1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAfghanistan

Vyuo vikuu Afghanistan vyafunguliwa bila wanawake

6 Machi 2023

Vyuo vikuu vya Afghanistan vimefunguliwa Jumatatu, baada ya likizo ya majira ya baridi kali, lakini ni wanaume pekee ndio walifika vyuoni, kutokana na marufuku iliyowekwa na utawala wa Taliban dhidi ya wanafunzi wa kike.

https://p.dw.com/p/4OJEG
Fatima Haidari | Afghanischer Flüchtling gibt virtuelle Tours  von Heimat
Picha: Piero Cruciatti/AFP

 

Marufuku dhidi ya wanafunzi wa kike kusoma katika vyuo vikuu ni moja kati ya vikwazo kadhaa ambavyo utawala wa Taliban nchini Afghanistan umewawekea wanawake, tangu ulipochukua madaraka Agosti mwaka 2021. Marufuku ambazo zimelaaniwa pakubwa ulimwenguni kote ukiwemo ulimwengu wa Kiislamu.

''Inasikitisha sana kuwaona wavulana wakiruhusiwa kusoma katika vyuo vikuu huku sisi tukilazimika kusalia nyumbani. Huu ni ubaguzi wa kijinsia dhidi ya wasichana kwa sababu Uislamu unaturuhusu kupata masomo ya juu. Hakuna anayepaswa kutuzuia kusoma,'' anasema Rahela mwenye umri wa miaka 22, anayetokea mkoa wa Ghor.

Utawala wa Taliban uliweka marufuku hiyo baada ya kuwashutumu wanafunzi wa kike kwa madai ya kupuuza kanuni kali ya mavazi ya kike, na vilevile takwa la kusindikizwa na jamaa wao wa kiume wakielekea au wakitoka vyuoni.

Afghanistan Frauen Mädchen Ausstellung Bildung
Katika maonyesho mkoani Ghazni, wasichana wa Kiafghanistan wakidai kufunguliwa kwa shule na walionyesha shauku hii kwa ulimwengu kupitia michoro.Picha: Ali Shah Hemta

Soma pia: Wanawake Afghanistan waandamana mjini Kabul

Vyuo vingi, tayari vilikuwa vimeanzisha juhudi za kuwapokea wanafunzi wa kike na hata kuandaa madarasa yaliyotenganishwa kwa ajili ya maprofesa wa kike au maprofesa wanaume wenye umri mkubwa kuwafundisha wasichana.

Mohammad Haseeb Habibzadah, mwanafunzi wa sayansi ya kompyuta katika Chuo Kikuu cha Herat ameliambia shirika la habari la AFP kwamba ''inahuzunisha sana kuwaona maelfu ya wasichana leo wananyimwa haki yao ya elimu''.

Ameongeza kuwa wanajaribu kulitatua suala hilo kwa kuzungumza na wahadhiri pamoja na wanafunzi wengine ili kuwa na njia ambapo wavulana na wasichana wanaweza kusoma na wapige hatua mbele kwa pamoja.

Ejatullah Nejati, mwanafunzi wa uhandisi katika Chuo Kikuu cha Kabul ambacho pia ni kikubwa zaidi nchini Afghanistan, amesema ni haki ya msingi kwa wasichana kusoma, hata kama itabidi wasome peke yao katika siku tofauti, hilo si tatizo.

Soma pia: Taliban yazuia wanawake kusafiri peke yao.

Waheeda Durrani ambaye alikuwa mwanafunzi wa uandishi habari kule Herat, hadi pale alipopigwa marufuku kufika chuoni mwaka uliopita, amesema, serikali ya Taliban inataka wanawake wabaki bila elimu. Ameongeza kuwa, ''Ikiwa wasichana na wanawake wa Afghanistan watapata elimu, hawatakubali kamwe serikali inayonyonya Uislamu na Quran, watapigania haki zao na hiyo ndiyo hofu ya serikali''.    

Afghanistan Professor Ismail Mashal
Profesa wa Kiafghanistan Ismail Mashal alichana vyeti vyake kwenye TV, baada ya Taliban kuwapiga marufuku wanawake kusoma, na kuapa kupigania haki yao ya kupata elimu.Picha: AFP

Katika Chuo Kikuu binafsi cha Rana, wanafunzi wa kiume walirudi madarasani Jumatatu. Ebratullah Rahimi, mwanafunzi mwengine anayesomea uandishi habari amesema anasikitika kwamba dada yake hawezi kurejea darasani. Hata hivyo, anajaribu kusoma akiwa nyumbani.

Vyuoni, mabango na picha zinazoelezea jinsi wasichana wanapaswa kuvaavingali vimetundikwa kutani.

Maafisa kadhaa wa Taliban wamesema marufuku hiyo dhidi ya elimu kwa wasichana ni ya muda mfupi tu. Lakini licha ya ahadi yao, kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, wameshindwa kuwaruhusu wasichana kurejea katika shule za sekondari.

Soma pia: Wanawake wameathirika zaidi katika utawala wa Taliban

Uhalisia ni kwamba, kulingana na baadhi ya maafisa wa Taliban, viongozi wa kihafidhina wanaomshauri kiongozi mkuu wa Afghanistan Hibatullah Akhundzada, wana mashaka makubwa na elimu ya kisasa kwa wanawake.

Tangu waingie madarakani, maafisa wa Taliban pia wamewalazimisha wanawake kujiepusha kuonekana hadharani kwa umma. Wanawake wameondolewa kwenye kazi nyingi za serikali au wanalipwa sehemu tu ya mshahara wao wa awali, ili wabakie majumbani.

Umoja wa Ulaya wa washinikiza viongozi wa Taliban

Wanawake hawaruhusiwi kuzuru mbuga na bustani, maeneo ya mazoezi na ni sharti wavae hijabu wakiwa maeneo ya umma.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameshutumu vikwazo hivyo ambavyo Umoja wa Mataifa umetaja kuwa ubaguzi kwa msingi wa jinsia.

Jumuiya ya kimataifa pia imefanya haki ya elimu kwa wanawake kuwa suala la msingi kwenye mazungumzo kuhusu misaada na utambuzi wa serikali ya Taliban.

Hadi sasa hakuna nchi ambayo imeitambua Taliban kama serikali halali ya Afghanistan.

Chanzo: AFPE