1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Burundi yafunga mpaka na Rwanda baada ya shambulio baya

11 Januari 2024

Burundi imetangaza kufunga mpaka wake na Rwanda, wiki 2 baada ya kuituhumu nchini hiyo jirani yake kuunga mkono waasi waliofanya mashambulizi kwenye ardhi yake. Rwanda imesema hatua hiyo inakiuka kanuni za ushirikiano.

https://p.dw.com/p/4b9B8
Grenze zwischen Burundi Ruanda | in Akanyaru
Eneo la karibu na mpaka baina ya Rwanda na Burundi ukitazama kutoka upande wa Rwanda.Picha: Stephanie Aglietti/AFP/Getty Images

Burundi inasema kundi la waasi wa RED-Tabara walifanya shambulizi Desemba 22 karibu na mpaka na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kuuwa watu 20, wakiwemo wanawake na watoto.

Tangu kutokea kwa shambulio hilo, Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye amekuwa akiituhumu Rwanda kuwaunga mkono waasi hao, madai ambayo serikali ya Rwanda imeyakanusha mara kwa mara.

Kundi hilo la Red-Tabara, lenye makao yake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, liliibuka mwaka 2011, na sasa ndiyo mashuhuri zaidi miongoni mwa vikosi vya waasi wa Burundi, likikadiriwa kuwa na wapiganaji kati ya 500 na 800.

Waziri wa mambo ya ndani wa Burundi Matin Nitereste, amewaambia waandishi habari hapo jana jioni kwamba wameamua kufunga mpaka na Rwanda na kwamba yeyote anayejaribu kupitia mpaka huo hatofanikiwa.

Waziri Nitereste ameongeza kuwa "baada ya kubaini kwamba tulikuwa na jirani mbaya, Rais wa Rwanda Paul Kagame, tulisitisha uhusiano wote naye hadi atakaporejea kwenye hisia bora."

Alisema Rwanda inawahifadhi wahalifu wanaowadhuru watu wa Burundi, na kuongeza kuwa wao pia hawawataki raia wa Rwanda.

Kombobild Präsident Evariste Ndayishimiye und Präsident Paul Kagame
Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye (kushoto) na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame (kulia)

Shuhuda aliekuwepo kwenye mkutano huo uliofanyika kwenye kivuko cha mpakani cha Kanyaru-Haut, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba walivuka mpaka majira ya saa sita mchana na kwamba ulifungwa muda mfupi tu baada ya hapo.

Soma pia: Ndayishimiye aituhumu Rwanda kuwaunga mkono waasi wa Burundi

Rwanda imesema imeuelezea uamuzi huo wa Burundi kuwa wa kusikitisha, na kusema utazuwia uhuru wa watu kusafiri pamoja na usafirishaji wa mizigo katika kanda, ikiutaka pia kuwa ukiukaji wa kanuni za ushirikiano wa kikanda na itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

"Serikali ya Rwanda imesikia kupitia vyombo vya habari juu ya uamuzi wa kusikitishwa wa upande mmoja wa serikali ya Burundi kufunga tena mpaka wake na Rwanda. Uamuzi huu utazuwia uhuru wa usafiri wa watu na usafirishaji wa bidhaa," alisema Msemaji wa serikali ya Rwanda katika taarifa fupi baada ya hatua ya Burundi.

Uhusiano wa panda shuka

Uhusiano kati ya Rwanda na Burundi umekuwa wa kupanda na kushuka mara kwa mara. Ingawa ulikuwa umeanza kuboreka baada ya Ndayishimiye kuingia madarakani mwaka 2020, umeharibika tena kuhusiana na ushiriki wa Burundi nchini DR Kongo.

Vikosi vya Burundi kwa miaka kadhaa vimekuwa vikiendesha operesheni za pamoja na wenzao wa Kongo dhidi ya waasi katika upande wa mashariki ambao umekumbwa na uasi wa makundi mbalimbali.

Moja ya makundi hayo, la M23, linaungwa mkono na Rwanda kulingana na serikali za mataifa ya Magharibi na Umoja wa Mataifa -- madai ambayo Kigali inayakanusha.

Mzozo wa Kongo Mashariki | Kikosi cha Burundi
Wanajeshi wa Burundi waliokuwa sehemu ya kikosi cha uingiliaji cha Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichopelekwa Kongo kupambana na waasi wa M23.Picha: Alexis Huguet/AFP

Burundi iliwahi kufunga mpaka wake na Rwanda mnamo mwaka 2015, katikati mwa madai ya kuunga mkono makundi ya waasi. Mpaka huo ulifunguliwa tena mwaka 2022.

Kundi la Red-Tabara linashtumiwa kuanzisha vurugu mbaya dhidi ya taifa hilo la Afrika Mashariki tangu 2015, lakini halikuwa linafanya chochote huko tangu 2021, lilipofanya mashambulizi kadhaa, ikiwemo dhidi ya uwanja wa ndege katika mji mkuu wa Bujumbura.

Soma pia: Rwanda yakanusha kuwafadhili waasi wa Burundi mashariki mwa DRC

Akizungumza mwishoni mwa mwezi uliopita, Rais Ndayishimiye alisema makundi hayo ya silaha yamepatiwa nyumba, chakula, ofisi na pesa kutoka taifa linalowahifadhi, na kuitaja wazi wazi Rwanda. Mjini Kigali, serikali ilikanusha madai hayo, ikisema katika taarifa kwamba Rwanda haihusiani kwa njia yoyote na kundi lololote la waasi wa Burundi.

Kundi la RED-Tabara lilidai kuhusika na mashambulizi hayo kupitia mtandao wa X, likisema lililenga kituo cha mpakani na kuuwa wanajeshi tisa na askari polisi.

Katika chapisho jingine kwenye mtandao wa X, lilikanusha kuuwa raia na kusema kundi haliungwi mkono na taifa lolote, na kwamba lina uungwaji mkono wa watu wa Burundi.

Burundi pia ilijiunga na kikosi cha uingiliaji cha Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichopelekwa Novemba 2022 kuzima vurugu nchini DRC, lakini iliondoa wanajeshi wake mwezi uliopita, baada ya Kinsasa kukataa kurefusha muda wa kikosi hicho.

Chanzo: AFP