1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Labour yatabiriwa kuwagaragaza Conservative uchaguzi UK

3 Julai 2024

Viongozi wa kisiasa nchini Uingereza wamefanya kampeni zao za mwisho Jumatano kulekea uchaguzi mkuu unaotazamiwa kukirejesha madarakani chama cha mrengo wa kushoto cha Labour, baada ya utawala wa miaka 14 wa wahafidhina.

https://p.dw.com/p/4hpqR
UK Salford | TV-Debatte zwischen Premierminister Sunak und Labour-Chef Starmer
Picha: Jonathan Hordle/ITV via Getty Images

Raia kote nchini Uingereza watapiga kura zao kuanzia saa moja asubuhi siku ya Alhamisi, huku uchunguzi wa maoni ukibashiri chama cha Labour kitashinda uchaguzi wake mkuu wa kwanza tangu 2005, na kumfanya kiongozi wake Keir Starmer kuwa waziri mkuu mpya.

Matokeo hayo yatashuhudia Uingereza ikirudi kwenye mrengo wa wastani wa kushoto baada ya karibu muongo mmoja na nusu wa serikali za mrengo wa kulia za chama cha Conservative.

Soma pia: Chama cha Labour chazindua ilani kuelekea uchaguzi Uingereza

Starmer amekuwa akiizunguka Uingereza siku nzima ya leo, kwa kufika England, Scotland an Wales katika juhudi za kuimarisha uungaji mkono wa chama cha Labour na kuonya dhidi ya uridhikaji wa kizembe katika saa za mwisho za kampeni.

"Ikiwa unataka mabadiliko, unapaswa kuyapigia kura," alisema Starmer mwenye umri wa miaka 61 wakati akizungumza na waandishi habari, na kuongeza kuwa hachukulii chochote kuwa jambo la kawaida.

Mdahalo wa TV UK| Rishi Sunak  na Sir Keir Starmer
Wawaniaji wa nafasi ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer wa chama cha Labour (kushtoto), na Rishi Sunak wa Conservative wakiwa kwenye mdahalo wa Televisheni Juni 26, 2024.Picha: Phil Noble/dpa/picture alliance

Wahafidhina wamekuwa wakicheza na hofu ya watu, wakionya juu ya kupandishwa kwa kodi na kudorora kwa usalama wa taifa endapo wataondolewa mamlakani, katika kile chama Labour kimeelezea kuwa hatua za mwisho za ukataji tamaa kujaribu kusalia madarakani.

Pia wamezidi kuwahimiza wapiga kura katika wiki za hivi karibuni kuzuwia uwezekano wa chama cha Labour kushinda "wingi uliyopitiliza" -- madai ambayo Labour inahofia yanakusudia kuathiri kiwango cha ushiriki wa uchaguzi huo.

Soma pia:Sunak na Starmer wakabiliana katika mdahalo wa mwisho kabla ya uchaguzi Uingereza 

Waziri wa Kazi na Pensheni Mel Stride, mmoja wa washirika wa karibu wa Sunak, alisema leo kuwa wapiga kura "watajuta" kuwapa Labour mamlaka "isiyo na kipimo" bila upinzani imara wa Wahafidhina.

"Ukiangalia uchaguzi, ni wazi kwamba Labour katika hatua hii wanaelekea kwenye ushindi wa kiwango ambacho pengine hakijawahi kuonekana katika nchi hii hapo awali," alikiambia kituo cha utangazaji cha mrengo wa kulia cha GB News.

Johnson: Siyo muda wa kukata tamaa!

Labour imefurahia uongozi thabiti wa alama 20 katika kura za maoni kwa muda wa miaka miwili iliyopita huku wapiga kura wengi wakielezea kutoridhishwa na namna chama cha Conservative kinashughulikia masuala mbalimbali yakiwemo gharama ya maisha, huduma za umma, uhamiaji na uchumi.

Soma pia: Rishi Sunak aitisha uchaguzi mkuu Uingereza

Lakini waziri mkuu wa zamani, Borris Johnson, aliyeondolewa madarakani na wenzake, akiwemo Sunak mwaka wa 2022 baada ya msururu wa kashfa, na ambaye hakuwepo kwenye kampeni muda wote, aliwataka wafuasi wa Conservative kutokata tamaa bado.

Great Britain London | Boris Johnson
Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Boris Johnson ameitwa dakika za mwisho kusaidia kampeni ya chama chake cha Conservative.Picha: Jessica Taylor/UK Parliament/PA Media/picture alliance

''Na kwa hivyo hakuna hata mmoja wetu anayeweza kukaa nyuma huku serikali ya Labour ikijiandaa kutumia wingi wa nyundo kuharibu mengi tuliyofanikisha, yale mlifofanikisha.''

Kinara huyo wa Brexit aliuambia mkutano wa hadhara Jumanne jioni kwamba Starmer atajaribu kuanzisha serikali ya mrengo wa kushoto zaidi ya Labour tangu vita vikuu vya pili vya dunia.

Mapema, kampuni ya uchunguzi wa maoni ya Survation ilibashiri kuwa Labour iko njiani kushinda zaidi ya viti 418 ilivyoshinda wakati Tony Blair alipohitimisha miaka 18 ya utawala wa Conservative mwaka 1997.

Chama hicho kinahitaji viti visivyopungua 326 kujipatia wingi wa kutosha kuunda serikali.