1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Lengo la usawa wa kijinsia halitaweza kufikiwa 2030

12 Septemba 2023

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imesema haitawezekana kufikia malengo ya usawa wa kijinsia ifikapo 2030 kutokana na upendeleo uliokita mizizi dhidi ya wanawake na hasa katika nyanja za afya, elimu, ajira na hata mamlaka.

https://p.dw.com/p/4WFkU
Wafanyakazi wanawake kote ulimwenguni bado wanakabiliwa na changamoto ya kupata ajira zenye staha, Umoja wa Mataifa umesema. Hii inawafanya wengi kubakia masikini.
Wafanyakazi wanawake kote ulimwenguni bado wanakabiliwa na changamoto ya kupata ajira zenye staha, Umoja wa Mataifa umesema. Hii inawafanya wengi kubakia masikini.Picha: AFP/Getty Images

Sehemu ya ripoti hiyo iliyopewa jina "The Gender Snapshot 2023" iliyoandaliwa na Shirika la Wanawake(UN-Women) na Idara ya Uchumi na Mahusiano ya Kijamii, zote za Umoja wa Mataifa imesema "Ulimwengu unawaangusha wanawake na wasichana."

Katibu Mkuu msaidizi Maria-Francesca Spatolisano ameuambia mkutano wa waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo kwamba "pengo la  kufikiwa kwa usawa linazidi kupanuka." Amevitaja vikwazo vya karibuni kwa wanawake na wasichana wanaoishi katika nchi masikini na zilizoathiriwa na migogoro, athari za mabadiliko ya hali ya hewa, na "upinzani katika suala zima la usawa na uwekezaji duni wa muda mrefu" ambao hata hivyo unazidi kupungua.

Ripoti ya kutathmini maendeleo kwa wanawake katika kufikia malengo 17 ya Umoja wa Mataifa ifikapo 2030 yanayohusiana na kuanzia masuala ya umaskini na elimu hadi mabadiliko ya hali ya hewa na haki za binadamu yanaonyesha dhahiri pengo lililopo la kijinsia na namna ulimwengu unavyoshindwa kujitoa kupambania usawa wa jinsia.

Katika lengo muhimu za kuondoa umasikini uliokithiri, ripoti hiyo imesema mmoja kati ya kila wanawake 10 hii leo ama asilimia 10.3 wanaishi na kipato cha chini ya dola 2.15 kwa siku, huu ukiwa ni umaskini wa kiwango cha juu kabisa. Na kama hali hii itaendelea, imesema asilimia 8 ya wanawake na wasichana duniani wataendelea kuishi katika umasikini mkubwa ifikapo 2030 na hasa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Refilwe Lwedwaba, msichana wa Afrika Kusini anayewafundisha wasichana wengine wa kiafrika kuwa marubani wa ndege na droni. Fursa kama hizi za kiteknolojia bado ni chache kwa wanawake.
Refilwe Lwedwaba, msichana wa Afrika Kusini anayewafundisha wasichana wengine wa kiafrika kuwa marubani wa ndege na droni. Fursa kama hizi za kiteknolojia bado ni chache kwa wanawake.Picha: Siphiwe Sibeko/REUTERS

Japo wasichana wanaongezeka mashuleni lakini hali bado ni mbaya.

Ingawa upatikanaji jumla wa elimu unaongezeka kwa wasichana na wavulana, ripoti hiyo imesema mamilioni ya wasichana hawajawahi kuingia darasani ama kumaliza elimu yao na hasa wanaoishi kwenye maeneo yenye mizozo. Na lengo la elimu linatoa Mwito kwa kila mtoto nchini Afghanistan kupata elimu bora ya sekondari na hasa baada ya utawala wa Taliban kuzuia elimu ya juu kwa wasichana.

Kwa mwaka huu wa 2023, hadi wasichana milioni 129 wanaweza kuwa nje ya mfumo wa elimu duniani, imesema ripoti hiyo. Kwa kiwango cha maendeleo cha sasa inakadiriwa wasichana milioni 110 watakuwa shuleni ifikapo mwaka 2030.

Na kuhusu lengo la kazi zenye staha, ripoti hiyo imesema bado wanaume wanapata kazi zenye staha kwa asilimia 90.6 ikilinganishwa na asilimia 61.4 ya wanawake wa kati ya miaka 25 hadi 54. Takwimu hizi za mwaka 2022 zinaonyesha pia kwamba wanawake walilipwa kidogo sana.

Na hata katika siku za usoni wanawake watakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na vizingiti vinavyowazuia sasa hususan kwenye nyanja za sayansi, teknolojia na uvumbuzi, katikati ya ukuaji wa kasi wa matumizi ya akili bandia ama Artificial Intelligence(AI).

Malengo katika uwanja wa siasa pia bado hayajafikiwa.

Na katika uwanja wa siasa, ni asilimia 26.7 tu wanawake kote ulimwenguni ambao ni wabunge, huku asilimia 35.5 wakiwa katika nafasi za serikalini. Ni asilimia 28.2 tu ya wanawake wanaoshika nafasi za kiutawala mahali pa kazi.

Ngozi Okonjo-Iweala, mkurugenzi mtendaji wa shirika la kimataifa la biashara, WTO na waziri wa zamani wa fedha nchini Nigeria, ni miongoni mwa wanawake wachache wanaoshika nyadhifa za juu miongoni ulimwenguni.
Ngozi Okonjo-Iweala, mkurugenzi mtendaji wa shirika la kimataifa la biashara, WTO na waziri wa zamani wa fedha nchini Nigeria, ni miongoni mwa wanawake wachache wanaoshika nyadhifa za juu miongoni ulimwenguni.Picha: Luca Bruno/AP Photo/picture alliance

Na kama hiyo haitoshi, wanawake na wasichana milioni 614 waliishi kwenye maeneo yenye mizozo mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 50 ikilinganishwa na 2017.

Soma Pia:Amnesty: Wanaharakati wanawake wanashambuliwa na kuuawa 

Ripoti hiyo ya UN Women na ECOSOC inaonya kwamba ikiwa ulimwengu utashindwa kutilia kipaumbele suala hili la kufikia malengo hayo 17, ni wazi yatakuwa hatarini. Aidha inatoa mwito wa ufadhili kwenye programu za kuhamasisha usawa wa jinsia na kutokuwepo kwa usawa wa ugavi miongoni mwa mataifa.

Kulingana na ripoti hiyo, kunatakiwa wastani wa dola trilioni 6.4 kwa mwaka ili kufadhili mataifa 48 yanayoendelea, yenye karibu asilimia 70 ya idadi jumla ya watu ili kufikia malengo ya usawa wa kijinsia katika maeneo muhimu na hasa katika kukabiliana na umasikini na njaa pamoja na kusaidia ushirikishwaji sawa wa wanawake kwenye jamii ifikapo mwaka 2030.