1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Ulaya yagawanyika Ukraine kutumia silaha za magharibi Urusi

29 Mei 2024

Mawaziri wa ulinzi wa Umoja wa Ulaya waliokutana mjini Brussels walishindwa kufikia makubaliano kuhusu kama Ukraine inapaswa kuruhusiwa kutumia silaha wanazoipa, kuyapiga maeneo ndani ya Urusi.

https://p.dw.com/p/4gObp
Vifaru vya kijeshi aina ya AS90
Wanajeshi wa Ukraine walipewa mafunzo ya kutumia vifaru vya kufyatua mizinga kutoka UingerezaPicha: Ben Birchall/empics/picture alliance

Nchi za Umoja wa Ulaya zilikuwa tayari zimekubali kwa pamoja kutoa msaada wa kijeshi kwa Ukraine. Lakini wakati baadhi ya wanachama wanatoa silaha kwa Kyiv zikiandamana na vikwazo kidogo, wengine wanafanya hivyo kwa masharti kuwa zitatumika ndani ya mipaka ya Ukraine.

Soma pia: Mawaziri wa EU waidhinisha vikwazo vipya dhidi ya Urusi

Lakini serikali ya Ukraine inasema wanajeshi wake wanahitaji kuyapiga maeneo ndani ya Urusi, kwa sababu Urusi inaanzisha mashambulizi kutokea nchini mwake.

Rais wa Ukraine Zelensky akiwa ziarani Ubelgiji
Ubelgiji imeahidi kuipa Ukraine ndege za kivita 30 aina ya F-16 katika kipindi cha miaka minne ijayoPicha: Piroschka Van De Wouw/REUTERS

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema katika kikao cha waandishi wa habari baada ya mkutano huo kuwa matumizi ya mashambulizi ya kujilinda dhidi ya maeneo ya kijeshi katika ardhi ya Urusi "ni kitendo halali chini ya sheria za kimataifa wakati inapotumiwa kwa usawa."

Soma pia: Zelensky awahimiza washirika kuongeza shinikizo kwa Urusi

Lakini pia ni wazi kuwa ni uamuzi wa binafsi wa kila mwanachama wa umoja wa ulaya. Borrell amesema hakuna anayeweza kumzuia nchi mwanachama kutoa silaha kwa Ukraine na kuwaruhusu Waukraine kuzitumia silaha hizo kuyalenga maeneo ya kijeshi ndani ya Urusi. Lakini pia Umoja wa Ulaya hauwezi kuwalazimisha kufanya hivyo.

Kwingineko, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anaunga mkono Ukraine kuruhusiwa kutumia silaha za Magharibi kuyashambulia maeneo ya Urusi katika ardhi ya Urusi. Akizungumza baada ya kukutana na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz karibu na mji mkuu Berlin, Macron amesema ni muhimu kuiruhusu Ukraine kuviangamiza vituo vya kijeshi ambavyo vinatumika kufyatua makombora yanayoelekezwa ndani ya Ukraine.

NATO ni nini?

Putin aonya dhidi ya "madhara makubwa"

Wakati huo huo, Rais wa Urusi Vladmir Putin amesema kuwa kutakuwa na kile alichokiita "madhara makubwa” kama nchi za Magharibi zitairuhusu Ukraine kutumia silaha zao kuyapiga maeneo ndani ya Urusi, kama inavyotaka Kyiv. Putin amesema barani Ulaya na hasa nchi ndogo, zinapaswa kufahamu zinachokichezea, akibainisha kuwa nchi nyingi za Ulaya zina maeneo madogo na idadi kubwa ya watu. Amesema hata kama askari wa Ukraine watafanya mashambulizi hayo, wauzaji wa silaha kutoka nchi za Magharibi ndio watakaowajibishwa.

Nchi za Umoja wa Ulaya zimegawanyika pia kuhusu kama watoa mafunzo ya kijeshi kutoka Umoja wa ULAYA wanapaswa kuruhusiwa kutoa mafunzo kwenye ardhi ya Ukraine, au kama askari wa Ukraine wanapaswa kupelekwa katika Umoja wa Ulaya kupewa mafunzo.

Rais wa Urusi Vladmir Putin
Rais Putin ameonya dhidi ya madhara makubwa kama Ukraine itatumia silaha za maghaeribi kushambulia ndani ya UrusiPicha: Mikhail Metzel/REUTERS

Putin pia amesema kuwa wakati anaamini watoa mafunzo ya kijeshi wa Magharibi wako tayari Ukraine wakihudumu kisiri kama mamluki, hatua yoyote ya nchi kuwatuma rasmi nchini humo itakuwa hatua nyingine ya kuongeza mvutano na hatua nyingine kuelekea mgogoro mkubwa barani Ulaya, kuelekea mgogoro wa kimataifa.

Baadhi wanahofia kuwa kuwapeleka askari nchini Ukraine kunaweza kuongeza kushiriki kwao katika vita na kuongeza hatari ya kuzuka mgogoro wa moja kwa moja kati ya Urusi na nchi za Magharibi.

Hata hivyo, mawaziri hao wa ulinzi waliweza kukubaliana kuhusu masuala ya kipaumbele kwa ulinzi wa Ulaya katika mkutano huo. Walitangaza uungaji mkono wa Umoja wa Ulaya usioyumba kwa Ukraine ambapo umoja huo utatumia nyenzo zote ilizo nazo. Miongoni mwazo ni mfuko wa nje ya bajeti unaoitwa Hazina ya Amani barani Ulaya ambapo Umoja wa Ulaya umeahidi dola bilioni 5.4 za msaada wa kijeshi kwa Ukraine. Serikali ya Uholanzi imesema itaongoza mpango wa baadhi ya nchi ta Ulaya ili kuipa Ukraine mfumo wa ulinzi wa angani aina ya Patriot.

Pia kwenye orodha ya vipaumbele vya mawaziri hao wa ulinzi ni kuimarisha uwezo wa kiviwanda wa Umoja wa Ulaya kutengeneza zana za kivita na teknolojia ya ulinzi.

afp, dpa, reuters, ap