1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Ukraine yadungua droni 36 katika mashambulizi ya usiku

25 Mei 2023

Ukraine imesema mifumo yake ya ulinzi imedungua droni zote 36 za Iran zilizorushwa katika eneo lake na Urusi katika mashambulizi ya usiku, ambayo inasema yalikuwa yameelekezwa dhidi ya miundombinu na maeneo ya jeshi.

https://p.dw.com/p/4Rnz8
Ukraine Russische Militärdrohne mit Bombe und Rakete
Picha: Aleksandr Gusev/Pacific Press/picture alliance

Rais Zelenskiy amesema ulikuwa usiku mgumu kwao lakini amesifu kazi ya mifumo ya ulinzi wa anga ya taifa hilo ambayo ilizidungua droni zote 36 chapa ya Shahed zilizitumiwa na adui.

Tangu Oktoba mwaka jana, Moscow, ambayo ilianzisha uvamizi kamili Februari mwaka jana, imekuwa ikituma wimbi la droni kushambulia maeneo ndani ya Ukraine, ambazo licha ya kwenda kwa kasi ndogo, zinatajwa kuwa nafuu na zinazoweza kutumika zaidi kuliko makombora ya kisasa.

Mkuu wa utawala wa kijeshi wa Kyiv alisema mji mkuu huo ulishambuliwa na mawimbi ya droni lakini zote zilidunguliwa, akilitaja hilo kuwa shambulio la 12 dhidi ya mji wa Kyiv mwezi huu. Mamlaka za mikoa na kijeshi katika mikoa ya kusini na magharibi mwa Ukraine pia ziliripoti kudungua droni.

Ukraine Drohnenangriff auf Kiew
Wakazi wa Kyiv wakikagua mabaki ya droni iliyodunguliwa wakati wa uvamizi wa Urusi mjini humo.Picha: Oleksandr Khomenko/REUTERS

Akizungumza katika ujumbe wake wa kila usiku kwa njia ya vidio, rais Zelenskiy alisema wanafanya maandalizi ya kupokea na kuanza kutumia ndege za kisasa za kivita chapa ya F-16, na kuongeza kuwa hiyo itakuwa moja ya ishara nzito kabisaa kutoka kwa ulimwengu kwamba Urusi itashindwa katika uvamizi wake.

Soma pia: Urusi yasema itajibu vikali mashambulizi dhidi yake

"Tunafanya kila tuwezalo kupunguza muda wa matokeo, kwa ajili ya kuonekana kwa ndege mpya na zenye nguvu zikiwa na marubani wa Ukraine katika anga ya Ukraine. Ni wazi kwamba hatua hii ya kimataifa itaturuhusu kupanua uwezo wetu wa ulinzi."

Zelenskiy alisema wanahitaji ndege zenye nguvu na ufanisi ili kukamilisha mfumo wa ulinzi wa anga. "Kwa upande mwingine, F-16 ya kwanza ya Ukraine itakuwa moja ya ishara kali kutoka kwa ulimwengu kwamba Urusi itapoteza tu kwa sababu ya uchokozi wake yenyewe, na itakuwa dhaifu na iliyotengwa zaidi."

Marekani: Uwezekano mkubwa Ukraine ilihusika na shambulio dhidi ya Kremlin

Gazeti la New York Times la nchini Marekani, limeripoti kuwa mashirika ya intelijensia ya Marekani yanaamini kwamba dhambulio la droni dhidi ya ikulu ya Kremlini mapema mwezi huu huenda lilipangwa na majasusi wa Ukraine au idara ya upelelezi wa kijeshi.

Soma pia: Eneo la mpakani kati ya Urusi na Ukraine laendelea kuwa tete

Tathimini hiyo ya Marekani ilitokana na mawasiliano yalionaswa kati ya Ukraine na Urusi, ambamo maafisa walisema wanaamini nchi yao ilihusika na shambulio hilo, na pia mawasiliano ya Warusi yalioashiria kwamba haikuwa operesheni ya uongo ya Urusi.

Msemaji wa Rais Vladmir Putin, Dmitry Peskov, ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa Urusi ilisema tangu mwanzo kwamba Ukraine ilihusika na shambulio hilo, na kuongeza kuwa haileti tofauti yoyote kuhusu kitengo kipi cha utawala wa Kyiv kilihusika.

Hata hivyo mshauri wa Rais Zelenskiy, Mykhailo Podolyak, amesisitiza kuwa Ukraine haihusiki kwa vyovyote vile na kile alichokiita shambulio lisilo na maana, na kwamba Urusi inajaribu kupunguza ugavi wa silaha kwa Kyiv, kwa kucheza na hofu ya magharibi juu ya uwezekano wa kuongezeka kwa vita kwa sababu ya madai ya shambulizi la Ukraine katika ardhi ya Urusi.

Wagner yaanza kuondoa wapiganaji Bakhmut

Mkuu wa kundi la mamluki la Wagner la Urusi, Yevgeny Prigozhin, alisema siku ya Alhamisi kuwa wanajeshi wake wameanza kukabidhi maeneo yao katika mji wa Bakhmut mashariki mwa Ukraine kwa jeshi la Urusi.

Tangazo lake linakuja siku chache baada ya jeshi la Moscow kusema kuwa lilikuwa limetuma ndege na mizinga katika ardhi ya Urusi dhidi ya kundi la "hujuma" lililovuka kutoka Ukraine.

Soma pia: Urusi yadai Ukraine imehusika kushambulia eneo lake la mpakani la Belgorod

Vita vya Bakhmut vimeendelea kwa karibu mwaka mmoja, vikiliharibu kabisaa jiji hilo na kuangamiza maelfu ya wapiganaji wa Wagner ambao wameongoza mashambulizi ya Urusi kwenye kitovu hicho cha viwanda.

"Tunaondoa vitengo kutoka Bakhmut leo. Tunakabidhi maeneo kwa wanajeshi, risasi na kila kitu," mkuu wa Wagner Yevgeny Prigozhin alisema katika video iliyotolewa kwenye mtandao wa kijamii.

"Tunarudi nyuma, tunapumzika, tunajiandaa na kisha tutapata kazi mpya," aliongeza Prigozhin, ambaye alikuwa amevaa vazi lisilopenya riasi na kofia ya kijeshi. Mapema wiki hii, alikiri kwamba karibu wafungwa 10,000 aliokuwa amewaandikisha kupigana nchini Ukraine waliuawa kwenye uwanja wa vita.

Mshirika huyo wa Kremlin mwenye umri wa miaka 61 alizuru magereza ya Urusi mwaka jana ili kuwashawishi wafungwa kupigana na Wagner ili kupata msamaha ulioahidiwa watakaporejea -- iwapo watanusurika.

Chanzo: Mashirika