1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Ushindi wa Museveni ni wa mashaka

17 Januari 2021

Uchaguzi uliokumbwa na vurugu na kuzimwa kwa intaneti ulishuhudia rais mkongwe Yoweri Museveni akitangazwa mshindi nchini Uganda. Ni ushindi wa mashaka, lakini vijana hawapaswi kukata tamaa, anaandika Iddi Ssessanga.

https://p.dw.com/p/3o2dL
Uganda Wahlen l Wahlplakate in Kampala
Picha: Baz Ratner/REUTERS

Kampeni za uchaguzi nchini Uganda zilikumbwa na vurugu kubwa za jeshi na polisi, mauaji na kamatakamata ya wagombea wa urais wa upinzani waliotuhumiwa kwa kukiuka masharti ya kuzuwia kusambaa kwa virusi vya corona, ambayo yanataka mikusanyiko isizidi watu 200.

Kisha, katika mkesha wa siku ya uchaguzi, mtandao wa intaneti ukazimwa -- katika ishara ya wazi kwmaba uchaguzi huo haungekuwa huru na wa haki. Rais Musevenialiamuru mtandao huo uzimwe baada ya kukasirishwa na hatua ya Facebook kuwafungia wafuasi wake.

Kwenye ziara za kampeni kote nchini, wagombea wa upinzani na wafuasi wao waliandamwa na maafisa usalama waliojihami kwa silaha. Mamia ya askari polisi na wanajeshi walikuwa wakiwafuatilia kila mahala na kuvunja mikutano yao.

Uganda l Unruhen im November während der Kampagne von Kyagulanyi
Wafuasi wa Bobi Wine wakitawanyika baada ya polisi kuwafyatulia mabomu ya kutoa machozi wakati wa kampeni, karibu na mji mkuu wa Kampala, Novemba 30, 2020.Picha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Licha ya hatari dhidi ya maisha yao, waganda waliodhamiria kuleta mabadiliko kwa kuchagua serikali mpya inayojali maslahi yao na kuondokana na utawala wa karibu miongo minne wa Museveni, walijitokeza kwa wingi kupiga kura.

Hata hivyo hali ilikuwa ya kukata tamaa baada ya hesabu ya mwisho ya kura kumpa Museveni ushindi wa asilimia 58 dhidi ya asilimia 34 za Bobi Wine siku ya Jumamosi.

Waganda wanajihisi kutelekezwa na kukosa msaada wakikabiliwa na miaka mingine mitano chini ya utawala wa Museveni, kiongozi pekee ambaye wengi wao ndiye wanaemjua.

Soma pia: Wine kupinga ushindi wa Museveni mahakamani

Wakati chaguzi zilizopita hazikuwa safi pia, lakini safari hii kulikuwa na viwango visivyokifani vya vurugu na mauaji, na upendeleo wa wazi wa tume ya uchaguzi.

Kutojali kwa mataifa ya magharibi

Chini ya Museveni, Uganda imekuwa mshirika muhimu wa mataifa ya magharibi katika mapambano dhidi ya ugaidi. Lakini katika utawala wake wa zaidi ya miongo mitatu, amefanya ukatili mkubwa pasipo kuwajibishwa na yeyote, pamoja na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, yote hayo yakichochewa na kutojali kwa mataifa ya magharibi.

DW Kiswahili | Iddi Ssessanga
Iddi Ssessanga ni naibu mkuu wa idhaa ya Kiswahili ya DW.Picha: DW/L. Richardson

Wakati Museveni akimtuhumu Bobi Wine kuwa wakala wa maslahi ya magharibi, mwenyewe aliziamuru ndege za kijeshi alizonunua kwa fedha za msaada kutoka mataifa hayo kuruka angani zikiwatishia wapigakura na wapinzani.

Marekani na Umoja wa Ulaya zimeunga mkono utawala wa Museveni kwa mamilioni ya pesa katika misaada, ambayo huitumia kuwakandamiza raia na kuimarisha utawala wake wa kidikteta huku akiendeleza ukosefu wa uwajibikaji.

Soma pia:Museveni ashinda muhula wa sita madarakani

Museveni haheshimu sheria, anajiona kuwa juu ya sheria, anahisi ndiye mmiliki halali wa rasilimali zote za nchi, huku akijifanya kuwa mdemokrat.

Baada ya vita vya ukombozi wa Uganda kutoka tawala za kidikteta na kuchukuwa madaraka, amebadili mwelekeo na kuigeuza nchi hiyo kuwa ya udikteta, ambao kiwango chake kinaweza kuwafanya madikteta waliotangulia wamuonee wivu.

Rais huyo wa muda mrefu ameweka wazi chuki yake dhidi ya uchaguzi. Mara kadhaa Museveni ametamka bayana kwamba kamwe hatokabidhi madaraka alioyachukuwa kwa mtutu wa bunduki kupitia makaratasi tu ya kura. Anatarajia Waganda wamshukuru kwa rekodi yake ya enzi za ukombozi na anajiona kama kwota pini ya baiskeli - ni ngumu kuondoa baada ya kuingizwa!

Uongo wa kiasa

Museveni alisema mwishoni miaka ya 1980, kwamba tatizo la Afrika ni viongozi wanaokaa muda mrefu madarakani, na mwaka 2001 aliahidi kwamba huo ndiyo ungekuwa muhula wake wa mwisho. Amekuwa akirejea ahadi hiyo tangu wakati huo, miomgo miwili baadae.

Soma pia:Bobi Wine: Jeshi limezingira makazi yangu, niko mashakani

Hivi karibuni, Museveni alisema haamini kwamba kiongozi mwenye umri wa zaidi ya miaka 75 anaweza kuwa na nguvu ya kuendelea kutawala, na aliahidi kuachia madaraka atakapofikia umri huo. Kisha nini? aliondoa ukomo wa umri kwenye katiba.

Wakati wa kampeni ya kura ya 2021, Museveni alisema kamwe hatokabidhi madaraka kwa wapinzani wake hata kama watamshinda. Kwanini sasa anapoteza rasilimali za nchi kuandaa uchaguzi?

Bobi Wine ayapinga matokeo ya uchaguzi

Matumaini bado hayajapotea

Kando na ushindi wa Museveni unaobishaniwa, chama chake tawala cha National Resistance Movement NRM, kilipata pigo kubwa katika uchaguzi huu kwa mawaziri kadhaa wa serikali kupoteza nafasi zao za ubunge.

Soma pia:Maoni: Uchaguzi wa Uganda ni fursa iliyopotea

Wapigakura waliwakataa mfano wa makamu wa rais Endward Ssekandi, ambaye alijikuta akikimbizwa hospitali baada ya sukari kupanda kufuatia mshutuko wa kushindwa na mgombea asiejulikana sana wa chama cha Bobi Wine.

Baada ya kupata zaidi ya wawakilishi 50 bungeni, chama cha upinzani cha Wine, cha National Unity Platform NUP, kimeibuka kuwa mshindi mkubwa zaidi. Chama hicho cha hasimu kijana zaidi wa Museveni sasa kinakuwa chama kikuu rasmi cha upinzani.