1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Milio ya mabomu yarindima karibu na Goma, DR Congo

27 Juni 2024

Serikali ya DRC yaahidi kusaka ufumbuzi wa haraka wa matatizo yanayowakabili wakaazi wa Goma

https://p.dw.com/p/4hbLv
Milio ya mabomu yasikika umbali wa kilomita 170 kutoka Goma
Milio ya mabomu yasikika umbali wa kilomita 170 kutoka GomaPicha: Wang Guansen/Xinhua/picture alliance

Wakati mapigano baina ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na waasi wa M23 yakiendelea kupamba moto katika baadhi ya maeneo mkoani Kivu Kaskazini. Waziri Mkuu Judith Suminwa ameutembelea mji wa Goma pamoja na makambi ya wakimbizi karibu na mji huo unaokabiliwa na kitisho cha usalama. Waziri mkuu huyo amewaahidi wakaazi wa huko kuwa serikali mjini Kinshasa inasaka ufumbuz wa haraka wa matatizo yanayowakabili, likiwamo hilo la ukosefu wa usalama. 

Ikiwa ni mara ya kwanza kulizuru eneo hilo miezi miwili baada ya kuteuliwa kama waziri mkuu wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Judith Suminwa alitumia fursa hii kukutana na viongozi wa asasi za kiraia ambapo walijadiliana kuhusu swala la usalama mkoani Kivu Kaskazini.

Soma pia: Mapigano kati ya wanajeshi wa FARDC na waasi wa M23 yaendelea

Akizungumza na vyombo vya habari muda mchache baada ya majadiliano hayo hapo jana, Waziri Mkuu huyo alisema kuwa alifanya ziara hiyo ili kuwaletea matumaini maelfu wa raia  wanaohangaishwa na vita:

"Ni kweli matatizo tunayajua, lakini ni muhimu siku zote kufika, kukutana na wananchi, kuonana na viongozi wa serikali za mitaa, viongozi wa kimila na kuweza kuzungumza nao. Ni muhimu kuwa na uwezo wa kuweka mbinu mpya za dharura kama sehemu ya utekelezaji wa mpango wa serikali na kwa upande wangu, kwa kweli ni njia ya kuonyesha mshikamano na watu hawa wastahimilivu, hasa wanawake."

Soma pia: AU walaani mauaji ya watu wengi nchini DR Congo

Waziri Mkuu wa DR Congo Judith Suminwa
Waziri Mkuu Suminwa amefanya ziara yake hapa wakati milio ya mabomu ikisikika mchana kutwa wa jana kutokea vijiji jirani na mji wa Kanyabayonga umbali wa kilometa 170  kutokea mjini Goma.Picha: BENOIT DOPPAGNE/Belga/IMAGO

Kiongozi huyo anayeongoza ujumbe wa mawaziri wengine kutoka serikali kuu ya Kinshasa, aliitembelea kambi ya wakimbizi ya Lushagala nje kidogo na mji wa Goma, ambako watu zaidi ya 30 waliuawa mapema mwanzoni mwa mwezi wa mei baada ya kuangukiwa na bomu lililorushwa na waasi wa M23,  kulingana na vyanzo vya kijeshi.

Ripoti mbalimbali za mashirika ya kiutu zinakadiria kuwa zaidi watu milioni 2 .7 wamehifadhiwa katika makambi baada ya kukimbia vurugu za vita katika wilaya za Masisi, Rusthuru na Nyiragongo, ambako hali inaendelea kuwa tete.

Soma pia: Takriban raia 11 wameuawa mashariki mwa DR Congo

Ombi kubwa la wakimbizi waliomo kwenye makambi haya ya wakimbizi ni upatikanaji wa amani badala ya ziara zisizomaliza vita, wamesema wananchi hao waliokuja kumlaki waziri mkuu huyo katikati mwa kambi hiyo ambamo upatikanaji wa maji safi na vyakula umekuwa ni jinamizi kubwa:

Akizungumza na DW, John Banyene, afisa mkuu wa asasi za kiraia mkoani kivu kaskazini ameelezea pia hisia zake:

"Sisi kama wananchi tunacho ihitaji kwa serikali ni kufuta ushuru unaotozwa kwetu kufuatia hali mbaya tunayoipitia kwa sasa. Sababu barabara zote zimefungwa na kwetu imekuwa ni vigumu kukidhi kwa mahitaji yetu. Maeneo yanayokaliwa na waasi huwa raia wanateseka sababu ya bei ghali ya kodi. Kwa hiyo tunamuomba waziri mkuu kushughulikia swala hilo."

Miaka mitatu baada ya uasi wa M23 kuanza, wamefanikiwa hadi sasa kulichukua eneo kubwa kwenye wilaya za Rutshuru na Masisi ambako wanatuhumiwa kuanza kujishughulisha na uchimbaji  haramu wa madini kwenye mji wa kimkakati wa Rubaya , walioudhibiti mapema mwanzoni mwa mwezi wa Mei.

Kwenye uwanja wa ndege mjini Goma Waziri Suminwa Tuluka alirusha njiwa wawili wenye rangi nyeupe angani kama ishara ya kuhimiza amani mashariki mwa jamuhuri ya Kidemokrasia ya kongo.