1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Labour kuzowa viti 410, Conservative yaambulia 131 tu

5 Julai 2024

Utabiri baada ya kura kupigwa nchini Uingereza unaonesha kuwa chama cha Labour kimeibuka na ushindi wa kishindo, huku kiongozi wake, Keir Starmer akielekea kuchukuwa nafasi ya Rishi Sunak kama waziri mkuu mpya.

https://p.dw.com/p/4htBv
Uingereza, Blackpool | Keir Starmer
Kiongozi wa Labour, Keir Starmer.Picha: Christopher Furlong/Getty Images

Matokeo yaliyopitiwa na mashirika mbalimbali ya habari yanaashiria kuwa chama cha Labour kinachofuata siasa za mrengo wa kati kushoto kimepata viti 410 kati ya 650 bungeni, huku wahafidhina wa mrengo wa kulia, Conservative, wakimudu kukusanya viti 131 tu, kiwango cha chini kabisa kwa chama hicho kwa zaidi ya miaka 100 sasa. 

"Kwa kila aliyeipigia kampeni Labour kwenye uchaguzi huu, kwa kila aliyetupigia kura na kukiamini chama chetu cha Labour kilichobadilika, ahsanteni." AliandikaStarmerkwenye mitandao ya kijamii.

Soma zaidi: Mamilioni ya Waingereza wapiga kura katika uchaguzi mkuu

Naibu wake, Angela Rayner, aliliambia shirika la utangazaji la BBC kwamba wametiwa moyo sana na matokeo, lakini asingeweza kusema zaidi mpaka pale matokeo yote yawe yamekusanywa na kutangazwa rasmi. 

Rishi Sunak  Sir Keir Starmer
Waziri Mkuu anayeondoka madarakani Uingereza, Rishi Sunak.Picha: Phil Noble/dpa/picture alliance

Katika kile kinachoonekana kama inuko jengine la wafuasi wa siasa za mrengo wa kati, chama cha Liberal Democrat kinatazamiwa kupata viti 61, na kukiondosha chama cha Wazalendo wa Scotland, SNP, kwenye nafasi ya tatu bungeni. SNP kinaelekea kupata viti 10 tu.

Nigel Farage akusanya viti 10

Kwa upande mwengine, chama kinachopinga wahamiaji cha Reform UK kinachoongozwa na mwanasiasa mwenye utata, Nigel Farage, kimepata viti 13, huku chama cha wazalendo wa Wales kikiwa na viti vinne na walinzi wa mazingira, the Greens, wakiwa na viti viwili. 

Kwa ushindi huu, Labour iko mbele kwa viti 170, ikiwa ni mara ya mbili ya ushindi wa Conservative kwenye uchaguzi wa mwisho wa mwaka 2019 uliokuwa umetawalliwa na ajenda ya Uingereza kujitowa kwenye Umoja wa Ulaya, Brexit. 

Nigel Farage
Nigel Farage wa chama cha Reform UK.Picha: Jeff Overs/BBC/Getty Images

Soma zaidi: Labour yatabiriwa kuwagaragaza Conservative uchaguzi UK

Kiongozi wa zamani wa Conservative, William Hague, ameiambia Times Radio kwamba matokeo yanayoendelea kukusanywa yatakuwa janga la kihistoria kwa chama chake, ambacho kwa matokeo yake ya mwisho mabaya yalikuwa viti 156 mwaka 1906. 

Lakini profesa wa siasa kwenye Chuo Kikuu cha London, Tim Bale, anasema matokeo haya si mabaya kama vile ambavyo ilitazamiwa yawe, na  kwamba sasa chama hicho kilichotandwa na vita ndani vya kiitikadi, kinapaswa kuchaguwa muelekeo kinaotaka kuuchukuwa. 

Kura kutoka vituo 40,000 kote nchini Uingereza zilianza kuhisabiwa mara tu baada ya vituo vya kupiga kura kufungwa na kuendelea hadi usiku wa manane, huku matokeo rasmi yakitazamiwa asubuhi ya Ijumaa (Julai 5). 

AP, AFP