1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Eneo la mpakani kati ya Urusi na Ukraine laendelea kuwa tete

Daniel Gakuba
24 Mei 2023

Maafisa katika mkoa wa Urusi wa Belgorod unaopakana na Ukraine wamesema eneo la karibu na mpaka limekabiliwa na mashambulizi mengi ya ndege zisizo na rubani. Urusi inaishutumu Ukraine kuhusika na mashambulizi hayo.

https://p.dw.com/p/4RkRi
Russland Belgorod | Kämpfe | Schäden in der Region Belgorod
Picha: Governor of Russia's Belgorod Region Vyacheslav Gladkov via Telegram/ via REUTERS

Gavana wa mkoa huo wa Belgorod, Vyacheslav Gladkov amearifu leo kuwa mashambulizi yameharibu majengo ya utawala, makaazi ya watu na magari, na kuongeza kuwa idadi kubwa ya ndege zisizo na rubani, au droni zilizohusika imedunguliwa.

Soma zaidi: Mji wa Belgorod washambuliwa kwa ndege zisizo na rubani

Eneo hilo la magharibi mwa Urusi limekumbwa na hujuma kwa miezi kadhaa sasa, na Moscow inadai mawakala wa Ukraine wamekuwa wakiyafanya mashambulizi hayo kwa kutumia maguruneti na mizinga.

Ripoti ya Urusi imesema kuwa tangu Jumatatu, dazeni kadhaa za iliowaita ''wawakilishi wa vikosi vya jeshi la Ukraine'' wamekuwa wakiendesha operesheni katika mkoa huo. Hapo jana, jeshi la Urusi liliondoa hali ya dharura iliyokuwa imetangazwa katika eneo hilo, likisema lilichokitaja kuwa ni ''operesheni dhidi ya magaidi'' ilikuwa imemalizika.

Image issued by Russian Ministry of Defense | Belgorod | Kämpfe | verbrannte Fahrzeuge angeblicher ukrainischer Saboteure
Urusi imedai zana za kivita zilizotengenezwa nchini Marekani zimeharibiwaPicha: Russian Defence Ministry/TASS/picture alliance

Maandalizi ya uwanja wa mapigano

Ukraine imekanusha kuhusika katika hujuma hizo, ikisema badala yake kuwa operesheni hizo zinafanywa na wazalendo raia wa Urusi wanaopinga utawala wa rais Vladimir Putin.

Akizungumzia kinachoendelea katika eneo hilo la mpaka baina ya Urusi na Ukraine, mtaalamu wa masuala ya kijeshi aliyeko mjini London, Mark Galeotti amesema yumkini lengo lake ni kuandaa mazingira ya Ukraine kuanzisha harakati zake za kuyakomboa maeneo yanayokaliwa na Urusi.

Soma zaidi: Urusi yadai kuwasambaratisha wanamgambo waliovamia Belgorod

''Pengine hiki ni kile ambacho katika lugha ya kijeshi kinajulikana kama kuandaa mazingira kwenye uwanja wa mapambano, kwa ajili ya mashambulizi ya kulipa kisasi ya Ukraine ambayo hayaepukiki,'' amesema Galeotti na kuongeza kuwa ''lengo la kwanza ni kuitia wasiwasi Urusi juuya kuwepo kwa uasi wa ndani, na lengo la pili ni kuifanya Urusi iwatawanye wanajeshi wake, ikiwapeleka baadhi yao kutoa msaada katika mkoa wa Belgorod.''

Image by Russian State Agency TASS | Russland Belgorod | Kämpfe | Einwohner Grayvoron-Distrikt
Idadi kadhaa ya raia wamejeruhiwa katika mapigano ndani ya mkoa wa BelgorodPicha: Pavel Kolyadin/Tass/picture alliance

Mbali na Ukraine, Urusi pia iliihusisha Marekani na matukio katika mkoa huo wa Belgorod, ikichapisha picha za zana za kijeshi zinazotengenezwa nchini Marekani iliyodai ziliharibiwa katika operesheni ya kupambana na wavamizi. Marekani imezipinga tuhuma hizo.

Kiongozi wa kundi la Wagner aonya kuwa Urusi inabweteka

Huku hayo yakijiri, kamanda wa kundi binafsi la wapiganaji la nchini Urusi la Wagner, Yevgen Prigozhin ameonya juu ya uwezekano wa Urusi kukumbwa na vuguvugu la mapinduzi mithili ya lile la mwaka 1917, na kwamba hali hiyo inaweza kuisababishia nchi hiyo kuvipoteza vita vyake dhidi ya Ukraine.

Soma zaidi:Urusi yadai Ukraine imehusika kushambulia eneo lake la mpakani la Belgorod

Prigozhin amesema njia pekee ya kuiepusha hali hiyo ni ikiwa kundi la watu wenye ushawishi nchini Urusi litaacha mzaha katika kupigana vita hivyo. Amesema kuna dhana nchini Urusi kuwa nchi za magharibi zitachoka na vita, na kwamba China itafanikiwa kuusuluhisha mgogoro huu, na kuongeza kuwa binafsi anaamini kuwa dhana hiyo haina mashiko.

Vyanzo: dpae,rtre