1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Upinzani nchini Israel waungana kukabiliana na Hamas

10 Oktoba 2023

Ubalozi wa Israel nchini Marekani umesema idadi ya Waisrael waliokufa tangu kuzuka kwa mzozo kati yake na Hamas mwishoni mwa wiki iliyopita imepindukia 1,000. Jeshi la Israel lasema raia na wanajeshi 900 wamekufa.

https://p.dw.com/p/4XMhn
Chama cha waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu cha Likud kimesema upinzani umekubali kuungana kupambana na uvamizi wa Hamas
Chama cha waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu cha Likud kimesema upinzani umekubali kuungana kupambana na uvamizi wa Hamas Picha: AFP

Chama cha waziri mkuu Benjamin Netanyahu nacho kimesema wakuu wa vyama tawala vya upinzani nchini humo wamekubaliana kuunda serikali ya dharura na upinzani, ili kwa pamoja kukabiliana na hali ya dharura inayolikabili taifa hilo kwa sasa. 

Kulingana na taarifa ya ubalozi wa Israel nchini Marekani, iliyochapishwa katika ukurasa wa mtandao wa X, watu 1,008 wameuawa. Chapisho hilo lilionyesha idadi hiyo, pamoja na watu wengine 3,418 waliojeruhiwa.

Muda mfupi baada ya chapisho hilo kusambazwa, jeshi la Israel IDF nalo lilisema kwenye ripoti yake kwamba watu 900, raia na wanajeshi waliuawa tangu shambulizi la kwanza la mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mapema leo, jeshi la anga la nchini humo, IAF limesema kwamba limewarejesha nyumbani mamia ya wanajeshi waliokuwa nje ya nchi ili kuongeza nguvu kwenye operesheni za kijeshi dhidi ya Hamas.

Tukisalia nchini humo, taarifa kutoka Tel Aviv zimesema wakuu wa vyama tawala wamekubaliana kuunda serikali ya dharura na upinzani, hii ikiwa ni kulingana na msemaji wa chama cha Likud cha waziri mkuu Benjamin Netanyahu. Netanyahu ameruhusiwa kuchukua hatua stahiki kufuatia maamuzi hayo ya pamoja yaliyofikiwa baada ya kikao cha vyama hivyo.

Benny Gantz, ambaye pia aliwahi kuwa waziri wa ulinzi wa Israel ameonyesha nia ya kuunganisha upinzani ili kukabiliana na kitisho shidi ya Israel
Benny Gantz, ambaye pia aliwahi kuwa waziri wa ulinzi wa Israel ameonyesha nia ya kuunganisha upinzani ili kukabiliana na kitisho shidi ya IsraelPicha: Ariel Hermoni/MOD

Siku ya Jumamosi, Netanyahu aliwaomba wakuu wa vyama viwili vya upinzani vilivyoko bungeni, Yair Lapid na Benny Gantz kuungana ili kuunda serikali ya dharura na kuanzisha mazungumzo ya ndani, ambayo matokeo yake yametangazwa mchana huu. Lapid tayari ameashiria kukubaliana na hatua hiyo ili kukabiliana na hali tete inayolikabili taifa hilo.

Soma pia: Nchi nyingi wanachama wa Baraza la Usalama la UN zimelaani mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel

Na huko Moscow, rais Vladimir Putin wa Urusi amesema mzozo unaoshuhudiwa sasa kati ya Israel na Hamas ni ishara tosha ya kushindwa kwa sera za Marekani kuelekea Mashariki ya Kati. Putin ametoa matamshi hayo alipokutana na waziri mkuu wa Iraq Mohammed Shia Al Sudani.

Msalaba Mwekundu wataka kusaidia juhudi za kuwatambua raia waliopotea

Tukiigeukia misaada ya kiutu, Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limejitolea kuwa mpatanishi ili kusaidia kutambua mustakabali wa watu ambao hawajulikani walipo baada ya shambulizi la Hamas.

Rais wa Kamati ya Msalaba Mwekundu Mirjana Spoljaric amesema ana mashaka makubwa juu ya mateso yanayozikumba familia zilizopotezana kutokana na kile kinachoendelea. Spoljaric aidha ametoa wito kwa Hamas kuwaachia huru mara moja mateka wote inaowashikilia na kuzitaka pande zote kuacha kuwalenga raia, miundombinu muhimu na maeneo ya huduma za tiba.

Soma pia: Mzozo kati ya Israel na Hamas wazidi kutokota

Katika hatua nyingine, Umoja wa Ulaya na Baraza la ushirikiano kwa Mataifa ya Ghuba wametoa wito wa kubakizwa kwa misaada kwenye maeneo ya Palestina kufuatia wasiwasi kwamba misaada hiyo inaweza kusitishwa baada ya shambulizi hilo la Jumamosi.

Raia wakiwa wamebeba misaada ya chakula kupitia shirika shirika la UNRWA, ambalo baadhi ya mataifa yalinuia kuzuia misaada zaidi baada ya Hamas kuivamia Israel
Raia wakiwa wamebeba misaada ya chakula kupitia shirika shirika la UNRWA, ambalo baadhi ya mataifa yalinuia kuzuia misaada zaidi baada ya Hamas kuivamia IsraelPicha: John Minchillo/AP Photo/picture alliance

Mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa hayo waliokutana Muscat, Oman wametoa wito huo katika azimio la pamoja, baada ya hapo kabla kutofautiana dhidi ya mpango huo wa kufutwa kwa misaada na kusisitiza umuhimu wa kuendelezwa kwa msaada wa kifedha kwa shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kiutu kwa wakimbizi wa Palestina, UNRWA. Azimio hilo lilisomwa na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell.

Aidha, amesema taarifa ya kwamba Ujerumani nayo inasitisha misaada hiyo ni ya uwongo na kusema waziri wa Ujerumani amethibitsisha kwamba hawataondoa msaada huo.

Kutokea Dubai, balozi wa Israel kwenye Umoja wa Falme za Kiarabu amesema hakuna kitakachoizuia Israel kuiangamiza Hamas. Balozi Amir Hayek ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba watafanya kila linalowezekana ili kuhakikisha watu wao hawatishwi na wala kuumizwa tena.

Amesema, wanalazimika kuhakikisha kwamba kila mtu ataelewa ya kwamba ikiwa mtu yeyote atafikiria kufanya kitu kama hicho na kuhatarisha maisha ya Waisraeli, atakabiliwa na majibu makali na kamwe hatarudia tena.

Na huko Geneva, tume ya Umoja wa Mataifa inayofuatilia mzozo huo imesema, upo ushahidi wa wazi wa uhalifu wa kivita uliofanywa na pande zote wakati wa mapigano makali nchini Israel na Gaza, ikiwa ni pamoja na wanamgambo wenye silaha kuwateka raia na kuwatumia kama ngao ya vita na kusema hayo hayakubaliki na wahusika wote wanatakiwa kuwajibishwa.