1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utulivu wa kiasi waripotiwa maeneo ya Gaza

Sylvia Mwehozi
18 Juni 2024

Israel imeishambulia Gaza sku ya jumatatu huku mashuhuda wakiripoti milipuko kadhaa upande wa kusini mwa eneo hilo lililozingirwa, ingawa mapigano yanaripotiwa kupungua kwa kiasi fulani.

https://p.dw.com/p/4hBST
Gaza-athari za vita
Wapalestina wakipita katikati mwa rundo la kifusiPicha: Mahmoud Issa/Middle East Images/picture alliance

Utulivu huo wa kiasi unashuhudiwa wakati Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akilivunja baraza lake la vita, hali inayoakisi migawanyiko ya kisiasa ya nchi hiyo. Msemaji wa ofisi ya waziri mkuu wa Israel David Mencer alisema kuvunjwa kwa baraza hilo la vita kunafuatia kujiuzulu kwa kiongozi wa siasa za wastani Benny Gantz, ambaye alihitaji kuundwa kwa baraza la mawaziri la vita ili kujiunga na serikali ya umoja.

Soma zaidi: Netanyahu avunja Baraza lake la vita nchini Israel

Mencer ameongeza kuwa majukumu ya baraza hilo yatachukuliwa na baraza lililokuwepo la ulinzi ambalo limekamilisha maamuzi yaliyopendekezwa na baraza la vita. Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kuwa hatua hiyo imechukuliwa ili kukabiliana na shinikizo la wanasiasa wa siasa kali wanaotafuta ushawishi katika maamuzi.

Khan Yunis | Eid al-Adha
Wapalestina wakiswali kusherehekea sikukuu ya Eid al AdhaPicha: Mohammed Salem/REUTERS

Tangazo la "kusimamisha shughuli za kijeshi" kwa muda haswa majira ya mchana kila siku kwa ajili ya kuruhusu usambazaji wa misaada kuzunguka njia ya kusini mwa Gaza, lilitolewa mwishoni mwa wiki na jeshi la Israel, na limeonekana kuendelea kufanya kazi siku ya Jumatatu. Tangazo hilo pia liligongana na sikukuu ya Kiislamu ya Eidna kuleta utulivu wa kiasi katika baadhi ya maeneo ya Gaza. Hata hivyo wizara ya afya ya Gaza inayoongozwa na Hamas, imesema imerekodi vifo vya watu 10 ndani ya saa 24 zilizopita, ikiwa ni idadi ndogo ya kila siku tangu vita vilipoanza. 

Siku ya Jumatatu mashuhuda walilieleza shirika la habari la AFP kwamba walisikia milipuko katikati na magharibi mwa mji wa kusini wa Rafah. Maafisa wa Palestina katika eneo hilo pia waliripoti ufyatuaji wa mizinga mapema siku ya Jumatatu, kabla ya kuanza kwa kipindi cha "usimamishaji shughuli za kijeshi" za kila siku zilizotangazwa na jeshi la Israel. Israel kusitisha mapigano kwa muda kila siku Gaza

Israel - Jerusalem-maandamano
Maelfu ya Waisraeli walioandamana kupinga serikali ya waziri mkuu Benjamin NetanyahuPicha: Ohad Zwigenberg/AP Photo/picture alliance

Na huko mjini Jerusalem, maelfu ya Waisreal waliandamana siku ya Jumatatu dhidi ya serikali ya Netanyahu kwa kushindwa kufikia makubaliano ya kuwakomboa mateka ambao bado wanashikiliwa na kundi la Hamas. Waandamanaji walikusanyika nje ya majengo ya bunge na karibu na makazi ya Netanyahu, wakishinikiza uchaguzi wa mapema na kuachiliwa kwa mateka wote.

Soma: Maandamano yaanza Israel kutaka mateka wakombolewe

Mmoja ya waandamanaji alinukuliwa akisema kuwa; "Tunapaswa kubadili serikali hii ovu. Huu ni wakati wetu. Mateka 120 bado wako Gaza. Lazima tubadilishe hii serikali. Hii ndio njia yetu pekee ya kuwaadhibu na kuirudisha Israeli, nchi ambayo tunaipenda sana. Inabidi tuendelee kupigana, tunapaswa kuendeleza maandamano hadi tuirujeshe Israel."

Hayo yanajiri mnamo wakati juhudi za upatanishi zinazofanywa na Marekani, Qatar na Misri kuelekea upatikanaji wa makubaliano ya kusitisha vita zikikwama kwa miezi kadhaa.