni muhimu kwa viongozi kuyapa kipaumbele masuala ya biashara na uchumi badala ya kutanguliza yale ya kisiasa wanapofikia maamuzi ya kufunga mipaka kati ya mataifa yao na mengine katika jumuiya hiyo.
Soma pia: Ndayishimiye aituhumu Rwanda kuwaunga mkono waasi wa Burundi
"Si sawa. Hii itatatiza biashara. Tunatoa mwito kwa rais wa Burundi kufungua mipaka na kuruhusu biashara kuendelea kwa hii itaathiri raia ya kawaida," alisema Mkurugenzi mkuu wa EABC John Bosco Kalisa, katika mazungumzo na DW.
Biashara kati ya Uganda na Burundi imefikia kiwango cha dola milioni 52 kwa mujibu wa taarifa za shirika la kimataifa la biashara ITC ambapo bidhaa zinazouzwa na Uganda ni sukari, saruji na vitu vingine vya ujenzi.
Biashara kati ya Rwanda na Burundi ni ya thamani ya dola milioni 5 hivi ambapo kati ya hizo Rwanda huiuzia Burundi bidhaa za thamani ya dola milioni 3.4.Kwa jumla Burundi huagiza asili mia 70 ya bidhaa kutoka afrika mashariki.
Bidhaa muhimu ambazo Burundi huuza kwa mataifa jirani ni mazao ya kilimo hususan kahawa ambayo huzalishwa kwa ngazi ya kaya kama shughuli yao kuu ya mapato.