1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden na Putin kukutana kujadili mgogoro wa Urusi/Ukraine

21 Februari 2022

Rais wa Marekani Joe Biden na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin wameridhia kukutana katika hatua za mwisho mwisho za kidiplomasia kujaribu kuepusha uwezekano wa Urusi kuivamia Ukraine.

https://p.dw.com/p/47Kyk
Kombobild Joe Biden und Wladimir Putin
Picha: AFP

Mkutano kati ya viongozi hao wawili wa Marekani na Urusi umeandaliwa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliyezungumza na pande zote mbili kwa njia ya simu. Ofisi ya Macron imesema Biden na Putin wamekubaliana kukutana na baadaye pia wamekubaliana kukutana na pande zote husika katika mgogoro wa Ukraine na Urusi ili kujadili masuala muhimu ya usalama na uthabiti wa Ulaya. Ofisi hiyo imesema mkutano huo utafanyika kwa masharti ya Urusi kutothubutu kuivamia Ukraine.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Jen Psaki amesema nchi yake iko wazi kabisa katika suala hili kwamba wamejitolea kutumia diplomasia hadi pale uvamizi utakapofanyika akisema kwa sasa Urusi inaonekana kuendelea kujitayarisha kuishambulia Ukraine.

soma zaidi: NATO yasema Urusi inapanga shambulio kamili dhidi ya Ukraine

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Anthony Blinken, na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov, watakutana siku ya alhamisi kujadili ajenda za mkutano wa marais wao. Ikulu ya Urusi haijatoa maoni yoyote juu ya kukutana kwa Biden na Putin lakini siku zote imekuwa ikisema Putin yuko tayari kwa mazungumzo ya aina yoyote ile.

Mkutano huo unatoa matumaini ya kuzuwia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ambako maafisa wa Marekani wamesema huenda ukatokea wakati wowote kutokana na wanajeshi zaidi ya 150,000 wa Urusi kujikusanya karibu na mpaka wa Ukraine

Borrell asema diplomasia ikishindwa vikwazo vitachukua nafasi yake

Frankreich | EU Verteidigunsministertreffen | PK Josep Borrell
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep BorrellPicha: AFP via Getty Images

Huku hayo yakiarifiwa Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, amekaribisha hatua ya kufanyika mkutano wa kilele kati ya Putin na Biden lakini akaonya kuwa iwapo diplomasia itashindwa, Umoja huo wa nchi wanachama 27, umeshakamilisha vikwazo vitakavyowekewa Urusi iwapo itaivamia Ukraine. Halmashauri ya Umoja wa Ulaya pia kupitia rais wake, Ursula von der Leyen, imesema imekwishatayarisha vikwazo vengine vitakavyoizuwia Urusi kufikia masoko ya kifedha vikwazo vinavyoulenga moja kwa moja uchumi wa taifa hilo.

soma zaidi: Urusi yawakosoa viongozi wa Magharibi kutabiri vita na Ukraine

Urusi kwa upande wake imeendelea kukanusha mipango yoyote ya ya uvamizi huo. Msemaji wa Rais Putin, Dmitry Peskov, amesema Urusi haina haja ya kushambulia huku akiwatolea mwito washirika wao wa Magharibi kufikiria wanachokisema. Peskov  amesema kutokana na historia ya Urusi haijawahi kumshambulia yoyote na urusi iliyopitia vita vingi ni taifa ambalo haliwezi kutamka hata neno vita.

Kwengineko Mawaziri wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kuujadili mgogoro wa Urusi na Ukraine katika mkutano wao mjini Brussels leo Jumatatu kufuatia mashambulizi yaliyopamba moto katika eneo la Donbass Mashariki mwa Ukraine, kati ya vikosi vya serikali na d putinwatu wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi. Zaidi ya watu 14,000 wameuwawa tangu kuanza kwa mashambulizi katika eneo hilo mwaka 2014 muda mfupi baada ya Urusi kunyakua rais ya Krimea kutoka kwa Ukraine.

 

Chanzo: afp/reuters