1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin asema maslahi ya Urusi hayana mjadala

23 Februari 2022

Rais wa Urusi Vladmir Putin amesema Jumatano maslahi ya nchi yake hayana mjadala, huku Moscow ikilundika zaidi ya wanajeshi 150,000 kwenye mipaka na Ukraine, na mataifa ya magharibi yakiiadhibu Urusi kwa vikwazo vipya.

https://p.dw.com/p/47SZm
Ukraine Konflikt | Russland PK Putin
Picha: Sergey Guneev/Kremlin/Planet Pix/Zuma/dpa/picture alliance

Katika ujumbe wa vidio wakati wa maadhimisho ya siku ya watetezi wa taifa, ambayo ni siku ya mapumziko nchini humo, Putin amelipongeza jeshi la Urusi na kusifu utayarifu wa jeshi hilo kuingia vitani, baada ya kuashiria mipango ya kupeleka wanajeshi ndani ya Ukraine.

"Nchi yetu mara zote iko tayari kwa mazungumzo ya kweli na ya wazi, kwa ajili ya kutafuta suluhisho la kidiplomasia kwa matatizo magumu zaidi," Putin alisema.

Soma pia: Urusi yatambua rasmi uhuru wa majimbo ya Ukraine

Lakini akaongeza: "Maslahi ya Urusi, na usalama wa raia wetu ni mambo yasio na mjadala kwetu. Kwa hiyo tutaendelea kuimarisha na kuendeleza jeshi letu na jeshi la wanamaji, kuongeza ufanisi wao, na kuwapa vifaa vya kisasa zaidi."

Ukraine Russland Konflikt | Wladimir Putin
Rais Vladmir Putin akiongoza kikao cha baraza la usalama la taifa katika ikulu ya Kremlin, Februari 21, 2022.Picha: Kremlin Pool Photo/Sputnik/AP Photo/picture alliance

Putin alizungumza baada ya baraza la juu la bunge la Urusi, jana jioni kumpa idhini kwa sauti moja, kupeleka vikosi vya kulinda amani kwenye mikoa mwili iliyojitenga nchini Ukraine, ambayo hivi sasa inatambuliwa na Moscow kama huru, na yumkini katika maeneo mengine ya Ukraine.

Jumanne usiku Urusi ilisema imeanzisha uhusiano wa kidiplomasia kwa ngazi ya ubalozi na mikoa hiyo iliyotangaza kujitenga na Ukraine mwaka 2014, katika mzozo uliosababisha vifo vya watu 14,000 mpaka sasa.

Soma pia: Viongozi wa dunia wailaani Urusi kuhusu Ukraine

Akizungumza na waandishi habari jana jioni, Putin aliorodhesha masharti makali ikiwa mataifa ya magharibi yanataka kutuliza mzozo huo, akisema Ukraine, ambayo inaelemea upande wa magharibi inapaswa kuachana na mipango yake ya kujiunga na NATO, na kubaki bila upande.

Marekani, washirika watangaza vikwazo vikali

Rais wa Marekani Joe Biden, siku ya Jumanne alitangaza vikwazo vipya vikali dhidi ya Urusi, lakini alisema bado kuna muda wa kuepusha vita. Japana na Australia zilifuata mara moja mapema leo kwa kutangaza vikwazo vyao vikali kwa Moscow na watu wanaohusishwa na uhasama dhidi ya Ukraine.

Ukraine-Konflikt | Präsident Biden unterschreibt Sanktionen für Russland
Rais wa Marekani Joe Biden akisaini vikwazo vipya dhidi ya Urusi akiwa katika ofisi yake ndani ya ikulu ya White House, Februari 21, 2022.Picha: Adam Schultz/White House/Planet Pix/Zuma/dpa/picture alliance

Ujerumani pia ilitangaza kusitisha mchakato ya kuidhinisha mradi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Urusi kwenda nchini humo, linalojulikana kama Nord Stream 2. Lakini Urusi imejigamba na kusema vikwazo hivyo vitaenda upogo.

Soma pia: Urusi yakabiliwa na vikwazo

Mipango ya Putin imesalia kuwa kitendawili, lakini maafisa wa magharibi wamekuwa wakionya kwa wiki kadhaa kwamba amekuwa akijiandaa kwa ajili ya uvamizi kamili wa Ukraine, hatua ambayo inaweza kusababisha vita mbaya barani Ulaya.

Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg, amsema muungano huo wa kijeshi una kila ishara kwamba Moscow inaendelea kupanga shambulio kamili dhidi ya Ukraine.

Chanzo: Mashirika

Mhariri: Josephat Charo