Senegal yaahirisha uchaguzi wa rais hadi Desemba 15
7 Februari 2024Muswada huo ulipitishwa kwa kura 105 dhidi ya kura moja iliyopinga, baada ya wabunge wa upinzani kuondolewa bungeni kwa nguvu.
Kuahirishwa kwa uchaguzi mkuu nchini Senegal kunammpa nafasi rais wa sasa Macky Sall, kubakia madarakani hadi pale mrithi wake atakapopatikana, licha ya wasiwasi uliopo juu ya kuvurugwa kwa demokrasia nchini humo.
Ayib Daffe ambaye ni mbunge wa upinzani amesema hali inayoshuhudiwa inasikitisha huku mwenzake Babacar Abba Mbaye akisema waliondolewa bungeni kwanguvu ili mswada upitishwe kwa urahisi.
Vurumai yazuka baada ya bunge la Senegal kuahirisha uchaguzi wa rais
Wakati mswada huo ulipokuwa unapitishwa, maafisa wa usalama waliwarushia gesi za kutoa machozi wafuasi wa upinzani waliokusanyika katika makundi madogo nje ya bunge mjini Dakar, wakibeba mabango na kusema kwa sauti "Macky Sall ni dikteta". Malick Diouf, mmoja ya waandamanaji aliye na miaka 37 amesema hana mgombea anaempendelea na wala hana kadi ya kupigia kura lakini ameona ni muhimu kushiriki maandamano kupinga kile alichokiita mapinduzi ya demokrasia.
Kiongozi wa upinzani Senegal alikosoa vikali kuahirishwa uchaguzi huo akisema ni sawa na mapinduzi ya katiba na mashambulizi ya demokrasia. Hapo jana serikali ilikata mtandao wa mawasiliano ya simu za mkononi ikisema inazuwia jumbe za chuki kusambaa katika mitandao ya kijamii.
Jumuiya ya kimataifa ina wasiwasi wa hali ilivyo Senegal
Hofu imetanda nchini Senegal kuanzia siku ya Jumamosi, wakati Rais Macky Sall alipotangaza kuahirisha uchaguzi wa rais uliotarajiwa kufanyika Februari 25, hatua hiyo ilichukuliwa saa kadhaa kabla ya kuanza kwa kampeni rasmi za uchaguzi. Sall amesema alichukua uamuzi huo baada ya mvutano kati ya bunge na Baraza la katiba kufuatia kukataliwa kwa wagombea wao.
Muswada wa kuahirisha uchaguzi uliwasilishwa bungeni na kamati ya maandalizi ya bunge na kuungwa mkono na chama tawala, kilichoshindwa kumpata mgombea wa pamoja atakayemrithi Sall. Kuahirishwa kwa zoezi hilomuhimu kumeipa wasiwasi Jumuiya ya Kimataifa huku Marekani, Umoja wa Ulaya na Ufaransa wakiomba uchaguzi ufanyike haraka iwezekanavyo.
Wabunge Senegal kukutana baada ya rais kuahairisha uchaguzi
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat ametaka kuwepo kwa mazungumzo ya kutatua mgogoro huo wa kisiasa. Kwa upande mwengine shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch limesema Senegal iko katika hatari ya kupoteza sifa yake kama taifa Imara kidemkorasia.
Rais Macky Sall awali alisema atatumikia kipindi chake cha muhula miwili lakini hivi karibuni ghasia zimekuwa zikishuhudiwa nchini humo juu ya hofu kwamba Sall huenda akajaribu kurefusha muda wake madarakani.
Vyanzo: afp/dpa