1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yakataa kuwa Prigozhin alikuwa tayari kulisaliti dola

15 Mei 2023

Mkuu wa kundi la wanajeshi wa kukodi wa Urusi, Wagner, amepuzilia mbali ripoti ya gazeti moja la Marekani kwamba alikuwa tayari kuisaliti Urusi, huku Ikulu ya Kremlin ikiitaja ripoti hiyo kama "uwongo."

https://p.dw.com/p/4RNPH
Russland Chef Söldner-Truppe Wagner Jewgeni Prigoschin
Picha: Konkord Company/Tass/IMAGO

Gazeti la Washington Post likinukuu ripoti ya kijajusi ya Marekani, limesema mkuu wa Wagner, Yevgeny Prigozhin, alikuwa tayari kufichua kwa jeshi la Ukraine sehemu walizokuwepo wanajeshi wa Urusi, kwa sharti kuwa Ukraine itawarudisha nyuma wanajeshi wake mjini Bakhmut.

Gazeti hilo limeendelea kuripoti kuwa, ofa ya mkuu huyo wa Wagner ya kufichua sehemu waliko wanajeshi wa Urusi ilikataliwa na Ukraine ambayo haikumuamini. 

Prigozhin ameibuka kuwa mkosoaji mkubwa wa jeshi la Urusi, akiwashutumu makamanda wa jeshi hilo kwa kuwasiliti wapiganaji wake katika uwanja wa mapambano.

Wapiganaji wa Wagner wamekuwa katika mstari wa mbele kwenye uwanja wa mapambano katika mji wa mashariki wa Bakhmut ambao umeshuhudia vita vya muda mrefu kati ya jeshi la Ukraine na wapiganaji wa Urusi.