1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC: Kundi la M23 na Rwanda wanavuruga safari za ndege

30 Julai 2024

Serikali ya Jmahuri ya Kidemokrasi ya Kongo imewashtumu waasi wa kundi la M23 na vikosi vya jeshi la Rwanda vinavyowaunga mkono waasi hao kwa kuvuruga mfumo wa mawasiliano ya safari za ndege.

https://p.dw.com/p/4iuAx
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo | Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa N'djili mjini Kinshasa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa N'djili mjini KinshasaPicha: Arsene Mpiana/AFP/Getty Images

Hayo yanaelezwa kutokea  katika mkoa wa mashariki wa Kivu Kaskazini, ambako jeshi la Kongo linapambana dhidi ya waasi wa M23. Hata hivyo baadhi ya wadau wameitaka serikali kuacha kuilamu Rwanda kila mara na badala yake itafute suluhisho la matatizo yake.

Katika taarifa yake jana Jumatatu, serikali ya Kongo ilisema kuwa imechunguza mfumo wa mawasiliano ya safari za anga wa GPS ambao ulikuwa ukitatiza usafiri wa anga, na kusema wachunguzi walifuatilia hujuma ya kudukuliwa kwa mfumo huo na kubaini unafanywa na Jeshi la Ulinzi la Rwanda, RDF na M23.

Udukuzi na kitisho cha usafiri wa anga nchini Kongo

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo | Ziwa Kivu
Mkoa wa Kivu Kusini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mwanzoni mwa Februari, 2024.Picha: ALEXIS HUGUET/AFP

Hujuma hiyo ni kitisho kwa usalama wa umma, lakini serikali inapaswa kufikiria kuisambaratisha  teknolojia ya Rwanda badala ya kupiga kelele za kuomba msaada," alisisitiza Placide Nzilamba, mwanachama mtendaji wa jamii ya kiraia ya mkoa wa Kivu Kaskazini.

Zaidi anasema "Serikali inapaswa kuwa na aibu kwa kila mara kupiga kelele za msaada, hasa kwa suala muhimu kama hili linalohusu usalama wa umma. Ni wakati wa kupanga majibu na kusambaratisha vifaa vyote ambavyo Rwanda inatumia kuishambulia DRC. "

Nzilamba aliongeza kwa kusema dunia nzima tayari imeelewa tatizo hilo na inaonyesha unafiki. Ni juu yao kujikomboa na vitisho hivi na siyo kungojea wengine. Kwa hiyo, wanaiomba serikali ianze kufanya kazi vizuri na kumvurga adui ambaye ni Rwanda kwa kusababisha ukosefu wa usalama kwa watu wa Kongo.

Hakuna juhudi za ndani katika kutatua tatizo la uingiliwaji wa usafiri wa anga

Kwa upande wake serikali haikueleza kwa undani, ukubwa wa athari zilizopo kwa usafiri wa anga, ambao unahusisha safari za abiria za ndani, za kijeshi na za ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa mkoani Kivu Kaskazini. Ilisema imewasilisha malalamiko kwa tawi la kikanda la Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga ili kuomba vikwazo vinavyostahili.

Kundi la M23 linaloongozwa na jamii ya Watutsi limekuwa likiendesha uasi mpya katika eneo la mashariki mwa Kongo tangu mwaka 2022. Juhudi za kijeshi za kuwarudisha nyuma zimeongezeka katika mwaka uliopita kwa kutumia droni na ndege za kivita.

Serikali ya Kongo, Umoja wa Mataifa, Marekani na mataifa mengine ya magharibi zinaishtumu Rwanda kwa kuunga mkono kundi hilo la waasi, shutuma ambazo Rwanda inazikanusha. Jeshi la Rwanda, M23 na Ujumbe wa MONUSCO  hawakutoa kauli kuhusu tuhuma hizo za serikali ya Kongo.

Soma zaidi:Milio ya mabomu yarindima karibu na Goma, DR Congo

Mapigano katika mkoa wa Kivu Kaskazini yamewahamisha zaidi ya watu milioni 1.7, na kufanya idadi jumla ya Wakongo waliokoseshwa makaazi yao na mizozo kadhaa kuwa milioni 7.2, kwa mujibu wa makadirio ya Umoja wa Mataifa.

DW, Goma