1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ANC chasaka washirika kuunda serikali

Angela Mdungu
4 Juni 2024

Chama tawala cha Afrika ya Kusini cha African National Congress (ANC) kipo njiapanda katika juhudi zake za kutafuta washirika kinachoweza kuunda nao serikali ya pamoja.

https://p.dw.com/p/4gccN
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa akiwa katikati ya maafisa wengine wa serikaliPicha: Emilio Morenatti/AP/dpa/picture alliance

Kinakabiliwa na changamoto hiyo baada ya kupoteza wingi wa viti vya bunge katika uchaguzi uliofanyika wiki iliyopita ikiwa ni mara ya kwanza tangu kilipoingia madarakani miaka 30 iliyopita.

Vyama vyenye uwezekano wa kuunda ushirika na chama cha ANC vyenye itikadi tofauti zinazokinzana ni pamoja na Demokratic Alliance, chama cha aliyekuwa Rais wa zamani Jacob Zuma cha uMkhonto we Sizwe pamoja Economic Freedom Fighters (EFF).

Soma zaidi: Ramaphosa apigia debe umoja baada ya matokeo mabaya ya ANC

Licha ya tofauti hizo, katibu mkuu wa ANC Fikile Mbalula alishasema Jumapili baada ya matokeo ya uchaguzi kuwa, chama chake kiko tayari kushirikiana na vya vyama vingine.

Huku mwelekeo wa sera ya serikali ukiwa mashakani, kamati ya maafisa 27 wa chama hicho ilipangwa kukutana Jumatatu na itawasilisha mapendekezo juu ya kinachoweza kufanyika mbele ya kamati kuu ya kitaifa ya ANC Jumanne.

Baadhi ya vyama vyaandaa wawakilishi wa mazungumzo ya kuunda serikali

Afrika Kusini | Siasa | Kiongozi wa chama cha upinzani Julius Malema
Kiongozi wa chama cha upinzani Afrika Kusini Julius MalemaPicha: Thuso Khumalo/DW

Chama cha DA na chama kidogo cha  Inkatha Freedom (IFP) vilishatangaza kuwa vimeandaa timu za wawakilishi wao kwa ajili ya majadiliano na vyama vingine. Vyama hivyo ni sehemu ya muungano ulioanzishwa kabla ya uchaguzi.

Katika uchaguzi uliofanyika Mei 29, chama cha DA kilishika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 21.8 ya kura zote zilizopigwa. Chama cha MK kilishika nafasi ya tatu kwa kupata asilimia 14.9 wakati EFF kilijizolea asilimia 9.5 ya kura na IFP asilimia 3.9

Soma zaidi: Chama cha ANC kuanza kuunda serikali ya mseto

Kulingana na katiba ya Afrika ya Kusini, bunge jipya lililotokana na uchaguzi huo linapaswa kuanza kazi ndani ya wiki mbili baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi na moja ya majukumu yake ya awali ni kumchagua Rais ajaye wa taifa hilo. 

Baadhi ya wachambuzi nchini humo wanasema licha ya changamoto zinazoweza kujitokeza katika kupata washirika wa kuunda serikali, kuna uwezekano mkubwa wa ANC kushirikiana na chama cha DA kwani chama hicho kimekuwa na historia nzuri katika ngazi ya mkoa wa Western cape unakopatikana mji mkubwa wa kitalii wa Cape town.