1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wine kupinga ushindi wa Museveni mahakamani

Yusra Buwayhid
17 Januari 2021

Kiongozi wa upinzani Uganda Bobi Wine amewasisitiza wafuasi wake kutofanya fujo, huku akipanga kupinga mahakamani matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Rais Yoweri Museveni.

https://p.dw.com/p/3o1yA
Uganda Wahl Robert Kyagulanyi Bobi Wine
Picha: Sumy Sadruni/AFP/Getty Images

Kiongozi wa Upinzani Uganda Bobi Wine amesema atapinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi mwengine tena Rais Yoweri Museveni mahakamani, huku akiwataka wafuasi wake kujizuia kufanya fujo.

Bobi Wine ametoa tangazo hilo Jumapili kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter kwenye ukurasa wa chama chake National Unity Platform (NUP), baada ya Tume ya Uchaguzi ya Taifa kumtangaza Museveni mshindi wa uchaguzi wa Alhamisi kwa kupata asilimia 58.6 ya kura zote zilizopigwa.

Kulingana na tume ya uchaguzi, Wine amepata asilimia 34.8 ya kura.

Soma zaidi: Museveni ashinda muhula wa sita madarakani

"Nachukua uamuzi huu kwa uchungu kuwasihi kujizuia kufanya aina yoyote ya fujo huku tukiwa tunajiandaa kuwasilisha mahakamani malalamiko ya kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyokuwa na kasoro za dhahiri kwa maslahi ya ushindi wa muda mrefu ujao na kwa Uganda," Wine ameandika Wine kwenye Twitter ya chama chake cha National Unity Platform (NUP).

Uamuzi huo ulichukuliwa baada ya majadiliano ya uongozi wa juu wa chama chake cha National Unity Platform NUP, Bobi Wine ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi.

Uganda Kampala | Präsidentschaftswahl: Wahlplakate
Uganda KampalaPicha: Sumy Sadurni/AFP/Getty Images

Visa vya udanganyifu wakati wa uchaguzi

Wine na chama chake wamedai kumefanyika "udanganyifu mkubwa" wakati wa uchaguzi wa Januari 14, ambao uliangaliwa kama uchaguzi wa kwanza Uganda uliotishia uongozi wa muda mrefu wa Museveni.

Museveni, 76, ni mmoja wa viongozi waliotawala kwa muda mrefu barani Afrika. Amekuwako madarakani kwa miaka 35, na kuibadilisha katiba ya nchi imruhusu kuwania muhula mwengine wa miaka mitano ya urais.

Uchaguzi huo ulifanyika chini ya kiwingu cha ghasia zilizoanza tangu wakati wa kampeni, huku kila siku kukiripotiwa visa vya matukio ya fujo.

Soma zaidi: Bobi Wine: Jeshi limezingira makazi yangu, niko mashakani

Nyumba ya Wine iliyoko mjini Kampala ilizingirwa na wanajeshi tangu Ijumaa jioni, hali iliyomuweka kiongozi huyo wa upinzani katika kifungo cha nyumbani.

Mtandao wa intaneti ulizimwa kote nchini humo kabla ya zoezi la kupiga kura kuanza na hali hiyo kuendelea hadi Jumapili.

Jiji la Kampala liko kimya Jumapili kuliko ilivyozoeleka, huku wanajeshi wa kulinda usalama wakiwa wanapiga doria katika kila barabara.

Vyanzo: (afp,dpa,rtre)