1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaidhinisha Ukraine itumie silaha iishambulie Urusi

31 Mei 2024

Rais Joe Biden wa Marekani ameidhinisha Ukraine itumie silaha ilizopewa na Marekani kuyashambulia maeneo ya Urusi yanayotumiwa kuishambulia.

https://p.dw.com/p/4gVqn
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Antony Blinken
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Antony BlinkenPicha: Petr David Josek/picture alliance/AP

Rais wa Marekani Joe Biden ameidhinisha Ukraine itumie silaha za Marekani kuyashambulia maeneo yaliyo katika ardhi ya Urusi ambayo yanaushambulia mji wa Ukraine wa Kharkiv, baada ya serikali ya mjini Kyiv kuomba idhini kutoka kwa serikaldi ya mjini Washington katika wiki chache zilizopita. Taarifa hiyo imethibitishwa leo na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi habari mjini Prague baada ya mkutano usio rasmi wa mawaziri wa mambo ya nje wa jumuiya ya kujihami, NATO, Blinken hakusema hasa ikiwa uidhinishaji alioutoa Biden huenda ukatanuka kujumuisha miji mingine ya Urusi na maeneo yaliyo ndani kabisa nchini Urusi.

Blinken amesema hatua ya Marekani, ambayo ni mageuzi makubwa katika sera ya rais Biden, ambaye amekuwa akipinga kuruhusu Ukraine itumie silaha za Marekani kwa mashambulizi nchini Urusi, imetokana na mkakati wa Marekani wa kuendana na hali halisi katika uwanja wa vita. Blinken pia amesema sasa Marekani inachukua hatua kutokana na kile ilichokiona ndani na nje katika viunga vya eneo la Kharkiv.

Ukraine na Urusi zabadilishana wafungwa

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amethibitisha kwamba wizara ya ulinzi ya Urusi imesema wanajeshi 75 wa Urusi waliokuwa katika hatari kubwa wamekabidhiwa kwa majeshi ya Ukraine. Pande zote mbili zimebadilishana miili ya wanajeshi waliokufa, huku Ukraine ikipokea mabaki ya miili 212, na Urusi ikipokea 45. Ukraine na Urusi zilibadilishana wafungwa mara ya mwisho mnamo Februari mwaka huu.

Siku mbili zilizopita, mwanaharakati wa haki za binadamu wa Urusi, Tatyana Moskalkova, aliutuhumu upande wa Ukraine kwa kuvuruga mchakato huo wa mabadilishano, akisema Ukraine ilikuwa ikiwasilisha matakwa mapya mara kwa mara.

Rais Zelensky yuko mjini Stockholm kusaini makubaliano ya ulinzi na Sweden, Iceland na Norway huku nchi za Magharibi zikiimarisha uungwaji mkono wake kwa nchi iliyovamiwa na Urusi Februari 2022. Mkutano huo umefanyika huku serikali ya Ujerumani ikisema imeidhinisha Ukraine itumie silaha ilizopewa na Ujerumani dhidi ya maeneo yanayotumiwa kuendeshea shughuli za kijeshi nchini Urusi.

Soma pia: Ulaya yagawika kuhusu Ukraine kutumia silaha za Magharibi ndani ya Urusi

Wakati haya yakairifiwa, katibu mkuu wa jumuiya ya kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg, amezitolea wito nchi wanachama ziahidi kutoa fedha zaidi kwa ajili ya Ukraine. Akizungumza katika mkutano wa NATO mjini Prage, Jamhuri ya Czech, Stoltenberg amesema, ”Sote tunataka kuvifikisha mwisho vita hivi, lakini kitendawili ni kwamba kadri tunavyojiandaa kwa kipindi kirefu, ndivyo vita hivi vinavyoweza kufika mwisho mapema. Urusi lazima ielewe haiwezi kutusubiri. Hakuna maamuzi ya mwisho yaliyopitishwa katika kikao cha leo lakini tumepiga hatua katika masuala matatu."

China yasema ni ngumu kushiriki mazungumzo kuhusu Ukraine

China imesema hivi leo kwamba itakuwa vigumu kutimiza miito ya mazungumzo kuhusu vita baina ya Urusi na Ukraine, ikidokeza kuwa ina matatizo na mipangilio inayoonekana kuelekea msimamo wa serikali ya mjini Beijing kuingua mkono Urusi. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China, Mao Ning amesema matumaini na matakwa ya China yanaonekana kuwa vigumu kutimizwa kwenye mkutano huo uliopangwa kufanyika nchini Sweden.

Mao pia amesema bado kuna mwanya ulio wazi kati ya maandalizi ya mkutano na matakwa ya upande wa China, pamoja na matarajio jumla ya jumuiya ya kimataifa. Mao hakutoa maelezo yoyote lakini akasema China imezifahamisha pande husika kuhusu wasiwasi wake na itaendelea kuwasiliana na pande zote zinazohusika.

(dpa, reuters, ap)