1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAfrika Kusini

Ramaphosa apigia debe umoja baada ya matokeo mabaya ya ANC

3 Juni 2024

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametoa wito kwa viongozi wa vyama nchini humo kufanya kazi pamoja kwa ajili ya umma wa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/4gZXc
Afrika Kusini| Pretoria | Cyril Ramaphosa
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini akihutubia taifa baada ya matokeo kamili ya uchaguzi wa taifa na majimbo kutangazwa. Picha: UPI Photo/IMAGO

Ramaphosa ameyasema haya baada ya chama chake cha African National Congress, ANC, kupoteza wingi wake wa miaka 30 bungeni katika uchaguzi mkuu nchini humo.

Lakini katika kile kinachoashiria msukosuko unaotarajiwa siku chache zijazo, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyechafuliwa na tuhuma za ufisadi Jacob Zuma, alisusia hafla ya kutangazwa kwa matokeo na chama chake kimekataa kuyatambua.

Hesabu za mwisho zimeonesha chama cha ANC kimepata viti 159 kati ya 400 katika bunge la nchi hiyo, kikifuatiwa na  Democratic Alliance kilichopata viti 87 na uMkhonto weSizwe cha Zuma kilichopata viti 58.