Viongozi wa ulimwengu wamuenzi Jimmy Carter
1 Januari 2025Ikulu ya Marekani imesema Rais Joe Biden katika taarifa yake amesema, Marekani na dunia nzima imempoteza kiongozi shupavu, mwanasiasa na mfadhili wa misaada ya kibinadamu.
Rais mteule Donald Trump, amesema Wamarekani wana deni kubwa la kurudisha shukurani kwa marehemu Carter. Trump ameandika kwenye mitandao ya kijamii kwamba marehemu Jimmy Carter, alikabiliana na changamoto kama zilivyokuja alipokuwa rais wa Marekani na alifanya kila awezalo kuboresha maisha ya Wamarekani wote.
Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton, amesema mtangulizi wake alifanya kazi bila kuchoka kwa ajili ya ulimwengu bora na wa haki.
Kiongozi mwingine wa Marekani George W. Bush amesema Carter aliiheshimu ofisi ya Rais na kutokana na juhudi zake hata baada ya urais, zimechangia ulimwengu kuwa mahala bora.
Rais mwingine wa zamani wa Marekani Barack Obama amemsifu Jimmy Carter, kwa kuwafunza walimwengu maana halisi ya kuishi maisha mema, yenye heshima, haki na kutoa huduma.
Soma Pia: Ujumbe wa Wakfu wa Jimmy Carter kwa Kenya wakati wa uchaguzi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amemkumbuka marehemu Jimmy Carter, aliyekuwa Rais wa 39 wa Marekani kwa kusema kuwa alitambua mapema juu ya umuhimu wa kuilinda sayari yetu pamoja na afya ya umma duniani ambayo ni mambo muhimu kwa maslahi ya usalama wakila taifa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema Carter atakumbukwa kwa kuhimiza mshikamano na kuwasaidia watu walio hatarini na imani yake isiyo na kifani kawa ajili ya manufaa ya wote.
Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni Tedros Adhanom Ghebreyesus amebainisha kazi ya Carter baada ya urais na Wakfu wa Carter alioungoza katika kuokoa maisha ya watu wengi na kusaidia katika kuyatokomeza magonjwa mengi ya kitropiki.
Soma Pia: Jimmy Carter asema kundi la Hamas liko tayari kuitambua Israel
Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen, ametoa wito wa kuendelezwa uongozi bora, maadili na demokrasia. Amesema Carter atakumbukwa kwa juhudi zake za kutetea amani, kuboresha afya ya umma na demokrasia duniani kote.
Naye Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, amesema kifo cha Carter,kimelinyag'anya taifa la Marekani mpigania demokrasia na ulimwengu umempoteza mpatanishi mkuu wa amani ya Mashariki ya Kati na mtetea haki za binadamu.
Miongoni mwa viongozi wanaoendelea kutoa salamu za rambirambi kwa kifo cha aliyekuwa Rais wa Marekani Jimmy Carter ni pamoja na Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau, Rais wa Israel Isaac Herzog ambaye amesema mkataba wa Amani uliowezeshwa kufanikiwa kwake na marehemu Jimmy Carter umeendelea kuwa nanga ya utulivu katika Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini miongo mingi baadaye.
Soma Pia: Jimmy Carter si ruhusa Gaza
Viongozi wengine ni Waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer, Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi, Mfalme Charles wa Uingereza, Rais wa Brazil Lula Da Silva, Rais wa Panama, Jose Mulino, Rais wa Ukraine Volodymir Zelensky, Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez na Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis ambaye amesema marehemu Carter atakumbukwa kwa kujitolea kwake kulikochochewa na imani ya kina ya Kikristo, kwa ajili ya upatanishi na amani kati ya watu.
Safari ya mwisho ya Jimmy Carter itaishia nyumbani kwake katika mji mdogo wa Plains, Georgia, alikokulia kwenye eneo la shamba la njugu karanga. Hapo ndipo mke wake, Rosalynn, alipozikwa mwaka jana katika eneo la makaburi walilolichagua miaka ya nyuma.
Vyanzo: AFP/AP