1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Burundi wawasili DR Kongo

6 Machi 2023

Wanajeshi wapatao 100 wa Burundi wamewasili mjini Goma mashariki mwa Jamuhuri ya Kidmokrasia ya Kongo ambako watahudumu katika kikosi cha kulinda amani cha Jumuiya ya Afrika Mashariki.

https://p.dw.com/p/4OJqA
Symbolbild I Soldaten Burundi
Picha: Mohamed Abdiwahab/AFP/Getty Images

Wanajeshi 30 wa Burundi waliwasili katika uwanja wa ndege wa Goma siku ya Jumapili kujiunga na kikosi cha kimataifa kinachoisaidia Kinshasa kukabiliana na ongezeko la wanamgambo katika kanda hiyo. Wanajeshi wengine 70 waliwasili kwa njia ya barabara kupitia mpaka wa Rwanda na Kongo.

Wanajeshi hao watatumwa kama sehemu ya kikosi cha kikanda kilichoundwa na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kujaribu kukomesha uasi wa M23 na kusambaratisha makundi mia au zaidi yenye silaha ambayo yanasababisha vurugu mashariki mwa DR Congo. Jumuiya hiyo yenye mataifa saba wanachama ilianza kupeleka wanajeshi mwaka uliopita.

Mapigano katika jimbo la Kivu Kaskazini yamesababisha idadi kubwa ya watu kuyahama makazi yao na kuzidisha hali ya wasiwasi, huku serikali ya DRC ikiishutumu Rwanda kwa kuunga mkono waasi wa kundi la M23 -- madai yaliyokanushwa na Kigali lakini yakiungwa mkono na Marekani na mataifa kadhaa ya Magharibi.

Staatschefs der Ostafrikanischen Gemeinschaft
Wakuu wa mataifa ya Afrika Mashariki wakiwa katika mkutano wa kilele mjini Bujumbura, kujadili mzozo wa Mashariki mwa Congo. Novemba 4, 2022.Picha: Tchandrou NIitanga/AFP/Getty Images

Soma pia: DR Congo: Mzozo uliopuuzwa

Wanamgambo hao waliibuka tena kutoka katika hali ya utulivu mwishoni mwa 2021, na baadaye kumiliki maeneo mengi ya Kivu Kaskazini, ikiwa ni pamoja na sehemu kubwa ya eneo la kaskazini mwa mji mkuu wake Goma.

EAC, ambayo imefanya mikutano kadhaa kusuluhisha mgogoro huo na kutoa wito wa kuondolewa kwa M23 kutoka maeneo yaliyokaliwa, iliunda kikosi cha kikanda kinacholenga kuleta utulivu mashariki mwa DRC.

Pande zote kuunga usitishaji mapigano

Taarifa ya EAC kwa vyombo vya habari siku ya Ijumaa ilithibitisha kuwa wanajeshi wa Burundi watatumwa, lakini haikufafanua idadi ya wanajeshi wanaosafiri kwenda DRC. Kulingana na ratiba mpya iliyopitishwa na viongozi wa Afrika Mashariki mwezi uliopita, "makundi yote yenye silaha", ikiwa ni pamoja na M23, lazima yaondoke ifikapo Machi 30.

Katika uwanja wa ndege siku ya Jumapili, Jenerali Emmanuel Kaputa Kasenga, naibu kamanda wa kikosi cha Afrika Mashariki, alikutana na waliofika Burundi na kuzungumza juu ya dhamira yao. Aliwaambia wanajeshi hao kwamba "watashiriki katika uondoaji bila masharti wa uasi wa M23".

Ruandas Präsident Paul Kagame Felix und DR Kongos Präsident Tshisekedi
Marais wa DRC, Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame, wakati nchi zao zikiwa bado na uhusiano mzuri. Picha: Simon Wohlfahrt/AFP

Soma zaidi: Congo : jopo la wataalamu laamini ungwaji mkono kwa M23

Wanajeshi hao wa Burundi wataungana na kikosi cha jeshi la Kenya chenye takriban watu 1,000 waliowekwa ndani na karibu na Goma tangu Novemba.

Siku ya Jumamosi, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, akizuru Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika hatua ya mwisho ya ziara ya Afrika, alisema pande zote zitaunga mkono kusitishwa kwa mapigano.

Wakati wa mazungumzo na Rais wa Angola Joao Lourenco na Rais wa DRC Felix Tshisekedi, pamoja na Rais wa Rwanda Paul Kagame, Macron alisema wote "wametoa uungaji mkono wa wazi" wa kusitisha mapigano Jumanne ijayo, kama inavyotarajiwa katika kalenda ya matukio iliyopatanishwa na Angola.