1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bobi Wine: Jeshi limezingira makazi yangu, niko mashakani

Sylvia Mwehozi
15 Januari 2021

Mgombea wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine, amesema jeshi limeingia nyumbani kwake na kuchukua udhibiti kamili akiongeza kuwa yumo katika matatizo makubwa.

https://p.dw.com/p/3nyjP
Uganda Wahl Robert Kyagulanyi Bobi Wine
Picha: Sumy Sadruni/AFP/Getty Images

Matokeo ya awali yameendelea kumweka mbele rais Yoweri Museveni huku akifuatiwa kwa mbali na Bobi Wine, ambaye amedai kushinda kwa mbali na kupinga matokeo yanayotangazwa na tume ya uchaguzi. 

Bobi Wine mwanamuziki ambaye aligeukia siasa amesema hayo kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter saa chache kabla ya kudai kuwa uchaguzi huo uligubikwa na udangayifu. "Hakuna hata mtu mmoja kati ya waliotuvamia anayezungumza nasi. Tupo katika matatizo makubwa. Tumezingirwa", Bobi Wine alieleza kupitia Twitter. Katika mkutano wake wa awali na waandishi wa habari, Bobi Wine amesema "chochote kinachotangazwa ni batili", huku akijitaja kuwa yeye ni "rais mteule". Zaidi anasema "namba kadhaa za simu ikiwemo yangu na mke wangu zimefungwa. Zimefungwa kinyume na sheria. Jeshi liko kila sehemu. Utawala wa kiimla upo katika mashaka makubwa. Nitahutubia taifa katika saa chache zijazo na pengine kutoa mwelekeo kwa watu wetu lakini mwishowe tunamuondoa dikteta".

Tume ya uchaguzi hata hivyo imesema mzigo umebaki kwa mgombea huyo kuthibitisha madai ya kuwepo na udanganyifu. Bobi wine amesema atawasilisha ushahidi hasa wa kura ambazo zilizopigwa kabla pamoja na hitilafu nyinginezo, pindi huduma ya intaneti itakaporejeshwa.

Bildkombo Yoweri Museveni und Bobi Wine
Rais Museveni na Bobi Wine waliochuana katika uchaguzi wa rais

Kulingana na matokeo ya awali yaliyotolewa na tume ya uchaguzi Museveni mpaka sasa amepata asilimia 65 na Bobi Wine anazo asilimia 27 ya asilimia 29 ya kura zilizohesabiwa. Matokeo kamili yanatarajiwa kutolewa  Jumamosi.

Mwanasiasa huyo anakusudia kufanya "maandamano ya amani" kupinga matokeo hayo yaliyotangazwa na kuongeza kwamba hatua za kisheria zitafuata. Wagombea nchini humo wana uwezo wa kupinga matokeo katika mahakama ya juu. Uchaguzi wa Uganda kwa kiasi kikubwa ulifanyika kwa amani lakin kampeni za uchaguzi huo zilitawaliwa na vurugu huku mwanasiasa huyo akikamatwa mara kadhaa kwa makosa tofauti na wanachama wa chama chake pia wengi walikamatwa.

Waangalizi wameripoti kupata ugumu katika kufuatilia uchaguzi huo, ikiwemo kupatiwa vitambulisho. Kiongozi mmoja wa kundi la uangalizi la nchini humo Charity Ahimbisibwe amesema kwamba yeye alikamatwa wakati akikutana na mwandishi wa habari hotelini jijini Kampala. Alipelekwa kituo cha polisi kabla ya kuelezwa makosa yake.

Tume ya uchaguzi imesema hadi kufikia sasa Museveni amejizolea kura zaidi ya milioni 2 na Bobi Wine naye amejizolea kura takribani milioni moja ikiwa ni asilimia 29 ya kura zilizohesabiwa. Huduma ya intaneti imeendelea kutopatikana hadi jioni hii baada ya serikali kuamuru ifungwe siku ya Jumatano, lakini tume ya uchaguzi imesema hilo halikuathiri mchakato mzima.