1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSenegal

Wabunge Senegal kukutana baada ya rais kuahairisha uchaguzi

Hawa Bihoga
5 Februari 2024

Wabunge wa Senegal watakutana hii leo kujadiliana baada ya tangazo la rais Macky Sall la kuahirisha uchaguzi wa rais hatua ambayo imeliingiza taifa hilo katika mgogoro na maandamano makubwa katika miji mikubwa.

https://p.dw.com/p/4c2yv
Demokrasia na siasa | Waandamanaji wanaopinga kuhairishwa uchaguzi wakiwa na bendera ya Senegal
Waandamanaji katika mji wa Dakar wakipinga kuahirishwa kwa uchaguzi wa rais Senegal.Picha: John Wessels/AFP

Hapo jana Jumapili serikali iliamuru televisheni za kibinafsi kuzimwa kwa kile kilichotajwa kuchochea vurugu kutokana na matangazo hayo kuonesha moja kwa moja hali halisi katika mitaa mbalimbali ya jiji la Dakar, hatua ilioashiria kuongezeka mvutano wa kisiasa nchini humo, baada ya tangazo la kuahirishwa kwa uchaguzi liliolotolewa na rais Sall.

Katikati ya hali hiyo ya wasiwasi wa kutofanyika uchaguzi kama ulivyopangwa viongozi wa vyama vya upinzani wamesema hali hiyo ni "mapinduzi ya kikatiba" na pia ni uvamizi wa demokrasia.

Leo wabunge wanatarajiwa kupigia kura pendekezo la kuahirishwa kwa uchaguziwa rais uliotarajiwa kufanyika mnamo Februari 25, kwa hadi kipindi cha miezi sita ijayo. Pendekezo hilo litahitaji kupata kura zisizopungua theluthi tatu kati ya wabunge165 ili kupitishwa.

Tangazo la Sall la kuhairishwa kwa zoezi la kupiga kura kwa ajili ya rais limeonekana kutokubalika katika ulingo wa siasa nchini Senegal na kusababisha maandamano makubwa katika mitaa hapo jana Jumapili.

Soma pia:Rais wa Senegal ahairisha uchauzi wa februari katika kipindi kisichojulikana

Rais Macky Sall alisema mwishoni mwa juma kwamba uchaguzi unahairishwa kutokana na sababu kadhaa ikiwemo kile alichokitaja mzozo kati ya Bunge la Kitaifa na Mahakama ya Kikatiba baada ya baadhi ya wagombea kuondolewa kwenye orodha.

Lakini kuhusu azma yake ya kushiriki katika uchaguzi huo alisema bado anayo nia na atashiriki katika mjadala wa kitaifa.

"Kwa upande wangu, ahadi yangu ya kutoshiriki uchaguzi bado haijabadilika," alisema sall wakati akitoa tangazo la kuhairishwa kwa uchaguzi uliotarajiwa kufanyika baadae mwezi huu.

Aliongeza kuwa "nitashiriki katika mjadala wa wazi wa kitaifa ilikuleta mazingira ya uhuru, uwazi na jumuishi kwenye uchaguzi." Alisisitiza kuhusu usawa na uwazi katika uchaguzi.

Wapinzani wapinga kuhairishwa kwa uchaguzi wa Februari

Kauli ya Sall imepingwa na baadhi ya viongozi wa vyama vya kisiasa ambao walikusanyika katika ofisi za makao makuu ya muungano wa upinzani wanaomuunga mkono Khalifa Sall, wakisema uamuzi huo haukubaliki.

Dakar, Senegal | Muandamanaji akionesha ishara ya amani
Msenegal alieingia mtaani kupinga kauli ya rais macky sall ya kuhairisha uchaguzi wa mwezi wa Februari.Picha: Zohra Bensemra/REUTERS

"Kamwe katika historia ya kisiasa ya Senegal hatujawahi kuona hali kama hii. Ni historia ya hatari, kuweza kuahirisha uchaguzi wa rais katika muda mfupi kabla ya kuanza kwake ni jambo lisilo kubalika."

Kufuatia kauli ya viongozi wa kisiasa baadhi ya wafuasi wao wameendelea kuingia mtaani kupinga kuhairishwa kwa zoezi hilo la kikatiba na kidemokrasia.

Polisi imetumia gesi ya kutoa machozi kuwasambaratisha katika mitaa waandamanaji waliokuwa wakipaza sauti"Macky Sall diktekta," wakitaka uchaguzi kufanyika kama ulivyopangwa.

Kufuatia hali ya mambo ndani ya Senegal jumuiya ya kimataifa imetolea mwito taifa hilo kuchukua hatua za haraka ili kuepusha kutumbukia katika mzozo wa wenyewe kwa wenyewe.

Soma pia:Umoja wa Afrika wamtaka rais Macky Sall aitishe uchaguzi wa rais haraka iwezekanavyo

Mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, mapema leo alilitaka Senegal kutatua "mzozo wake wa kisiasa kwa mashauriano, maelewano na mazungumzo, baada ya kushuhudiwa kwa makabiliano makali baina ya wafuasi wa kisiasa na jeshi la polisi.

Faki kupitia katika mtandao wa X zamani ukijulikna twitter alitoa wito kwa mamlaka "kuandaa uchaguzi haraka iwezekanavyo, kwa uwazi, kwa amani na utangamano wa kitaifa.

Nao washirika wa kimaendeleo wa Senegal wakiwemo Marekani, Umoja wa Ulaya na mtawala wa zamani wa kikoloni Ufaransa wote wameomba uchaguzi huo kupangwa upyaharaka iwezekanavyo.

Vyama vya siasa vya upinzani Afrika vimetekeleza wajibu wao?