1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSenegal

Vurumai yazuka baada ya bunge la Senegal kuahirisha uchaguzi

6 Februari 2024

Bunge la Senegal limepiga kura jana kuahirisha uchaguzi wa urais hadi Disemba 15, hatua ambayo imezua wasiwasi wa kimataifa kuhusu nchi hiyo ambayo inachukuliwa kama kinara wa demokrasia Afrika Magharibi.

https://p.dw.com/p/4c5dM
Maandamano ya upinzani nchini Senegal
Polisi wa kutuliza ghasia wakipambana na waandamanaji kwenye mji mkuu wa Senegal, Dakar.Picha: John Wessels/AFP

Muswada huo wa kuusogeza mbele uchaguzi ulipitishwa na wabunge 105 kwa kura za ndio huku mmoja tu akiupinga, baada ya wabunge wa upinzani kuondolewa kwa nguvu bungeni.

Kupitishwa kwa muswada huo kunamfungulia njia Rais Macky Sall kusalia madarakani hadi mrithi wake atakapotangazwa licha ya wasiwasi unaoongezeka kuhusu mmomonyoko wa demokrasia.

Rais Sall ambaye amehudumu kwa mihula miwili madarakani, alipaswa kuondoka madarakani mnamo Aprili 2. Awali, alisema hana nia ya kuongeza muda wake madarakani japo kutokana na hali inavyoendelea, upinzani umeonyesha mashaka.