1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu alivunja Baraza lake la Vita

17 Juni 2024

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amelivunja Baraza lake la Vita ambalo husimamia operesheni za kijeshi huko Gaza. Mapigano yanaendelea pia kuripotiwa katika ardhi ya Palestina huku idadi ya vifo pia ikiongezeka.

https://p.dw.com/p/4h9uu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: JACK GUEZ/REUTERS

Taarifa ya kuvunjwa kwa baraza hilo la vita la Israel lenye wanachama sita, imetangazwa na msemaji katika ofisi ya waziri mkuu David Mencer. Hatua hii inakuja baada ya kujiondoa kwa mbunge wa upinzani Benny Gantz ambaye kwa wiki kadhaa sasa amekuwa akimlaumu Netanyahu kuwa ameshindwa kuwa na mpango thabiti katika vita vya Gaza.

Maafisa wa serikali ya Israel waliozungumza kwa sharti la kutotajwa majina wamesema kwa sasa Netanyahu ambaye amekuwa akikabiliwa na shinikizo la ndani na hata kimataifa, atakuwa akifanya majadiliano kuhusu vita hivyo na kundi dogo la mawaziri akiwemo waziri wake wa Ulinzi Yoav Gallant.

 Benny Gantz aliyejiondoa kwenye Baraza la Vita la Netanyahu
Mbunge wa upinzani Benny Gantz aliyejiondoa kwenye Baraza la Vita la NetanyahuPicha: ABIR SULTAN/EPA

Kwa miaka mingi Benny Gantz amekuwa mpinzani mkuu wa Netanyahu na alikubali kujiunga na serikali yake kama ishara ya mshikamano baada ya shambulio la Hamas la Oktoba 7 mwaka jana.

Lakini amechukua uamuzi wa kujiondoa akisema haafikiani na maamuzi ya Netanyahu katika vita hivyo. Mara kadhaa Benjamin Netanyahu amekuwa akitaja kuwa hatua zote anazochukua ni kwa manufaa ya taifa la Israel.

Mapigano yaendelea kuripotiwa huko Gaza

Makumi ya watu wamearifiwa kuuawa katika kipindi cha saa 24 zilizopita. Wizara ya Afya eneo hilo inayodhibitiwa na Kundi la  Hamas imesema watu 37,347 ndio tayari wameuawa tangu kuanza kwa mzozo huu. 

Aidha, Israel imesema itakuwa ikisitisha mapigano kila siku kwa saa kadhaa katika eneo la kusini mwa Gaza ili kuruhusu usafirishaji wa misaada ya kibinaadamu. Msemaji wa taasisi za Kiraia za Israel katika maeneo ya  Palestina  Shimon Freedman amesema:

"Israel imeendelea kuboresha uwezo wake wa kufanya ukaguzi wa kiusalama kwa shehena za misaada ya kibinadamu, na hakuna kikwazo chochote kinachozuia misaada hiyo kufika inakohitajika. Changamoto iliyosalia ni kwenye usambazaji. Tuna uwezo wa kukagua idadi kubwa zaidi ya misaada ya kibinadamu kuliko ile inayoweza kusambazwa na Umoja wa Mataifa."

Lakini Shirika la kimataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limesema Israel imeendeleza mashambulizi yake eneo hilo na hususan huko Rafah.

Katika hatua nyingine, Mjumbe wa Marekani Mwanadiplomasia Amos Hochstein yupo Israel na baadaye ataelekea Lebanon ili kujaribu kutatua kwa njia ya mazungumzo mzozo unaotokota kati ya jeshi la Israel na wanamgambo wa Hezbollah ambao wamekuwa wakishambuliana katika eneo la mpakani kati ya mataifa hayo mawili.

Gaza| Wapalestina wakishiriki sala ya Eid
Wapalestina wakishiriki sala ya Eid huko Khan Younis katika Ukanda wa GazaPicha: Mohammed Salem/REUTERS

Soma pia:Baraza la Usalama laidhinisha azimio la kusitisha vita Gaza 

Wakati huo huo, waisalamu wanasherehekea sikukuu ya Eid huku Wapalestina wakiendelea kukabiliwa na mateso makubwa yatokanayo na vita. Mataifa mengi ya barani Asia, ikiwa ni pamoja na Indonesia, Malaysia, India na Bangladesh, wamesherehekea sikukuu ya Eid al-Adha leo Jumatatu, wakati Waislamu katika maeneo mengine duniani kote, ikiwa ni pamoja na Saudi Arabia, Libya, Misri na Yemen wakisherehekea sikukuu hiyo hapo jana.

(Vyanzo: Mashirika)