1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani ya Kusini

Magenge ya uhalifu yazidi kuitikisa Ecuador

Angela Mdungu
1 Septemba 2023

Mfululizo wa mashambulizi ya maguruneti na mabomu vimeutikisa mji mkuu wa Ecuador, Quito usiku wa kuamkia leo. Saa chache baadaye, wafungwa takribani 6 waliwashikilia mateka zaidi ya walinzi 50 wa magereza tofauti.

https://p.dw.com/p/4Vquk
Gari lililolipuka mjini Quito
Gari lililolipuka mjini QuitoPicha: Carlos Noriega/AP Photo/picture alliance

Matukio haya yanajiri  wiki kadhaa baada ya nchi hiyo kutikiswa na mauaji ya mgombea wa kiti cha Urais.

Mamlaka nchini humo zimesema, vitendo hivyo ni majibu ya magenge ya uhalifu yaliyotokana na kuhamishwa kwa baadhi ya wafungwa na hatua nyingine zilizochukuliwa na mfumo wa magereza wa urekebishaji wa wahalifu nchini humo.

Waziri wa mambo ya ndani wa EcuadorJuan Zapata amesema kati ya waliochukuliwa mateka kutoka kwenye magereza sita tofauti, hakuna afisa yeyote wa jeshi la polisi aliyejeruhiwa.

Uhalifu huo umetokea wiki tatu baada ya kuuwawa kwa aliyekuwa mgombea wa kiti cha Urais Fernando Villavicencio. Katika miaka ya hivi karibuni, mfumo wa urekebishaji wa wahalifu nchini humo umeshindwa kudhibiti jela kubwa ambazo zimekuwa vituo vya ghasia zilizosababisha vifo kadhaa. Umechukua hatua ya kuwahamisha wafungwa ili uweze kusimamia migogoro inayohusiana na magenge ya uhalifu.

Soma zaidi: Mkuu wa genge la uhalifu anayehusishwa na kuuliwa kwa mgombea urais Ecuador ahamishiwa jela nyingine

Kuhusu mashambulizi ya mabomu mjini Quito, bomu mojawapo lililipuka katika eneo ambako ofisi ya magereza ya urekebishaji wa wahalifu ilipokuwa awali. Mlipuko mwingine ulitokea mapema alhamisi nje ya ofisi za sasa.

Mkurugenzi wa uchunguzi wa kupambana na dawa za kulevya wa Equador, Jenerali Pablo Ramirez jana Alhamisi aliwaambia waandishi wa habari kuwa kati ya mabaki yaliyokutwa na polisi kwenye eneo la tukio mjini Quito ni pamoja na mitungi ya gesi, mafuta na baruti.

Waziri wa mambo ya ndani wa Equador Juan Zapata (aliyeshika kipaza sauti)
Waziri wa mambo ya ndani wa Equador Juan Zapata (aliyeshika kipaza sauti)Picha: Ecuador's Interior Ministry/AFP

Idara ya zimamoto kwenye mji wa Cuenca, katika gereza moja ambako maafisa wa polisi wanashikiliwa iliripoti kwamba bomu lililipuka Alhamisi usiku ilakini haikutoa maelezo zaidi ya kusema kuwa mlipuko huo uliharibu gari moja.

Mmoja wa mateka azungumza

Waziri wa mambo ya ndani wa Ecuador  Juan Zapata amesema mateka saba ni maafisa wa polisi na waliosalia ni walinzi wa magereza. Katika moja ya video ambayo Zapata aliithibitisha, afisa mmoja wa polisi aliyejiita Luteni Alonso Quintana ameomba mamlaka zisifanye maamuzi ambayo yatakiuka haki za watu walionyang'anywa uhuru wao. Ameonekana akiwa amezungukwa na kundi la askari na maafisa wa magereza na akisema kuwa takribani watu 30 wanashikiliwa na wafungwa.

Mamlaka za Ecuador zinahusisha ongezeko la vurugu kwa zaidi ya miaka mitatu sasa kuwa zilichochewa na kuuwawa kwa kiongozi wa genge  la Los Choneros, Jorge Zambrano aliyejulikana pia kama "Rascaina", mwaka 2020. Wafuasi wa genge hilo hufanya mauaji kwa mikataba,  unyang'anyi, kununua na kuuza dawa za kulevya na pia wanatawala magereza.